Wednesday, 3 July 2013

"MZIGO MZITO APEWE MNYAMWEZI"

  1. Photo: Ulinzi Mkali wakati wa Mazishi ya Karume.
  2. Photo: MUSOBI MAGENI MUSOBI, HAKI, UTU, UADILIFU, UCHAPAKAZI, DEMOKRASIA NA UONGOZI WA KUTUKUKA.

HASARA YA KUWAPOTEZA WATU WEMA.

Tarehe 30 mwezi Mei Mwaka huu, Jiji la Mwanza na Taifa kwa ujumla lilishtushwa mno na taarifa za kifo cha shujaa na mzalendo wetu wa kupigiwa mfano, Mzee Musobi Mageni Musobi. Mzee Musobi, ambaye aliugua kwa muda mrefu maradhi ya Moyo na Kisukari, alifariki dunia Siku ya Jumatano ya tarehe 30 Mei 2012, majira ya Saa 2.00 usiku, Nyumbani kwake, Ngudu,
Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza.

Mara baada ya taarifa za kifo hicho ambacho kilimkuta mzee wetu huyu akiwa kijijini kwake Nguda, Wilaya ya Kwimba katika mkoa wa Mwanza kutangaa, huzuni, majonzi na masikitiko viliwaingia WanaKwimba, wanaMwanza na Watanzania wote kwa ujumla kwa kumpoteza mpigania Haki, Ukweli na Demokrasia kama Mzee Musobi. Pengo lililoachwa kwa kifo chake li dhahiri kwa Taifa hili. Busara,Hekima na Ushauri wake mwema ni miongoni mwa vitu ambavyo tulivihitaji zaidi katika nyakati zetu hizi zenye kugubikwa na Changamoto nyingi zenye kutishiwa Ustawi wetu kama Taifa.

Mzee Musobi amelitumikia Taifa hili kwa Uadilifu na Uchapakazi wa hali ya juu, athari nyingi za Utumishi wake wa kutukuka bado zingalipo kwa kizazi hiki kujionea. Maisha yake binafsi ni Kiigizo Chema kwetu cha namna Mtumishi wa Umma anavyopaswa kuishi hasa katika wakati huu ambao Maadili katika Utumishi wa Umma yameonekana kupotea kabisa.

Alikuwa Mnyenyekevu, Msikivu, Muadilifu, Rafiki wa wote, Kiongozi Mahiri na Mtu Mwema kwa watu, wengi wetu tutakosa vipawa vyake adhimu ambavyo ni adimu kupatikana kwa viongozi wetu wa zama hizi.

MFANO HAI WA KUIGWA, JUHUDI HAZIRUDI UTUTPU.

Mzee Musobi Mageni Musobi amezaliwa Aprili Mosi mwaka 1931 katika Kijiji cha Kinang'weli mjini Ngudu Wilayani Kwimba, alipata Elimu ya Msingi katika Shule ya Kakola iliyopo Wilayani humo na baadaye alipata Elimu ya Sekondari huko Dole mjini Zanzibar. 

Wakati ule wa Ujanani Mzee Musobi alihangaika sana katika kujiendeleza na kutafuta Maarifa Mbalimbali, Miongoni mwa Maarifa hayo ni Mafunzo ya Uhasibu na Ukarani, Elimu kwa njia ya Posta, Mafunzo ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Cambridge University mwaka 1968 na pia Mafunzo ya Utumishi wa Jamii katika Chuo cha Social Training Centre cha Nyegezi (Sasa SAUT).

Pamoja na kutokea katika Familia Masikini na iliyokosa Fursa, Musobi aliminyana kwa nguvu zake zote kutafuta fursa za kujiendeleza kwa kuwa aliamini ni elimu pekee ndiyo ambayo ingeweza kuyabadili maisha yake na maisha ya Jamii inayomzunguka. Jambo ambalo alifanikiwa sana katika maisha yake na kuwa mfano wa kuigwa kwetu vijana wa sasa.

MTUMISHI WA WATU MUSOBI, KIONGOZI MTENDAJI.

Musobi alizunguka sana wakati wa utafutaji wake wa elimu na maarifa, Mwaka 1950 ndipo alirudi rasmi Nyumbani kwao wilayani Kwimba na mwaka mmoja baadae (yaani mwaka 1951) alipata kazi ya ukarani (Area Secretary) katika Halmashuri ya Maswa chini ya Serikali ya Kikoloni, na baadae 1954 akahamia Halmashauri ya Kwimba kama Mhasibu.

