Saturday, 20 July 2013

Dawa za Kulevya;



Dawa za Kulevya; Wasanii 

wawakemea vijana wenzao



Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio yanayowahusisha wasanii na tuhuma za utumiaji na ubebaji wa dawa za kulevya , kitendo ambacho kinawashushia hadhi kwani si tu wanahatarisha maisha yao na watuamiaji lakini wanachafua jina la nchi.
Kuna baadhi ya wasanii kwa nia njema waliwahi kujitangaza na kuahidi kuacha ambao ni pamoja na Langa  Kileo ambaye alijitangaza kuwa anatumia na hadi anafikwa na umauti mwezi uliopita, alikuwa ameshaacha kutumia.
 Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye hadi sasa anapambana na tatizo hilo ingawa amefanikiwa kwa kiasi fulani lakini matumizi ya dawa hizo yalimrudisha nyuma na kumfanya aanze upya akirudi kwenye tasnia ya muziki.
Msanii mwingine aliyekuwa akiunda kundi la Nako 2 Nako Soldiers, Ibra Da Hustler, nae hivi karibuni ametangaza kuwa alikuwa anatumia  dawa za kulevya na sasa anapambana kuacha.
Msanii wa Ragga ambaye aliwahi kutamba mwanzoni mwa miaka ya 2000, Mark 2 B alitangaza kutumia na sasa anapambana kuacha.
Hao ni baadhi tu kuna wengi wanaofanya siri na kuna ambao wamepotea kabisa hata habari zao hazisikiki kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Kama hiyo haitoshi kuna wanaodaiwa kubeba  na wanafanya hivyo kwa muda mrefu sasa, kitu ambacho kimekuwa kikiwakatisha tamaa hata wazazi wenye watoto wao ambao wanataka kuwa wanamuziki, wakiamini kuwa watajiingiza katika matumizi ya dawa au kusafirisha.
Starehe iliwatafuta baadhi ya wasanii na kutaka wazungumzie hali hiyo na nini mitazamo yao hasa ukizingatia hiyo ni ajira yao.

Mwasiti Almasi
Anasema wasanii waangalie nafasi yao katika jamii kabla ya kufanya vitu ambavyo vinawaweka katika hatari ya kupoteza heshima yao na mashabiki wao, ambao wengi wao hawapendi matumizi ya mihadarati na hata wakati mwingine pombe kupita kiasi.
Anasema kuwa matumizi au ubebaji wa dawa za kulevya unawashushia heshima yao, kuwafanya waonekane  wahuni na kuzidi kuleta ugumu katika kuifanya jamii iuchukulie muziki na sanaa kwa jumla kama kazi nyingine.
Anaongeza kuwa ni vyema Serikali nayo ikatilia mkazo suala la kuhakikisha kazi za wasanii zinakuwa na ulinzi, kwa maana ya kumnufaisha mwanamuziki au mwigizaji mwenyewe tofauti na sasa ambapo wasanii wanategemea shoo pekee.


“Sanaa ni ajira Serikali ilitambue hilo na isimamie kazi za wasanii ili kuwapa nafasi ya kufurahia matunda ya kazi zao, naamini likifanyika hili litapunguza hata wimbi la vijana kujihusisha na ubebaji na utumiaji wa dawa za kulevya kwa kuwa watakuwa wanakipata kile wanachokifanyia kazi,” anasema Mwasiti.

Ommy Dimpoz
Anasema kuwa ubebaji na utumiaji wa dawa za kulenya ni hatari kwa kuwa una athari kwa pande zote mtumiaji, jamii na hata mbebaji.
Anaonyesha mshangao wake kwa kusema kuwa kwa nini vijana wanapoteza muda kufanya yale ambayo mwisho wake siku zote huwa ni mabaya, aliongeza sanaa nchini japo siyo sana, lakini inalipa na kama watafanya kazi kwa bidii watapata mafanikio bila kutumiwa na vigogo wa dawa za kulevya kuwa ‘punda’ wa kubebea au watumiaji.
“Ninachokiona hapa ni ukosefu wa ajira kwa vijana ndiyo maana wanakaa vijiweni na kushauriana kutumia na hatimaye wanakuwa mateja au makontena ya kubebea, lakini vijana nao watambue uhuru hauuzwi hivyo wautumie vizuri kujiletea maendeleo na siyo matatizo,” anasema Dimpoz.

