Friday, 5 July 2013

Watoto kuzaliwa kwa wazazi watatu


Watoto kuzaliwa kwa wazazi watatu

 si wawili Mmoja!!!!


Ni ugunduzi mpya ambao unatarajiwa kupata upinzani kutoka kwa watu mbalimbali duniani
Wakati njia ya uzazi kwa upandikizaji wa mbegu ikiendelea kushamiri pia katika Tanzania, wanasayansi wameendelea kuvumbua njia zaidi za uundaji wa watoto ambapo sasa mtoto anaweza kuzaliwa na wazazi watatu.
Mbinu hiyo ya uzalishaji itatumia upandikizaji (IVF) ambapo vinasaba vya wazazi watatu vitachanganywa pamoja na kinasaba kimojawapo kitatumika kuharibu magonjwa ya kurithi.
Imeelezwa kuwa mtoto wa kwanza mwenye wazazi watatu anaweza kuzaliwa mapema mwaka 2015 baada ya utafiti  huo wa muda mrefu kuonyesha mafanikio mwezi Juni mwaka huu.
Wanasayansi wa Uingereza huenda wakaifanya  nchi yao kuwa ya kwanza kukubali  na kuunda sheria  ya uundwaji wa watoto hao wenye vinasaba vya wazazi watatu licha ya kuwepo kwa hofu ya watoto watakaotengenezwa kama mtindo.
Mchakato  huo wa uundaji wa watoto hao utajumuisha kuweka vinasaba katika yai la mama na mayai mengine kutoka kwa mwanamume mchangiaji ambapo mtoto atakayezaliwa atakuwa na wazazi wawili wa kike na mmoja wa kiume.

Kiongozi mkuu wa uvumbuzi huu, Profesa Doug Turnbull anasema mbinu ya uzalishaji huo itafanyika kwa kuchukua yai kutoka kwa mama na yai, jingine toka kwa mwanamke, ambaye atakuwa ni mchangiaji (donor).
Anaongeza,  mayai hayo yatachanganywa kabla ya kuondoa kiinitete au nyukilia(muundo wa seli unaobeba taarifa za urithi:vinasaba) kutoka yai la mama mchangiaji, kisha kuwekwa katika nyuklia za mama  asili  pamoja na mbegu za baba, kisha kuchavushwa.
Profesa Malise Kaisi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambaye ni Mtanzania wa kwanza kuzalisha watoto kwa njia ya upandikizaji (IVF) anasema kwa Tanzania bado tupo nyuma  mno kwa utalaamu huo  uliovumbuliwa hivi karibuni.
Kwanza, Profesa Kaisi anasema Tanzania bado haina mtaalamu wa masuala ya urithi na upandikizaji(embrologyst) hivyo ina safari ndefu kufika huko.
Anauelezea mchakato huo na kusema una nia ya kuondoa maradhi ya urithi ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na seli za nyuklia kutoka kwa mama.
‘Yai la mama linachanganywa na yai la mwanamke mwingine bila yeye kujua, pamoja na  mbegu za baba, kisha anaundwa mtoto ambaye hatarithi ugonjwa wowote toka kwa baba au kwa mama,” anasema Profesa
 Anaongeza kuwa kuna idadi kubwa ya watoto wanaorithi maradhi kutoka kwa wazazi wao hivyo njia hiyo pengine itasaidia kuondoa tatizo hilo.
 Anaeleza kuwa, maradhi ya misuli, moyo, utumbo yanarithiwa kwa kiasi kikubwa na kusababisha kizazi chenye watu wenye ulemavu au vifo vya watoto.
“Kitu cha muhimu hapa ni kuwa, uundaji huu utasaidia kuondoa kabisa maradhi yanayorithiwa katika ukoo,” anasema Profesa Turnbull.
 Dk Josh Noreh, Daktari Bingwa wa Masuala ya Uzazi na Mmiliki wa Kituo cha Upandikizaji cha Kenya(KIVF) anasema anafahamu kuwa mchakato huo bado haujakamilika bali upo katika majaribio ya maabara bado.

“Ninajua kuwa upo uwezekano huo, lakini mimi bado sijaweza kufanya hivyo lakini nikifika Uingereza mwezi Oktoba, nitajifunza na nitajaribu hapa Kenya na Tanzania,”

anasema Dk Noreh.
Mganga Mkuu wa Serikali ya Uingereza, Profesa Dame Davies anasema uvumbuzi huo una maana kubwa ya kuondoa uwezekano wa mtoto kupata maradhi ya kurithi ambayo mara nyingi husababishwa na mtoto kuzaliwa na wazazi wawili tu.
“Ni matokeo ya hali ya juu ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa watoto wasirithi Maradhi kutoka ukoo,” alisema.
 Profesa Davies, anasema madaktari nchini humo sasa wameanza mchakato wa kutunga sera ya kuzalishwa kwa watoto hao, kuichambua na kuunda muswada kisha ikiwezekana kuupeleka bungeni. “Kama wabunge wataikubali sheria hiyo mwishoni mwa mwaka 2014, mtoto wa kwanza anaweza kuzaliwa mwaka 2015 mwanzoni,” anasema Profesa Davies.
 Ingawa asilimia 99.8 ya vinasaba ikiwa ni pamoja na tabia zetu zinazoonekana zinarithiwa kutoka kwa baba na mama na kuhifadhiwa katika seli za nyukilia, kijisehemu kidogo cha vinasaba hivyo, huhifadhiwa katika  nyumba ya kuzalisha nguvu za seli(mitochondria) na hutoka kwa mama pekee.
 Hivyo basi, urithi unaopatikana toka kwa mama, unaoingia katika mitochondria, huathiri zaidi mtoto na ndiyo maana wanasayansi wametafiti njia hii itakayotumia wazazi wawili wanawake na mwanamume mmoja.
 Watafiti hao walipewa kiasi cha dola milioni sita katika kufanikisha utafiti huo ambao madhumuni yake makuu ni kuondoa magonjwa ya urithi au yanayotokana na familia kwa watoto na kwa vizazi na vizazi. Inatarajiwa kuwa kati ya watoto watano hadi kumi wenye afya watazaliwa na wazazi watatu kila mwaka.
 Mtoto mmoja kati ya 6,500 huzaliwa na maradhi ya urithi ambayo mara nyingi huwa ni matatizo ya kuona, kusikia, moyo, mapafu, ini na pumu hivyo njia hiyo itasaidia watoto wasipate maradhi kutoka katika ukoo.
“Ninafurahia mchakato huu na ninahisi kuwa tutaokoa watoto watano hadi kumi wasizaliwe na maradhi ya kurithi au vifo vya awali. Hiyo itafanyika bila kubadilisha sura au tabia zao na itawasaidia zaidi wagumba,” anasema Profesa Davies.

  Dk David King, Mkurugenzi wa Usimamiaji wa Vinasaba vya Ubinaadamu, anasema mbinu ya uzalishaji wa aina hiyo haina umuhimu na si salama.
Hata hivyo, baadhi ya makundi ya haki za binadamu na wenye imani kali, nchi za Ulaya wameupinga mchakato huo wakidai kuwa unaondosha dhana ya kiasili ya uzazi.

No comments:

Post a Comment