Mnamo mwaka 1957 alihamishwa tena na kurudishwa kwenye ukarani tena katika Halmashauri hiyo hiyo ya Kwimba hadi 1961 alipoamua kuacha kazi na kujiingiza katika shughuli za ukulima huku pia akijiendeleza kimasomo kwa njia ya Poata. Mafanikio yake kwenye Kilimo yalichochea sana harakati zake za kuingia kwenye Siasa na ni jambo ambalo lilichangia sana kuonyesha namna alivyo mtendaji kwa Jamii yake wakati alipoomba ridhaa ya kutaka kuwatumikia.

Ilipofika mwaka 1965 Mageni Musobi Mageni aliamua kugombea Ubunge wa Jimbo la Mwamahimba wilaya ya Kwimba, katika uchaguzi huo Mageni alikuwa Kivutio sana kwa sababu ya ujana wake wa Umri wa miaka 35 tu tofauti na aliyekuwa akigombea naye ambaye alionekana ni Mzee sana. Alishinda kwa kupata kura 13,516 ikiwa ni takribani mara mbili zaidi ya kura alizopata mpinzani wake, Bwana M. Malaba aliyeambulia kura 6, 621. 

Usindi wake huo Mkubwa ulichangiwa zaidi na Kaliba ya Musobi ya kutopenda kujikweza na kujinadi kwa Elimu yake iliyokuwa kubwa kwa wakati huo bali alijinadi tu kwenye Kampeni za Kinyang'anyiro cha Ubunge kama Mkulima Mzawa wa Mwamahimba anayetaka kuwatumikia Wakulima wenzie, jambo ambalo lilimuongezea mvuto tofauti na mgombea mwenzie ambaye aliinadi sana elimu yake kubwa.

Alifanikiwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu mbili kuanzia Mwaka 1965 hadi mwaka 1975. Musobi atakumbukwa sana na watu wa Kwimba kama Mbunge ambaye amaeleta Maendeleo na Mafanikio makubwa Wilayani hapo kuliko Mbunge mwengine yeyote, zaidi akisifiwa kwa uendelezaji wa Sekta ya Nyumba na Majengo Jimboni hapo jambo ambalo baadaye lilichangia kupewa kwake Uwaziri.

Majengo kama Makao Makuu ya Wilaya ya Benki ya NBC (sasa NMB) wilayani Kwimba, Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na hospitali na Kliniki inayojitegemea ya watoto pamoja na soko Kuu la Ngudu ni moja ya Majengo ambayo yalijengwa chini yake, Majengo ambayo mpaka leo yameifanya Kwimba iwe miongoni mwa Wilaya zinazovutia zaidi nchini.

Mchango wa Mzee Musobi alipokuwa Mbunge wa jimbo hilo si huo wa Majengo tu, ni yeye yeye ambaye pia alipigania kuhakikisha wachimabji Madini Wadogo wa machimbo ya Mabuki yatoayo almasi safi lakini isiyojulikana nchini, wananufaika na uchimbaji wao. Wanahistoria wanaandika kuwa hakuna mbunge mwingine katika historia ya Jimbo hilo ambaye kawatumikia na kuwaletea Maendeleo watu wa huko kama yeye.

UZALENDO NA HURUMA KWA UMMA.

Wakati mmoja akihojiwa juu ya Sakata la kuongezeka kwa Mishahara, Posho na Marupurup yaliyofurutu Ada ya Wabunge wa sasa wa Tanzania alisema kuwa yeye alifanya kazi ya ubunge kutoka mwaka 1965 hadi 1975 lakini katika nyumba yake anayoishi hivi sasa hakuwahi kuwa na hata jiko la umeme kwa vile ilikuwa kosa kubwa kwa kiongozi kujilimbikizia mali.

Anasema mbali ya kukopeshwa magari, mwaka 1965 alipokuwa Mbunge alikuwa anapokea kiasi cha sh 1,166.66 kwa mwaka, ambapo kwa kila mwezi Mbunge alikuwa akipokea sh 100. Mbali ya wabunge na mawaziri, mshahara wa Rais wakati huo ulikuwa sh 6,000.

