Raha, karaha ziara ya Rais Obama
Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Barack Obama amefanya ziara ya kihistoria nchini Tanzania, lakini ameacha mazuri na makovu.
Ziara ya kiongozi huyo nchini aliyewasili juzi mchana ikiwa ni mwishoni mwa ziara yake barani Afrika baada ya kuzitembelea Senegal na Afrika Kusini, ilikuwa na furaha na karaha zake nchini.
Rais Obama na ujumbe wake waliondoka jana saa 6:03 mchana kurejea Washington, Marekani kupitia Dakar, Senegal alipokuwa anatazamiwa kujaza mafuta kwenye ndege yake ya Air Force One.
Ilikuwa ni ya furaha kwa Watanzania wote, lakini ilikuwa karaha kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam.
Ujio wa Obama, ambaye ana asili ya Afrika, ulisubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi, wakitaka kumuona na kujua alichokuja kufanya.
Furaha
Moja ya mambo ya kufurahisha ni alipotaja vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania, ambavyo vinajumuisha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Katika eneo la miundombinu ya barabara licha ya kuwa tayari Marekani imeshasaidia ujenzi wa barabara ya Namtumbo-Songea, Mbinga, Horohoro na baadhi Kisiwa cha Pemba, itaendelea kutoa misaada zaidi.
Mpango wake wa kuisaidia Tanzania sekta ya nishati kupitia mpango wa Power Afrika ambao utafikisha umeme vijijini, ni jambo la kufurahisha na lilipokelewa kwa shangwe.
Mpango huo ambao utatumia dola 2.5 bilioni za Marekani (Sh4 trilioni) ni wa kati ya Marekani na nchi sita za Afrika; Tanzania, Ghana, Kenya, Liberia, Nigeria na Ethiopia.
Karaha
Pamoja na kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya furaha kwa Watanzania, pia ilikuwa na karaha ambazo zilisababisha mtiririko wa shughuli za kila siku kwa wakazi wa Dar es Salaam kukwama kutokana na ujio wake.
Kufungwa kwa barabara ya Nyerere, Mandela, Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi kulisababisha karaha kwa wananchi na kushindwa kwenda ofisini na pia kufanya biashara zao.
Watu walishindwa kutoka nyumbani kuelekea katika shughuli zao kutokana na magari kutoruhusiwa kupita barabara alizokuwa akitumia rais huyo.
Wafanyakazi wengi walishindwa kwenda ofisini kutokana na ratiba ya kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment