Wanawake ni waathirika wakubwa
maeneo ya kazi

Dar es Salaam. Kwa miaka mitatu iliyopita, Rehema Nduguru (50) anayeishi Mkoa wa Njombe alikuwa katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya ngono ikiwamo Ukimwi kutokana na kazi yake ya uhudumu wa baa.
Akitoa maelezo yake jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, Rehema anasema kutokana na kazi hiyo alikuwa akilazimika
kufanya ngono zembe ili kujiongezea kipato. Hata hivyo, anashukuru Mungu
hakupata maambukizi ya Ukimwi.
“Wakati tukifanya kazi hiyo, mimi na wenzangu
tulikuwa tukifanya ngono zembe, hasa na madereva wa magari ya mizigo
yanayoegeshwa karibu na baa tulizokuwa tukifanyia kazi,” alisema Rehema.
Hata hivyo, Rehema sasa ameachana na kazi hiyo na amepata msaada kutoka Shirika la Kazi duniani (ILO).
Kwa upande wake Mwajuma Sabuni anayefanya kazi
katika kiwanda kimoja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa)
analalamikia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa waajiri wao.
“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba
sasa. Kwa miaka miwili ya awali nilifanya kazi kama kibarua, lakini
baadaye nikaingizwa kwenye mkataba wa kazi na kuanza kukatwa mafao ya
uzeeni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), bila kupewa kadi ya
uanachama na mwajiri wangu. Hadi sasa sijui hatima ya pensheni yangu,”
anasema na kuongeza:
“Kwa jumla hali ya ajira katika kiwanda hiki ni
ngumu hasa sisi wafanyakazi wa kike kwani rushwa ya ngono iko nje nje.
Wasimamizi wa vitengo ndiyo wahusika na ukiwakataa ajira yako inakuwa
hatarini. Licha ya kuwepo kwa Chama cha Wafanyakazi (Tuico) kinachojua
kero zote hizi, bado hazijashughulikiwa. Naiomba Serikali iingilie
katika kwa kuchunguza madai haya kwani tunanyanyasika mno.”
Maelezo ya wanawake hawa yanawakilisha kilio cha
wafanyakazi wengi wanaonyanyaswa kijinsia kutokana na kazi zao. Wengi
hulazimika kujiingiza kwenye ngono zisizo salama, hivyo kuhatarisha
maisha yao hasa kwa kupata ugonjwa wa Ukimwi.
Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa
Ukimwi, hasa maeneo ya kazi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, wadau wanasema kuwa wanawake na wasichana wako kwenye hatari
zaidi ya kuathirika na ugonjwa huo na kwamba hatua stahiki zinapaswa
kuchukuliwa ili kukabilia na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi
Tanzania (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema kuwa makundi ya wanawake
walijitokeza kuomba msaada ili kujikwamua kimaisha na kujilinda.
“Hatari ya wanawake hawa kuathirika na Ukimwi ni
kubwa mno. Ni changamoto kubwa inayohitaji jitihada za kila mmoja wetu,”
anasema Dk Mrisho.
Wito wa ILO
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
nchini (Tucta), Hezron Kaaya anapendekeza mifuko ya hifadhi ya jamii
kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wanawake na wasichana wanaofanya kazi
zenye hatari ya maambukizi ya magonjwa ya ngono ukiwamo Ukimwi.
Kwa upande wake Justina Lyela, Mkurugenzi wa Sera
na Utetezi wa Chama cha Waajiri Tanzania(ATE) amewataka waajiri nchini
kuepuka kuwapunja wafanyakazi wa kike ukilinganisha na wanaume ili
kuwawezesha kiuchumi, hivyo kuwasaidia kuepuka maambukizi ya Ukimwi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Kijakazi Mtenga aliyemwakilisha Waziri Sophia Simba katika
mkutano huo, ametaka kuwepo kwa usawa wa fursa kama vile elimu na
rasilimali za uchumi hasa kwa wanawake ili kuepusha hatari ya maambukizi
hayo.
Hali ya maambukizi
Wito wa wadau hao umekuja wakati kiwango cha maambukizi kikionyesha kuwa kikubwa zaidi kwa wanawake.
Ripoti ya Tacaids inaonyesha kuwa maambukizi
kitaifa yamefikia asilimia 5.7 huku wanawake wakiwa na maambukizi ya
asilimia 6.8 huku wanaume wakiwa na asilimia 4.7.
Sababu kubwa ya maambukizi inatajwa kuwa ni
umaskini, kuhama, mila na desturi mbaya, mfano mimba za utotoni.
Nyingine ni kutokuwa na usawa, ulevi wa kupindukia na matumizi ya dawa
za kulevya.
Ripoti hiyo inapendekeza kuongeza kipato cha makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi.
“Baadhi ya wanawake waliohojiwa wamebainisha kuwa
hulazimika kurithiwa baada kufariki kwa waume zao ikiwa ni mila
inayowataka kufanya hivyo ili kulinda mali za marehemu.
Wengine wamesema kuwa hulazimika kukubali kufanya
mapenzi kwa kuogopa kufukuzwa au kukosa misaada kutoka kwa wanaume wenye
uwezo. Wahudumu wa baa na wafanyakazi wa ndani wamekubali kufanya ngono
ili kulinda kazi zao,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Upimaji unaongezeka
Kwa upande mwingine utafiti uliofanywa na Taasisi
ya Taifa ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMR), mwaka 2008 unaonyesha
kuwepo kwa ongezeko la watu wanaopima afya zao na kupata ushauri kuhusu
ugonjwa wa Ukimwi.
“Katika nchi nyingi, mwamko wa kupima VVU kwa hiari umeongezeka
kwa kasi kutokana na upanuzi wa tiba ya VVU. Katika Tanzania, uwiano wa
idadi ya watu waliowahi kipima umeongezeka kutoka asilima 15 hadi 32
kati ya 2004 na 2007,” inaeleza sehemu ya utafiti huo na kuongeza:
“Hata hivyo, mwelekeo wa kupima VVU kwa watu
walioambikizwa katika katika ngazi ya jamii unafahamika kwa kiwango
kidogo sana. Hii ni kwa sababu ni watu wachache sana wanaojua hali zao
za maamukizo ya VVU kabla ya Upimaji wa hiari na ushauri nasaha.”
Utafiti huo ulifanyika Kata ya Kisesa jijini
Mwanza kwa lengo la kuelewa kiwango ushauri nasaha unavyovutia watu
walioambukizwa VVU na kutoa taarifa muhimu kuanzisha mpango wa ‘matibabu
kama kinga’.
Wito wa ILO
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Shirika la Kazi
Ulimwinguni (ILO) kuhusu VVU na Ukimwi katika maeneo ya kazi ya mwaka
2010, ugonjwa huo una athari kubwa katika jamii na uchumi katika sekta
rasmi na isiyo rasmi, kwa wafanyakazi na wategemezi wao.
“Jukumu la ILO ni kuhamasisha kuhusu ugonjwa huo
katika ulimwengu wa kazi na haja ya kuongezwa kwa juhudi za kujikinga na
kupambana na ubaguzi na unyanyapaa kwa walioathirika,” inasema taarifa
ya ILO.
Inasisitiza pia umuhimu wa kupunguza kazi zisizo
rasmi kwa kuongeza zenye staha na maendeleo endelevu ili kufikia malengo
ya ulimwengu wa kazi bora bila maambuki ya VVU na Ukimwi.
No comments:
Post a Comment