Musobi ana mengi ya kutufunza juu ya kuwatumikia watu, Mwaka 1966 yeye pamoja na Wabunge wenzake walionyesha Uzalendo kwa kukukubali kukatwa Shilingi 40 kwenye Mishahara yao ya kila Mwezi ili pesa hizo zirudi kuja kuchangia Miradi ya Maendeleo ya Wananchi wa Tanzania, ambapo Rais Nyerere naye aliupunguza Mshahara wake mpaka kufikia Shilingi 4000.

“Utaona hata Rais aliamua kutoa sh 2,000 kwenye mshahara wake kwa ajili ya kusaidia matatizo ya wananchi kwenye maeneo ambayo yalikuwa yakihitaji msaada,” alipenda kukumbusha Mzee Mageni kusisitiza haja ya Viongozi kuwa na huruma na Wananchi wao.

"MARAFIKI AMBAO HAWAJAKUTANA BARABARANI", HAKUNA "USHKAJI" KWENYE UTUMISHI WA UMMA.

Mzee Musobi amekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini wakati wa Utawala wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kazi ambayo aliifanya kuanzia mwaka 1972 mpka mwaka 1975. Ustawi wa Nyumba nyingi za Serikali ambazo zilitapakaa Nchi nzima kwa ajili ya Makazi ya Watumishi wa Umma ni Sehemu ya mambo mema yake, ilimuuma mno "Manyang'au" walivyopeana 'bure' Nyumba hizo ambazo yeye na Wazalendo wenzake walifanya jitihada kubwa katika kuzijenga.

Mzee Musobi Mageni Musobi na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 'hawakukutana barabarani', walikuwa ni marafiki na watu wenye kusuhubiana mno. Kwa kuonyesha namna walivyopendana na kuhusudiana waliunganisha Familia zao kwa kuwaoza(kuwaozesha) watoto wao Madaraka Julius K Nyerere na Letsia Musobi Mageni musobi (maarufu kama Letsia Nyerere, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema).

Mzee Musobi alikuwa Mtumishi muadilifu, mchapakazi na aliyezifuata hasa kanuni na taratibu za kazi. Siku zote hakuyaacha mahusiano ya ya kindugu na kirafiki yaliyokuwa kati yake na Nyerere yaathiri utendaji wake au yamfanye abweteke. Kwake hilo lilimfanya aongeze uchapakazi na kufanya hata yale ya ziada ili kuhakikisha malengo ya kumkomboa Mtanzania yanafikiwa, jambo ambalo limekuwa kinyume katika tawala za sasa.

MAAMUZI MAGUMU NA MATUNDA YA DEMOKKRASIA.

Mzee Musobi amefanya maamuzi mengi magumu, ikiwemo uchocheaji mkubwa wa Demokrasia hapa Nchini. Amekuwa sehemu ya Vuguvugu la Uanzilishi Demokrasia ya Vyama Vingi hapa Tanzania, amezunguka Nchi nzima akiwaelimisha Wananchi juu ya Haki zao mbalimbali za Kidemokrasia, mwamko wa utambuzi wa Demokrasia tulio nao Wananchi wengi kwa sasa ni sehemu ya Ufinyanzi wake.

Mwaka 1991 ndiyo kipindi ambacho aliamua iwe maisho wake kuendelea kuwa mkuu wa wilaya na akaomba kustaafu kwa hiari. Hata hivyo kwa iliyokuwa nafasi yake ya Ukuu wa Wilaya alishaona na kugundua Mapungufu na uozo mwingi ambao aliamini kwa dhati kuwa Serikali ya CCM haikuwa na uwezo wa kuviondoa. Jambo hilo lilimpelekea kuanza kujiweka pembeni na CCM na kujiingiza kwenye harakati za kutaka mageuzi ya Vyama vingi ili kutafuta chama mbadala cha Kuondoa uozo na mapungufu hayo.

Ni Mwenyekiti Mstaafu wa Taifa wa Chama cha Wananchi, CUF, Akijiunga na Chama hicho miaka ya Mwanzoni kabisa pamoja na Muasisi Mapalala. Mwanzoni Marehemu Mzee Musobi aliombwa akiongoze Chama hicho kwa kukaimu nafasi hiyo nzito mara baada ya sakata la kuondolewa kwa aliyekuwa Mwenyekiti na mmoja wa waasisi wake Bwana Mapalala.

