Saturday, 27 July 2013

NASHANGAA MSHITAKIWA KUFUTUWA DHAMANA


 NASHANGAA MSHITAKIWA
 KUFUTUWA DHAMANA

SHERIA MSUMENO
Dar es Salaam. Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alishangaa kuona Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Pamela Kalala, amemfutia dhamana mshtakiwa bila kueleza sababu.
Msumi alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kupokea rushwa inayomkabili Hakimu Pamela Kalala, anayedaiwa kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mke wa mmoja wa washtakiwa ambao alikuwa akisikiliza kesi yao, Josephine Omar Wageb.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Sophia Gula, Msumi, alidai kuwa katika tarehe asiyoikumbuka Februari, mwaka jana, alipokea maelekezo ya kushughulikia barua ya malalamiko dhidi ya Hakimu Kalala.
Alidai kuwa maelekezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Mahakama za Wilaya hadi Mahakama ya Rufani.
Alidai kuwa maelekezo hayo yaliambatana na barua iliyoandikwa na Josephine, akimlalamikia Hakimu Kalala kufuta dhamana ya mumewe, na mazingira yasiyoridhisha ya uendeshaji wa shauri la mumewe.
Alidai kuwa aliitisha jalada la kesi hiyo namba 703 ya mwaka 2008 na kwamba baada ya kulipitia, pamoja na mambo mengine alibaini kuwa mshtakiwa alifutiwa dhamana bila sababu.
Alidai kuwa baadaye alimwandikia Jaji Mfawidhi muhtasari na maoni yake kwa maelekezo zaidi.
Wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Karoli Muluge, Msajili Msumi alidai kuwa wakati wakiwa katika mchakato wa kulishughulikia suala hilo, walisikia kuwa mshtakiwa alikuwa ameshafunguliwa mashtaka ya rushwa.
Alisema hata hivyo Josephine hakumwambia kuwa mshtakiwa alipokea rushwa kutoka kwake.
Wakati akihojiwa na wakili mwingine wa utetezi, Twaha Taslima, alidai kuwa kesi hiyo ilikuwa imefikia hatua ya mwisho na kwamba ilikuwa imeahirishwa mara kadhaa kusomwa hukumu.
Alisisitiza kuwa hukumu ya kesi hiyo ilikuwa haijawahi kusomwa ingawa ilionyesha kuwa washtakiwa walikuwa wametiwa hatiani wakisubiri kusomewa adhabu.
Msajili Msomi alidai kuwa katika jalada hilo kulikuwa na mkanganyiko mkubwa kiasi kwamba Jaji Mfawidhi Bethuel Mmila, alikusudia kumwita mshtakiwa ili kupata ufafanuzi wa mkanganyiko huo.


Alibainisha kuwa mkanganyiko huo ulikuwa ni hukumu iliyoandikwa kwa mkono ambayo ilionyesha kuwa washtakiwa walikuwa wametiwa hatiani na tayari wakiwa wameshahukumiwa adhabu.
Alihitimisha kuwa Jaji Mfawidhi alipomuuliza mshtakiwa sababu za kutokusoma hukumu hiyo, alichokijibu kilikuwa ni tofauti na alichokiandika.
Shahidi Lyimo alidai kuwa alipokea barua ya malalamiko dhidi ya mshtakiwa na kwamba alipomhoji, mshtakiwa alidai kuwa alikuwa akimfutia dhamana kwa kuwa alikuwa ameshamtia hatiani.

No comments:

Post a Comment