Wednesday, 3 July 2013

Ukweli kuhusu jeshi la Polisi, Ingawa hawapendi kuusikia.

Ukweli kuhusu jeshi la 

Polisi, Ingawa 

hawapendi kuusikia.

 


MKUU wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la
Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, ni
mweledi wa kuzungumza hasa pale ambapo
watendaji wake (polisi), wanapokuwa
wanatuhumiwa kwa makosa ya wazi.
Lakini wakati anapozungumza anasahau
kwamba, taarifa yake inaweza kuonekana ya
kujihami au kuupotosha umma na hata
kuvunjia heshima Taasisi anayoitumikia.
Wakati wa tukio la mauaji ya mwandishi wa
habari wa Channel Ten, lililowahusisha polisi,
Chagonja alizungumza na waandishi wa habari
akisema hakuna picha halisi inayoonyesha
marehemu Mwangosi aliuawa na askari wake,
kwamba picha zilizopo kwenye magazeti si
halisi, zimetengenezwa.
Hata hivyo, ushahidi wa picha pamoja na
Tume zote zilizoundwa baada ya tukio hilo,
ikiwemo ya Waziri wa Mambo ya Ndani Dk.
Emmanuel Nchimbi, Baraza la Habari
Tanzania (MCT), pamoja na ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora iliyoongozwa na
Jaji Kiongozi mstaafu, Mussa Kipenka,
zilithibitisha polisi kuhusika moja kwa moja na
mauaji hayo.
Katika tukio la ulipuaji bomu kwenye Uwanja
wa Soweto, ulipokuwa mkutano wa kisiasa,
Chagonja alirudia kosa lile lile la awali, akisema
wananchi wanahusika kumlinda aliyedhaniwa
kurusha bomu hapo.
Hivyo kufanya polisi wenye mafunzo ya
kutosha kuhusu ukamataji wa wahalifu,
kushindwa kufanya kazi waliyoisomea!
Lakini, hakuishia hapo, Chagonja alikwenda
mbali zaidi akisema katika uwanja huo
waliokota silaha pamoja na risasi na kwamba
risasi moja ilionekana ya moto ikiwa
imeonesha kutumika. Kwa ujanja uleule,
Chagonja akawaambia wananchi walijilipua
wenyewe.
Lakini wakati anasema hivyo, shuhuda nyingi
za watu waliokuwa kwenye tukio wakiwemo
wanahabari zinawatuhumu moja kwa moja
polisi kwamba ndiyo waliohusika kurusha
bomu hilo.
Maswali magumu ambayo yanamfikirisha
yeyote mwenye akili, ni polisi kuhusishwa na
vifo vilivyotokea. Lakini kubwa ni tuhuma za
mtuhumiwa kutoroshwa na gari la polisi
zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe.
Ushuhuda wa mtoto Abubakar Adam (11),
ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya
Mount Meru Arusha, kwamba kifo cha
mtoto mwenzake, Amir Ally (7) pamoja na
yeye kujeruhiwa vibaya vimetokana na
kupigwa risasi na polisi.
Wakuu wa polisi walikiri kupatikana kwa
maganda ya risasi katika eneo la tukio,
jambo ambalo linathibitisha nguvu nyingine nje
ya bomu iliyotumika katika uwanja huo.
Maswali magumu ambayo wananchi
wangependa kupata majibu yake ni kwa vipi
mtuhumiwa ambaye wananchi walimuona kwa
macho, lakini polisi na watu wengine wa
usalama wameshindwa kumkamata hadi leo?
Ni mbinu gani ya kisayansi inayoelekeza
askari waliopewa kazi ya kulinda usalama wa
wananchi, kuamua kuzima moto kwa kutumia
moto mwingine!
Chagonja atueleze, katika taharuki na
mashaka ya kila mtu kujaribu kuokoa maisha
yake mwenyewe katika tukio kama lile,
wananchi wanawezaje kuzuia polisi
kumkamata mhalifu? Hiyo nguvu waliipata
wapi?
Simulizi za waandishi wa habari waliokuwa
katika eneo la tukio, hazionyeshi kabisa
kuwepo kwa tukio wala dalili za wananchi
kuzuia polisi kufanya kazi yao, je polisi hao
waliamua kutumia risasi za moto kwa sababu
gani na kwa manufaa ya nani?
Rejea simulizi ya mwandishi wa habari wa
gazeti la Raia Mwema, Paul Sarwatt, Juni 19
-25 mwaka huu, hazionyeshi kuwepo kwa
upinzani wowote kati ya wananchi na polisi.
Kamishna Chagonja aseme, kwanini polisi
waliamua kutumia silaha za moto kwa raia
ambao hawakuwa wakihatarisha maisha ya
askari kama sheria inavyosema?
Ni vipi polisi watumie mabomu ya machozi
katika tukio kama hilo lenye taharuki na
mashaka makubwa?
Kamishna Chagonja asikwepe wajibu wake.
Atoe majibu yanayoeleweka kuhusu
mazingira yaliyosababisha matumizi ya silaha
za moto, mabomu ya kutoa machozi wakati
huo tayari kuna bomu limerushwa na
kusababisha mauaji na majeruhi ya watu.

No comments:

Post a Comment