Saturday, 10 August 2013

Ahoji maharage kuwa hatari kwa afya???




Ahoji maharage kuwa

 hatari kwa afya???

Wali kwa nyama

 

 Wataalaamu wa ubora wa vyakula kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wametakiwa kufanya utafiti makini kuhusu ubora wa vyakula kabla ya kutangaza madhara ili kuondokana na mkanganyiko katika jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd alisema hayo wakati akihutubia kwenye Kilele cha Maonyesho ya Wakulima (Nanenane) Viwanja vya Nzuguni Dodoma ambako yalifanyika kitaifa.
Balozi Idd alisema taarifa za harakaharaka kuhusu ubora wa vyakula zinawakanganya wananchi na kwamba lazima zifanyiwe utafiti wa kutosha kabla ya kuzitangaza.
Alitoa mfano wa taarifa iliyowahi kutangaza kwamba maharage ni hatari kwa afya ya binadamu, jambo ambalo alisema analitilia shaka kutokana na ukweli kwamba chakula cha aina hiyo kinaliwa na Watanzania wengi.
‘’Jamani maharage ni chakula kikuu kwa Watanzania wote, hivyo msitangaze madhara kwa harakaharaka bali ufanyike utafiti wa kutosha.
Kuhusu maonyesho wakulima, Balozi Idd aliwapongeza wakulima nchini kwa kazi kubwa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wakulima ili kukifanya kilimo kiwe na tija.
Awali, akizungumza machache kwenye hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Christopher Chiza aliwaonya wauzaji wa mbegu feki nchini akisema Serikali imejipanga kuwadhibiti vya kutosha.
Chiza alisema Serikali haitawavumilia hata kidogo wauzaji mbegu bandia za mazao mbalimbali yakiwamo mahindi, pamba na hata maharage na kwamba tayari wachache walishakamatwa na wanashughulikiwa.
Hata hivyo aliwataka wakulima kununua pembejeo kwenye maduka yaliyosajiliwa pekee ili kuepuka utapeli huo ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika.

No comments:

Post a Comment