Mzindakaya: Tunaandaa
viongozi wavivu
![]() |
kubomu |
MWANASIASA mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chrisant Mzindakaya, ameponda malumbano ya baadhi ya viongozi wa sasa na wastaafu akisema ni dalili ya taifa kupata viongozi wavivu siku zijazo.
Mzindakaya ambaye ni mbunge wa zamani wa Kwera, alitoa angalizo hilo jana wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa changamoto za kuongoza mabadiliko ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Mzindakaya alifafanua kuwa imefika wakati kiongozi anayeingia madarakani anaogopa kukalia kiti alichokiacha mtangulizi wake.
“Taifa linaelekea kuzalisha viongozi wavivu kwa sababu watu wote wamekuwa wanasiasa, hakuna kiongozi wa kuamuru. Wanakumbatia wageni na kuwaacha wazawa.
“Huko tunakokwenda watoto wetu watakuja kufua chupi za wageni… tunataka kuwa wazuri kuliko Papa huko Roma, nchi gani isiyowezesha wananchi wake! Hakuna kitu kama hicho duniani,” alisema.
Naye mbunge wa zamani wa Ukerewe, Getrude Mongella, alisema siku hizi hakuna heshima kwa viongozi kiasi cha wananchi kudiriki kumtukana Rais.
“Watanzania sasa wamekuwa kama kambale wote wameota sharubu… hawaheshimu mamlaka zilizopo kisheria, ipo haja ya kujifunza na kuwafundisha wengine zaidi.
“Naamini wapo viongozi waliopata uongozi tu kwa bahati mbaya ambao hata historia ya nchi hii hawaijui,” alisema Getrude.
Wanasiasa hao walisema hayo muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kufungua mkutano huo na kuwaeleza washiriki kwamba mabadiliko ni safari.
Pinda alisema ni lazima viongozi wawe tayari kufanya uamuzi mgumu ikiwemo kurudi nyuma kwa nia njema na kuangalia walipokosea ili mradi wasipoteze lengo.
Kwa mujibu wa waziri mkuu, upo wakati mabadiliko hukosa kuungwa mkono, hupingwa, huambatana na hatari na kuhitaji muda mrefu kutoa matokeo ili kuthibitisha umuhimu wake.
“Mabadiliko ni safari inayofuata uelekeo wa kimkakati uliokubalika kama ilivyo safari yoyote ambayo inaweza kukumbana na matokeo yasiyotarajiwa na hata kusababisha migogoro.
“Hiyo ndiyo sababu ya uongozi wenye ufanisi hasa katika nchi maskini ambapo inahitaji msimamo ili kutekeleza na kuyafikia mabadiliko yaliyokusudiwa,” alisema Pinda na kuongeza kwamba viongozi muda wowote lazima wawe na mawazo ya kuleta mabadiliko.
Alisema lazima kiongozi kuwa mwadilifu, ajijue ni mtu wa aina gani na kwamba anaongoza kwa manufaa ya nani.
Waziri mkuu alisema mabadiliko hayana mwisho hivyo ni lazima yaambatane na changamoto ambazo hazina budi kutatuliwa.
Naye mwanasiasa nguli nchini, Kingunge Ngombale Mwiru alisema katika uongozi kuna mtawala na mwonesha njia na kusisitiza kwamba mtawala sio kiongozi.
Alisema mwonesha njia ndiye kiongozi wa watu, mnyenyekevu, mtu wa watu ambaye kwake anaowaongoza ndio kipaumbele chake na kuzungumzia maendeleo ya watu yenye faida kwa kuwashirikisha.
Katika mdahalo huo, walitangazwa washindi wa insha kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Mtanzania, Redemta Benedict aliibuka mshindi wa kwanza na kupata dola za Marekani 2,000.
Washindi wengine walioingia kwenye tano bora na zawadi zao kwenye mabano ni Wakenya Joah Wanjiku (dola 1,000), Peter Mgai (dola 500), Cynthia Msembi (dola 300) na Mtanzania Seuri Owoko (Dola 200).
No tags for this post.
No comments:
Post a Comment