Alishika Rasmi Mamlaka Kamili ya Uongozi wa Chama mara baada ya kuidhinishwa na Mkutano Baraza Kuu la Chama hicho kwa kupata kura 268 kutoka kwa Wajumbe 383 na alikiongoza Chama hicho kama Mwenyekiti wa Pili kuanzia tarehe 13 Julai, 1995 hadi alipong'atuka.

KUNG'ATUKA, JAMBO ZITO LINALOWASHINDA WENGINE.

Mzee Musobi Mageni Musobi amekitumika Chama hicho kama Mwenyekiti kwa muda wa Miaka minne, aliamua kung'atuka katika kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika Chama hicho kwa hiari yake na kwa heshima zote, Disemba, 1999 na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ambaye amebaki kuwa Mwneyekiti wa Chama hicho kutoka wakati huo mpaka sasa.

Ametumia Nguvu nyingi, Uwezo mkubwa, Uzoefu wa kutosha, Uongozi wa kutukuka na usiomithilika na Uchapakazi wa kupigiwa mfano katika kukijenga Chama hicho. Ni Kiongozi shupavu, ambaye alibeba jukumu la uongozi katika wakati mgumu kwa moyo wake wote, chini ya Misingi ya Nidhamu, Umoja, Uwazi, Uadilifu, na Demokrasia ya Kweli. Nguvu, hamasa na kukubalika kwa Chama hicho hapa Nchini ni Matunda ya Uongozi wake.

Amekiongoza Chama hicho kuvuka Vizingiti vingi mno, akitumia busara na hekima kuenenda na kuepusha Maafa kwa Wananchi hata pale yeye na Chama chake walipoonekana kuonewa.

Siku zote alitangaza ujumbe wa Amani, kwake Demokrasia ya Kisiasa haikumaanisha kuitoa kafara damu ya Wananchi wasio na Hatia. Akisimama imara katika kuhakikisha amani iliyokuwa ikichafuliwa makusudi na watawala walio walafi wa Madaraka haiondolewi kwa kuwa athari zake ni kubwa mno kwa watu wa chini. Musobi aliwapenda sana Watanzania.

URITHI MWEMA.

Kwa sababu ya Uzee alistaafu Siasa na kubaki kuwa Mshauri kwa Vijana wote bila kujali itikadi zao, akiwa mfano bora wa namna Jamii inavyopaswa kuandaliwa kushika Uongozi kutoka Kizazi kimoja hadi Kizazi kingine kwa kurithisha vimelea, hekima na busara za Uongozi kwa kizazi kipya cha Vijana.

Amekuwa Mwema kwa Jamii inayomzunguka, ameishi vyema na Watu wa kwao na akaonyesha Mapenzi yake kwao kwa kurudi kuishi nao Kijijini kwake Nguda Wilayani Kwimba, Mkoani Mwanza mara baada ya kustaafu, jambo ambalo ni nadra kuliona kwa Wastaafu wengi waliowahi kushika Madaraka makubwa kama yeye.

BABA WA DEMOKRASIA.

Amekuwa Mlezi mwema wa Familia yake, siku zote amekuwa akisisitiza Maadili, Wema, Ukweli, Demokrasia na Utu. Wajane wake wawili, Watoto wake 15, Wajukuu wake 28 na Vituu vyake 6 ni Mashahidi juu ya haya. Akiwa baba na babu mwenye upendo mno, huzuni ya watu wake ikithibitisha hilo wakati wa msiba na mazishi yake.

Ugwwiji wake wa Demokrasia ulipituka mipaka, akiiga mfano wa Mwalimu Nyerere wa kuruhusu na kuvumilia Mwanaye Makongoro kuwa Kiongozi na Mwanachama wa Chama tofauti naye. Lakini yeye akienda mbali zaidi kwa kumpokelea mwanaye Letcia Musobi Nyerere kadi ya chama tofauti na alichokiongoza yeye (Chadema), kadi ambayo ilikabidhiwa kwake na Ndugu Zitto Zubeir Kabwe apokee kwa niaba ya mwanaye huyo aliyekuwa Marekani wakati Operesheni Sangara ilipokuwa ikipita Wilayani hapo.

