Urais si kuandikwa
sana gazetini
![]() |
ujumbe umefika |
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ametahadharisha wanaowania urais 2015 kwa kusema ushindi wa urais haupatikani kwa kuandikwa sana kwenye magazeti bali kura za wananchi ndizo zinazoamua.
Membe aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa
akizungumza kwenye Kipindi cha ‘Jenerali On Monday’ kinachorushwa hewani
kila Jumatatu na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.
Waziri huyo alialikwa kuzungumzia uchaguzi wa
Zimbabwe uliofanyika wiki iliyopita na ndiye aliyekuwa kiongozi wa
waangalizi kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kusini mwa Afrika, (Sadc).
Katika uchaguzi huo, Rais Robert Mugabe alitetea
nafasi yake kwa kuzoa kura 2,110,434 ambazo ni sawa na asilimia 61% ya
jumla ya kura zote, huku Kiongozi wa MDC-T, Morgan Tsvangirai akiambulia
34%. Tayari Tsvangirai amepinga matokeo hayo.
Akizungumzia kushindwa kwa Tsvangirai, alisema:
“Vyombo vya habari vilikuwa vinamkubali, alikuwa anaandikwa sana,
alikuwa na mashabiki wengi kwelikweli na alikuwa anajiamini...huyu
alijiamini mno kushinda, lakini hatimaye alianguka na hakuamini.
Uchaguzi Zimbabwe
Akizungumzia utata wa uchaguzi wa Zimbabwe kuwa
baadhi ya mataifa ya Magharibi, Marekani, Uingereza na Australia kusema
haukuwa huru na haki, Membe alisema: “Nilikuwa na Kundi la waangalizi
600 wa Sadc, walifanya kazi nzuri na walihakikisha mambo yanakwenda
vizuri.
Vikosi vya Tanzania DRC
Akizungumzia wanajeshi wa Tanzania wa kulinda
amani kwenye Mji wa Goma, nchini Congo, chini ya Umoja wa Mataifa
(Monusco), alisema vijana wanafanya kazi nzuri na wamefanikiwa
kuwakimbiza waasi wa M23 kutoka kwenye mji wao.
“Kule kuna makundi mawili; walinzi wa amani ambao
wanalindwa na kifungu cha sita na hawa hawapigani, wanailinda amani na
wapo wanaopigania amani. UN wanasema kama amani haipo, itafutwe na kisha
ilindwe, sasa hawa wako kwa kifungu cha saba.
Kuhusu uvumi wa kutekwa askari wa Tanzania na
majeshi ya M23, Membe alikanusha na kusema: “Hizi habari si kweli
kabisa. Hakuna kitu kama hicho kwani hawa wamekuwa wazuri kwa kupiga
propaganda...hata pasipoti inayotajwa ni kuundaunda tu ikatiwa ufundi
kwenye kompyuta,” alisema.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Rwanda, Membe alisema uhusiano wa nchi hizo mbili, uko imara, haujatetereka na kwamba wako wachache wanaotaka kutuchonganisha.
“Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete, urafiki wa
Tanzania na Rwanda uko imara na ninataka kusema Watanzania tuwe makini
na watu wanaotaka kutuchonganisha.
“Urafiki wetu na Rwanda ni wa siku nyingi,
tumefanya mengi kwa Rwanda, itakumbukwa pia tuliwahi kumtetea Kagame
kupelekwa Ufaransa kutokana na madai ya kuhusika kwake na kifo cha
aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana.
Dawa za kulevya
Akizungumzia kushamiri kwa dawa za kulevya, Membe
alionyesha masikitiko yake kwa wanaojihusisha na kusema kuwa zinaharibu
diplomasia ya Tanzania.
Membe ambaye alisema wanaotaka urais wapige vita
dawa za kulevya, alisema Tanzania ina sura nzuri katika medani ya
kimataifa, lakini tatizo la dawa za kulevya linatia doa
No comments:
Post a Comment