Hussein Machozi
Anaanza kwa kuwaasa wasanii wa rika zote kwa kusema kuwa wao ni kioo cha jamii ambacho kikichafuka na wanaokiangalia wanachafuka pia, ambapo wakichafuka kuna aina mbili za uchafu wa upande wao  kwa kuiga mabaya yao au kwa upande wa kuacha kutumia  kazi zao.
Anafafanua kuwa kukubali kuwa kontena au kutumia hakupunguzi matatizo waliyonayo, bali ni kuyaongeza ambapo mwisho wa siku watakaoumia ni wao.
“Siamini kama kuna wasanii wenye mtaji mkubwa wa kubeba dawa au kuuza bali wanatumika na vigogo ambao wanajulikana lakini wao hawapatwi na madhara kwa kuwa hawatumii wala hawabebi na wala hawawashirikishi watu wa karibu nao kwa kujua ni hatari , inabidi wasanii na vijana kwa jumla wawe macho,” anaasa Machozi.

Hassan Tx Moshi
Anasema ni kitu cha ajabu sana kumwona kijana ana nguvu na kipaji kujiingiza katika masuala haya ambayo mara zote yamekuwa ni mwisho wa maisha ya wahusika, ama wafe au kupotea kwenye sanaa kabisa.
Anaongeza kuwa kuna starehe nyingi za kufanya na kuna njia nyingi za kuwafanya waende nje kuliko kujiingiza kwenye ubebaji au utumiaji, kwa lengo la kujitajirisha huku wakijua wanaharibu maisha yao.


“Tena afadhali nimepata nafasi ya kutoa dukuduku langu kwa wasanii wenzangu kukubali kuwa vifungashio vya matajiri wachache huku wakibaki kuwa masikini na kuwatajirisha wengine na wao kudhoofu,” anashangaa Moshi.
Aidha Moshi aliwataka wasanii wenzake kufanya kazi kwa bidii, bila kuingiza mambo ambayo yanawashushia hadhi yao na kubadilisha maisha yao kiafya kimaadili na kimtazamo.

Siwema Mohamed ‘Shilole’
 Anasema kuwa kukubali kubeba au kutumia wamejiweka katika wakati mgumu wanapokuwa na safari za nje ya nchi, kwani hawataaminika tena.
Anasema hakuna haja ya kuchungwa kila mmoja afahamu kuwa yeye ni nani na anatakiwa kuifanyia nini jamii, lakini siku zote lengo ni jema, kuwa itendee mema na si maovu kwa kuipotosha kwa namna yoyote ile.
“Tutapata shida tukitaka kusafiri kwani hakuna atakayekuwa na imani na sisi kutokana na kuvuma sana siku hizi, kuwa tunatumia au kutumiwa kubeba dawa na hivyo itakuwa ngumu kupita katika viwanja vya ndege vya ndani na nje kwa kuwa tutaonekana wahalifu,” anaasa Shilole.

Jokate Mwegelo
Anasema kuwa wasanii wasikubali kutumiwa kwa kuwa wanahatarisha maisha yao na jamaa zao pia, kwani kwa kubeba wanaleta sumu nyumbani kwa kutumia wanaweka sumu mwilini.
Anasema waache kutafuta fedha au maisha kwa njia za mkato, badala yake wafanye kazi na watapata wanachokitaka.
“Tatizo wasanii wanatamni vitu vya kwenye mitandao na kudhani ni rahisi kuwa navyo bila kujali hao walionavyo wamevipataje na kwa muda gani, wao wanataka kurahisisha na kuvipata matokeo yake wanajikuta mateja au wabebaji  hakuna mkato katika maisha wakaze buti watafanikiwa,” anasema Jokate.
Aidha Jokate anasema kuwa wanafanya kitu mwaka huu bila kujali miaka ijayo watataka kuwa nani na kwa kashfa kama hii, hawawezi kufikia malengo kwani jina likichafuka kulisafisha ni kazi.
“Huwezi jua siku za baadaye unataka kuwa nani lakini kwa kashfa kama hizi huwezi kufikia malengo yako, kwani ukifanya mazuri kusahaulika ni rahisi kuliko mabaya kila mmoja atakuwa anayakumbuka na hakuna atakayetaka kubeba lawama isiyomuhusu, watu watakutenga na kukukana kwa kila jambo,” anasema Jokate

No comments:

Post a Comment