MUSOBI, VIATU VYENYE KUMPWAYA KILA ALIYEJARIBU KUVIVAA.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 1975 Mzee Musobi aliangushwa na mpinzani wake katika jimbo la Kwimba kwa sababu Wananchi wengi wa Kwimba waliona natumia muda mwingi kwenye Majukumu ya kitaifa kama Waziri kuliko kuwa Mbunge wao, Mbunge mpya aliyechaguliwa alikuwa ni Bwana Balozi George Maige Nhighula. Pamoja na Bwana Maige kumshinda Musobi kwa kura lakini hakuweza kuvivaa viatu vyake katika kuwatunikia na kuwaletea maendeleo wananchi na hivyo kiasi flani kufifisha kasi na misingi ya maendeleo ya watu wa Kwimba iliyowekwa na Musobi.

Juhudi za kaka yake, Mzee Moses Kiyungu kutaka kulichukua jimbo hili zilikwama aliposhindwa na Philip Bujiku Sakila mwaka 1985 na juhudi nyingine za mwanae Musobi, aliyekuwa Mhandisi Maarufu, Marehemu John Kiyungu Mageni nazo hazikufanikiwa. Hata Mwanawe Letcia naye alishindwa kwenye Kinyang'anyiro cha Ubunge wa Jimbo hilo na Mfanyabiasha Sharif Hiran Mansoor (CCM).

PUMZIKA KWA AMANI MUSOBI WA WATANZANIA, UMTU MASHUHURI MIONGONI MWETU.

Mzee Musobi Mageni Musobi amefariki Dunia akiwa na Umri wa Miaka 82, Mchana wa siku ya Jumatatu ya tarehe 3 mwezi Juni mwaka huu  amezikwa huko kijijini kwake Nguda, Wilayani Kwimba katika Mkoa wa Mwanza katika Mazishi ambayo yalihudhuriwa na Umati wa Watanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Haruna Lipuumba pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Musobi si wa TANU/CCM kwa kuwa alikuwa Waziri katika Serikali yao, Musobi si wa CUF kwa kuwa amekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama chao, Musobi si wa Chadema kwa kuwa ni Baba Mzazi wa Mbunge wao, Mzee Musobi Mageni Musobi ni wa Watanzania wote.

Tulimpenda sana lakini Mola wetu Muweza amempenda zaidi, Tulimhitaji sana lakini Mola wetu Muumba Mbingu na Nchi(Ardhi) amemuhitaji zaidi, Alikuwa Amana njema kwetu ambayo Mwenyezi Mungu alituazima kwa muda ili tuitumie duniani, Mola ameamua kuchukua Amana yake.

Mola Karima amlaze pema Mzee wetu Musobi Mageni Musobi.
  3. Photo: FRANK JOSEPH HUMPLICK, MSANII MASHUHURI ALIYEHAMASISHA HARAKATI ZA KUDAI UHURU.

UMEWAHI KUUSIKIA WIMBO HUU?.

"Tanganyika ikichangaruka, Uganda, Kenya na Nyasa zitaumana. Nasikia fununu wanavyoichanachana China, Kitisho! 

I am a democrat, I don't want communism, English, Yes, No I don't know, Kizungu sikijui. Wanyika msishindane na Watanganyika" 

Wakati wa harakati za kugombea Uhuru wa Tanganyika Miaka ile ya 50 jina moja lilitamba sana katika fani ya muziki, Jina hilo ni la Frank Humplink. Humplink alikuwa Mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule. Alikuwa akipiga muziki wake akishirikiana na dada zake wawili Maria Regina na Tecla Humplink.

Mashairi ya Wimbo huo hapo Juu yamemfanya Mzee Frank Humplick kukumbukwa sana kwa wimbo wake ambao ulikuwa ukiwasisimua sana wananchi. Wimbo Husika ulikuwa umesheheni ujumbe mkali wa kisiasa jambo ambalo lilikifanya chama cha TANU kuufanya kama vile wimbo wake rasmi kwani ulikuwa ukipigwa katika mikutano yake yote. 

Mikutano ya TANU ya siku za mwanzo ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti.

CHOTARA WA KICHAGA, "MSETO" WA MADADA NA MAKAKA.

Franz Yosef Humplick ndilo jina alilopewa Frank Humplick baada ya kuzaliwa katika shamba la baba yake huko Moshi, Baba yake Frank alikuwa Mhandisi wa Ujenzi wa Kiswisi ambaye alishiriki katika ujenzi wa reli ya Tanga hadi Arusha. Tarehe 3 April 1927 wakati ule wa Ukoloni ndio siku ambayo Gwiji huyu wa Utunzi wa Mashairi, Uimbaji na kupiga Vyombo alizaliwa. 

