Wednesday, 14 August 2013

Hii siyo dini wala itikadi, ni uhalifu




Hii siyo dini wala

 

 itikadi, ni uhalifu


Wiki iliyopita Zanzibar kulifanyika tukio la kusikitisha baada
ya watu wasiojulikana saa moja usiku, kuwashambuliwa kwa kuwamwagia tindikali raia wa Uingereza, Kate Gee na Kirstie Trup wote wakiwa na umri wa miaka 18.
Shambulizi hilo lilifanyika katika eneo la Shangani katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Tukio hili ni mfululizo wa matukio kadhaa ya watu kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali hapa Zanzibar.
Baadhi ya matukio kwa mfano kumwagiwa tindikali kwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga na kumwagiwa tindikali kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, hatujapata kusikia kama kuna watu waliokamatwa na kufikishwa mahakamani.
Ni jambo la kusikitisha na linalovunja moyo kuona kwamba nchi yetu iliyokuwa ikisifika kwa hali ya amani, utulivu na ukarimu wa watu wake leo imekuwa midomoni katika vyombo vya habari vya kimataifa kwamba watu wanashambuliwa kwa kumwagiwa tindikali.
Tukiwa raia wema tuungane kwa nguvu moja na Serikali katika kuwatafuta na kuwafichua wote wanaohusika na kushambuliwa kwa raia hao wa Uingereza na wengine ambao wamepatwa na mikasa ya aina hiyo.
Tayari Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk imeshatoa kauli ya kuwaomba wananchi washirikiane na vyombo vya dola kuwafichua wahalifu waliotenda tukio lile.
Tunafarijika kuona kwamba Serikali imeahidi siyo tu kukomesha vitendo hivyo, pia kuanza kuratibu na kusimamia kwa makini zaidi biashara ya tindikali kwa kutunga sheria itakayoweka masharti maalumu.
Tukio hili linapaswa kutokuingiza hisia zozote zaidi ya uhalifu, maana siyo dini wala siasa inayoeleza mtu au kikundi cha watu kufanya vitendo vya kuvunja sheria kama kilichofanywa.
Zanzibar ni moja kati ya nchi zenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo pia ina historia ndefu ya dini za Uislamu na Ukristo. Hivyo ni suala lililowazi kuwa vitendo vya watu kumwagiwa tindikali ni vya kihalifu na hakuna budi tuvikatae kwa nguvu zote.
Zanzibar dini zote za Uislamu na Ukristo ziliingia mapema katika eneo hili na hakukuwa na matatizo miongoni mwa wananchi wake na pia utamaduni wa watu wa Zanzibar kwa karne nyingi ni wa kuvumiliana katika kila jambo.
Msikiti wa Kizimkazi ni uthibitisho usio na shaka kwamba katika kipindi cha mwisho wa karne ya 11 AD kuingia karne ya 12 AD Zanzibaar tayari ilikuwa na Waislamu wengi.
Hata hivyo, pengine walikuwepo watu ambao bado hawakusilimu. Ushahidi uliokuwepo katika kisiwa kidogo cha Mtambwe Mkuu Pemba umeonesha kuwa mnamo karne ya 11 AD kulikuwa na baadhi ya watu waliozikwa ambao hawakuwa wa miji ya Afrika ya Mashariki, walikuwa ni wafuasi wa madhehebu ya Sunii/Shafii.


Kule Pemba kuna mabaki ya msikiti wa kale unaokadiriwa kujengwa mwaka 1300 AD karibu na Ras Mkumbuu. Wanazuoni mbalimbali wanasema kwamba Uislamu ulikuwa unaenea kwa haraka zaidi katika maeneo ya Bahari ya Hindi kunako karne ya 14.
Kwa mujibu wa maelezo ya historia ya dini ya Kikristo Zanzibar iliyoandikwa na Dayosisi ya Kanisa la Kianglikana Zanzibar ni kwamba Ukristo kwenye Visiwa vya Zanzibar kihistoria unaweza kuzungumzwa tangu wavumbuzi wa Kireno wakiwa hapa, hata hivyo siyo rahisi kupata moja kwa moja mlolongo unaoonyesha hiyo historia.
Katika Mji Mkongwe, mji wa miaka 500, kuna makanisa mawili ya Kikristo, ambayo hayakujengwa mbali sana kutoka moja hadi lingine. Makanisa haya; moja la Kianglikana na lingine la Kikatoliki.
Huko Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Unguja, kuna kanisa pia la Kianglikana ambalo nalo ni miongoni mwa makanisa makongwe hapa Zanzibar.
Dayosisi hiyo inasema badala ya kuangalia haya makanisa kama ushahidi wa Ukristo mkongwe Zanzibar, ule ushahidi wa majina ya Kireno kwenye makaburi na vielelezo vinginevyo vinaonyesha kwamba Ukristo kwenye visiwa hivi ulikuwepo tangu enzi hizo za wavumbuzi wa Kireno.
Zanzibar hakuna udini, hakuna matatizo miongoni mwa waumini wa dini tofauti, Wazanzibari wote wanaishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana.
Matukio ya kushambuliwa kwa risasi viongozi wa kidini yanaitia doa nchi hii yenye historia ndefu ya uvumilivu wa kidini miongoni mwa watu wake.
Mfalme ambaye kwa wakati huo alikuwa Seyyid Sayyid Barghash bin Said Al-Busaid alivutiwa na aliamua kutoa saa kubwa, ili kuupamba mnara wa kengele ambao uliwekwa pembe ya Kusini Magharibi ya jengo la Kanisa la Anglikana Mkunazini, saa hiyo hadi hivi leo ipo. 
Ushahidi mwingine ambao unathibitisha uvumilivu wa kidini Zanzibar ni ule uamuzi wa Serikali ya Zanzibar ilipoamua kutoa stempu mwaka 1963 kuadhimisha historia ndefu ya uvumilivu wa kidini Zanzibar.
Picha zilizowekwa kwenye Stempu zilijumuisha Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Kanisa Kuu la Kristo, Msikiti wa Malindi, Msikiti wa Hujjatul Islam na Hekalu la Kihindi.
Kadhalika, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatuna matatizo kati ya Waislamu na Wakristo na hali hiyo inajidhihirisha katika maisha ya kila siku ya raia wa nchi hii.
Katika Tanzania, uvumilivu wa kidini unaweza kuupata katika nyumba za kupanga, Wakristo wengi wamepanga kwenye nyumba za Waislamu na Waislamu wengi pia wamepanga katika nyumba za Wakristo
 
 
Kwa upande wa ndoa ambalo ni suala nyeti sana hasa inapokuwa mume ni dini nyingine na mke ni dini nyingine, lakini hilo katika nchi yetu si tatizo kwani Wakristo na Waislamu wameoana.
Kwa mantiki hiyo, hakuna udini katika maisha ya kawaida ya Mzanzibari wala Mtanzania. Hawa ni wahalifu wasakwe hadi wakamatwe, ili Zanzibar iendelee kuwa salama kwa wakazi na watalii wanaoitembelea.

No comments:

Post a Comment