Sunday, 30 June 2013

Azimio la Arusha





 Kwa ufupi
Azimio la Arusha lipitishwa na almashauri kuu ya TANU mwezi januari 1967 na kuthubitishwa na mkutano mkuu wa TANU mwezi na kutolewa mwaezi Februari 1967. Imani ya TANU siasa ya TANU ni kujenga nchi ya ujamaa.
Azimio hilo lilifafanua falsafa ya ukombozi wa kiuchumi na kijamii chini ya misingi ya Ujamaa na Kujitegemea kama lengo la muda mrefu kwa Watanzania.


 Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere 

lilihitimishwa katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam wiki iliyopita, Ijumaa 13 Aprili 2013. Miongoni mwa mambo ambayo yameendelea kutawala vinywa vya watoa mada na wachangiaji mbalimbali ni kupoteza mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yetu na Azimio la Arusha.

Azimio hilo liliifanya Tanzania Bara kufuata Sera za Ujamaa na Kujitegemea zilizolenga kuleta usawa wa kijamii, kuondoa matabaka ya kiuchumi, kulipa dola hodhi ya njia kuu za uzalishaji mali. Kwa ufupi, sera zile zililenga kuuweka utu wa mtu mbele kabla ya vitu.
Mimi ni miongoni mwa wale ambao hawakukulia enzi za Azimio hilo. Kwangu mimi, kama ilivyo kwa Watanzania wengi vijana ambao ni takriban nusu ya Watanzania wote, lile kwetu ni historia.Kama taifa, leo tunakabiliwa na changamoto tele ambayo baadhi ya wanazuoni wamekuwa wakijenga hoja kwamba likirudishwa Azimio lile litakuwa mwarobaini kwa changamoto na matatizo yanayotukabili.
Uzito wa changamoto zenyewe, ukubwa wa matatizo yetu umeongeza kilio cha hao waliao nyikani, wakipaza sauti kwamba Azimio lirudishwe.
Azimio la Arusha na misingi yake ilirithiwa na makubaliano ya viongozi wa chama na Serikali waliokubaliana “kulegeza” masharti kutokana na maombi ya viongozi kuwa maisha yalikuwa magumu.Tangu mwaka 1992, nchi ikaanza kufuata mfumo wa sera za kiliberali kwenye nyanja zote za kuu za maisha yetu kama taifa. Waliofanya mabadiliko hayo walinufaika na Azimio lile moja kwa moja na wale wanaopigia chapuo lirudishwe pia walinufaika nalo.
Sera za uliberali wa kiuchumi na kisiasa ambazo zilishuhudia Serikali ikijitoa kwenye uendeshaji na umiliki wa njia kuu za kiuchumi, mashirika ya umma yakabinafsishwa, mengi kwa bei za hasara, kuanzishwa kwa utaratibu wa kuchangia gharama kwenye huduma mbalimbali za jamii kama vile elimu na afya.
Hali ingelikuwaje leo kama ubinafsishaji ungeliendeshwa vizuri? Je, mahitaji ya kufufuliwa kwa Azimio la Arusha bado yangelikuwapo kwa kiasi gani? Je, kipi ni tatizo zaidi kati ya sera hizi za uliberali wa kiuchumi au namna namna ambavyo zinaendeshwa hapa kwetu? Je, Azimio likirudi leo litakuwa mwarobaini  wa haya?
Tanzania leo, ni nchi yenye hali duni kiuchumi, pamoja na rasilimali tele tulizonazo. Bado ni nchi inayoishi kwa mikopo na misaada ya hali na mali kutoka kwenye nchi zilizopiga hatua kimaendeleo na pia kutoka kwenye taasisi na mashirika ya kifedha duniani mathalan Benki ya Dunia na Shirika la fedha Duniani (IMF).
Hata enzi ya Azimio la Arusha, nchi yetu ilikuwa ni miongoni mwa nchi maskini kabisa, ikitegemea misaada. Kama kweli Azimio la Arusha lingekuwa ni mwarobaini kwa nini hatukuendelea?
Azimio lilianzishwa wakati wa TANU likafia mikononi mwa CCM.Kesho kikitawala chama kingine  kisichofuata sera za kijamaa (sera ambazo hata CCM wenyewe wameziweka kando katika vitendo ila maneno na makaratasi tu). Je, chama hicho kitaona umuhimu wa kulirudisha?  Azimio lilisaidia kutuunganisha Watanzania, viongozi na wananchi wote waliitana ‘ndugu’ , lilileta usawa wa kijamii. Uzalendo wetu ulikuwa juu kwa taifa hili. Azimio lilifanikiwa kwenye masuala ya kijamii na kufia kwenye mfumo wa chama kimoja, enzi ya ‘analojia’, litamudu kuiokoa nchi yetu na kizazi ambacho kwa sababu mbalimbali kinawaza kuihama nchi kila uchao? Litakuwa mwarobaini wa kizazi hiki cha zama za kidigitali?
Wanasiasa wetu hawaishiwi kashfa, kuanzia zile za kutumia madaraka yao vibaya, mpaka tuhuma za rushwa. Hatari zaidi ni kwamba taasisi nyeti kabisa kwa ustawi wa taifa letu zinalalamikiwa na kutuhumiwa kwa rushwa kama vile polisi, mahakama na hospitali na vituo vyetu vya afya. Imekuwa kawaida kuyaona magari ya taasisi na mashirika ya umma  yakitumiwa isivyo na katika muda usio.
Je, Azimio la Arusha litaiokoa jamii ya namna hii, jamii ndumilakuwili, yenye pande mbili tofauti kama Janus-mmoja wa miungu ya kale ya Kirumi? Ni kwa kiasi gani taifa hili linakerwa kwa dhati na rushwa? Au pengine ni yale aliyopata kuandika mwandishi nguli wa Afrika,marehemu Chinua Achebe, kwamba, ‘jamii hii inachukia rushwa kwa vile tu wale wanaonyoosha vidole na kupaza sauti hawajapata fursa hizo za kuliibia taifa’?
Gharama za maisha zinazidi kuwaelemea wananchi wa kawaida.
Je, Azimio la Arusha litamrudishia mkulima wa nchi hii heshima yake na kusaidia kumkwamua kiuchumi? Litadhibiti kupanda kwa gharama za maisha kiholela?
Mwenendo wa Bunge letu sasa ulivyo ni wananchi wachache wakiwa na akili zao timamu watasema kwamba wawakilishi wao wanafanya Azimio la Arusha litawarudisha kwenye mstari mnyoofu wabunge hawa? Je, litawafanya waone aibu kwa wanayoyafanya-kama manyani wa Adili?



No comments:

Post a Comment