Wakati wa Ujana wake Frank alijulikana zaidi kama "Kijana wa Kichaga" kwa sababu Mama yake aliyejulikana kwa jina la Odilia Shayo alikuwa anatokea Kilema, Moshi mkoani Kilimanjaro. Frank pia alizaliwa na dada zake wawili Thecla clara na Maria Regina ambao hatimae alifanya nao kazi nyingi za muziki wao wakiwa waimbaji, yeye akitunga, akiimba na kupiga gitaa.

Wakati ule akisoma Majengo Middle School ilikuwa ni kawaida kumuona Frank akiendesha Baiskeli yake huku akiwa amefunga Gitaa lake kwenye Baiskeli yake.

MITAA INAONGEA, KIPAJI CHA KIPEKEE CHADHIHIRI.

Kipaji cha Frank na dada zake kilijidhihirisha siku za mwanzoni tu za Ujana wao, wazazi wao kwa kutambua na kuthamini Vipaji hivyo walijaribu kuwapa msaada katika kila hali ili kuviinua zaidi vipaji hivyo. 

Katika wakati husika fursa za kuvionyesha vipaji vyao kwa jamii ilikuwa ndogo sana, Frank na Dada zake walipata Umashuhuri sana kwa kuimba kwenye Sherehe kama vile Harusi, Ubatizo, Sikukuu na hata kuwaburudisha Marafiki zao tu Mtaani, Burudani ambayo waliitoa haikuwa na kifani na kwa muda mfupi tu wakawa gumzo katika Mitaa yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.

"KUTOKA", MUONGO MMOJA WA UMASHUHURI WA HALI YA JUU.

Frank alianza rasmi Umaarufu wa kazi ya muziki kwa kurekodi 1950, Akiwa Katika bustani iliyokuweko katika ghorofa la KNCU, Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro, alirekodi nyimbo chini ya Kampuni ya Galatone kutoka Afrika ya Kusini. 

Peter Colmore ambaye aliweza kugundua vipaji vya wanamuziki wengi kama Edward Masengo, Mathias Mulamba, Esther John kupitia Kampuni yake ya High Fidelity Productions, alianza kuzitangaza kazi za Frank na dada zake akitumia Kampuni yake ya Usambazaji ya "His Masters Voice Blue Label". 

Kazi za Ndugu hawa zilipata Umaarufu sana mara tu zilipoanza kusambazwa na kwa miaka zaidi ya kumi sauti ya Frank Humplick na dada zake ilitawala anga za Muziki za Afrika ya Mashariki. 

Kundi lao lililoitwa Frank na dada zake waliuletea ulimwengu nyimbo nyingi ambazo mbaya zaidi mara nyingi nyimbo hizo zimekuwa zikitambulishwa kama nyimbo za mwanamuziki mwingine kutoka Kenya marehemu Fundi K.

WIMBO WA HARUSI WA AFRIKA MASHARIKI, "VYA KALE DHAHABU"

Nyimbo zao nyingi zilipendwa na kuwapa Umashuhuri Mkubwa sana, Lakini wimbo ambao ulitamba zaidi na kuwafanya wajizolee Mashabiki kila kona ni ule wa "Harusi" ambao ilifikia kipindi uliitwa wimbo wa Taifa wa Harusi wa Afrika ya Mashariki.

Kuonyesha wimbo huo ulivyo na mvuto, unavyopendwa na usivyochuja ulikuja kurudiwa tena na bendi ya Afro70, chini ya Patrick Balisidya na pia The Mushrooms wakaurekodi tena na kuupa umaarufu mpya, kuufanya kuwa moja ya vibao vinavyopigwa hadi leo kwenye sherehe za harusi na hata wao nao kujipatia umaarufu na malipo makubwa japo haukumpa chochote Frank wala ndugu zake.

Frank na dada zake waliimba nyimbo kadhaa za Kichaga, kuna habari inasema Chief Thomas Marealle alimwomba Frank atunge nyimbo za Kichaga kwani wakati huo akina George Sibanda toka Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe) na Manhattan Brothers kutoka Afrika ya Kusini waliimba kwa lugha zao za Kishona na Kizulu ambzo zilivutia sana. Frank alitimiza kazi hiyo kwa kutunga nyimbo kama Wasoro na Kiwaro.

"YES NO", WIMBO WA KUMBUKUMBU ULIOTUPWA.

