Wadau washauri sheria itoe
fursa sawa kwa wananchi

“Tunaiomba Serikali kuongeza kifungu ambacho
kitaweza kuwatetea wananchi wa kawaida pindi wanapotaka kutumia maji kwa
ajili ya shughuli za kilimo,” alisema Pasiansi Mlowe kutoka Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mlowe alitoa maoni hayo alipotoa maoni yake kwenye
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Maji na Umwagiliaji iliyokutana na
wadau mbalimbali ili kujadili Muswada wa Sheria ya Umwagiliaji
inayotarajiwa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Bunge.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti
wa kamati, Peter Msola alisema kuwa, lengo la mkutano huo ni
kushirikisha wadau kutoa maoni yao kwenye vifungu ambavyo vina upungufu
ili viweze kufanyiwa kazi kabla ya kwenda bungeni.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa, muswada huu
unakidhi matakwa ya wananchi, jambo ambalo limetufanya tushirikishe
wadau mbalimbali ili waweze kujadili,” alisema Msola.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania
wanategemea shughuli za kilimo, mpaka sasa kuna zaidi ya hekta 44
milioni nchi nzima, kati ya hizo ni asilimia 24 tu ndizo zinazotumika
kwa ajili ya kilimo.
Alisema hekta 29.4 milioni zinafaa kwa matumizi ya
kilimo cha umwagiliaji,huku hekta 450,000 ndizo zinazotumika kwa
shughuli hiyo.
Alisema baada ya kufanya utafiti, wamebaini kuwa,
hekta milioni 2.3 zinafaa kwa kiwango cha juu,huku hekta milioni 4.8
zinafaa kwa kiwango cha kati, kutokana na hali hiyo, Serikali imepanga
kuboresha maeneo hayo ili yaweze kutumika katika shughuli hizo.
“Mkakati wetu ni kuhakikisha kuwa, sekta ya kilimo
inakua kwa kasi,jambo ambalo linaweza kuwaondoa wananchi wengi katika
hali ya umaskini,”aliongeza.
Alibainisha kuwa, kutokana na hali hiyo, Serikali
imeboresha muswada huo ambao wanaamini unaweza kukidhi matakwa ya
wananchi ambao wengi wao ni wakulima.
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Christopher Chizza alisema kuwa, ikiwa sheria hiyo itafanyiwa
marekebisho, wakulima wengi watakijikita kwenye kilimo cha umwagiliaji
na si kusubiri kilimo cha msimu wa mvua.
“Hivi sasa wakulima wengi wanasubiri kilimo cha
mvua za msimu, jambo ambalo limesababisha baadhi ya mikoa kuingia kwenye
umaskini wa chakula, kutokana na kupitishwa kwa sheria hii kutasaidia
kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujiunga katika kilimo cha
umwagiliaji,”alisema Chizza.
Aliongeza,licha Tanzania kulisha baadhi ya nchi zinazotuzunguka
zikiwamo za Rwanda, Burundi, Kenya na Sudan Kusini, lakini bado kuna
maeneo mengi ambayo hayatumiki.
Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa
kupewa elimu ili waweze kujua umuhimu wa kilimo hicho ambacho
kitawakomboa katika shughuli zao.
No comments:
Post a Comment