Kati ya nyimbo ambazo zinastahili ziwekwe katika kumbukumbu ya Taifa hili ni wimbo "Yes No" (ambao muendelezo wa Mashairi yake nimeuweka kule juu). Wimbo huu uliotugwa wakati wa mapambano ya kutafuta Uhuru wa Tanganyika. Ni wimbo ambao ulikuwa na mafumbo mengi na ulitumika kabla ya kila mkutano wa TANU na kutumiwa sana na wanasiasa wa wakati huo.

Pamoja na kutamba sana kwa wimbo huo na kutokea kupendwa mno na halaiki haikupita muda serikali ya kikoloni ikaelewa ujumbe mzito uliokuwemo katika wimbo huo ambao kimsingi ulikuwa unasema Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland (Malawi)(

Kwa ya Amri ya Gavana Sir Edward Twining ulizuia kupigwa tena Sauti ya TBC/RTD na msako wa nyumba kwa nyumba ulifanyika kutafuta nakala za wimbo za wimbo huo wa Frank Humplick.

NYIMBO ZAKE NYENGINE. 

Ukiachilia mbali Nyimbo zake hizo mbili ambazo zilikuwa maarufu zaidi nyimbo zingine za Frank na dada zake zilizotamba sana na zingali zinapigwa hadi leo katika sehemu mbalimbali ni pamoja na Chaupele Mpenzi, Mwalimu Shekinuru, Sisi kwa sisi, Hodi mimi mgeni, Kichupukizi, Bibi Maria Salome, Shida, Masuti Njiani, Pondamali Hujafa, Wanipenda Juu kwa Juu na Nyoka Kabatini ambayo ilikuwa Maarufu zaidi kwa Watoto.

BURIANI "MGOSI" FRANK JOSEPH HUMMPLICK, MSINGI WA MUZIKI WA DANSI AFRIKA MASHARIKI.

Habari za kusikitisha ni kwamba Frank Humplink hatunaye tena. Mzee Humplink alifariki dunia tarehe 25 mwezi Agosti 2007 huko nyumbani kwake Lushoto, mkoani Tanga, Sehemu ambayo alihamia na kuishi muda mwingi mwishoni tokea miaka ya 60.

Marehemu Frank aliacha mjane, watoto sita (watatu wa kiume na watatu wa kike), wajukuu kadhaa na kilembwe mmoja. Alizikwa wiki moja tokea kifo chake huko huko Lushoto Mkoani Tanga.

Habari za Msiba wake hazikutangaa sana Nje ya Mji wa Lushoto kama zilivyotangaa Nyimbo zake Mashuhuri, Vyombo vya Habari vya wakati huo aidha havikumkumbuka au kumjua kabisa au havikumpa uzito aliostahili kwa Mema yake kwa Taifa hili. NiGaeti moja tu la Serikali ambalo liliweka habari ndogo juu ya kifo chake siku kadhaa mara baada ya kufariki.

Mzee Ally Kleist Sykes ambaye ni mmoja wa Wanamuziki Wakongwe na Wa zamani anapenda kuonyesha Picha ambayo alipiga yeye, Joseph Humplick na Peter Colmore wakiwa Mjini Moshi miaka ile ya Mwanzoni mwa 50 kuonyesha namna harakati zao za siasa zilivyosaidiwa naye.

Frank Joseph Humplick amekufa lakini Muziki wake ni wenye kuvutia mpaka leo kwa jamii kusikiliza, Mashairi yake yenye Ujumbe na Mafunzo Maridhwawa ni burudani tosha kwa wasililzaji wake, Upigaji na mirindimo ya Gitaa lake vikiashiria namna alivyokuwa Mwanamuziki kamili kwa Mashairi, Sauti na Vyombo, huku Nyimbo zake na kauli zake za kimafumbo zikichochea na kushajiisha Uchapakazi, Ndoa, Furaha na Upendo.

Katika ulimwengu wa muziki Marehemu Frank Humplink anasimama kwenye safu moja na Magwiji wenzie kama Mzee Gabriel Omolo, Marehemu Fadhili William, Marehemu Fundi Konde, Marehemu Ahmed Kipande, Marehemu salum Abdallah na wengine wengi waliovuma katika miaka ya sitini. Ni hoja isiyo na ubishi kwamba majina kama hayo hapo juu ndiyo yanaweza kusemwa kuwa ni msingi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki.

Mungu ailaze roho yake Mahali Pema Peponi.
    · Share

No comments:

Post a Comment