Sunday, 25 August 2013

HEKAYA ZA MLEVI : Mbwa na chatu; nzi na kidonda?



Punda milia









Taifa kubwa
Niacheni
Kuna kitu ambacho sijawahi kukishuhudia lakini hata wewe umeshawahi kukisikia. Kama uliwahi kukiona kwa macho ninakuomba
unithibitishie ili nisiendelee kubaki kizani. Ati ni kweli mbwa akihisi harufu ya chatu anaufyata mkia na kumfuata ili akamezwe? Mimi kama mwanafunzi mwerevu kwako, naweka sharti kwamba nataka jibu kwa aliyeshuhudia. Wengine tubaki kujifunza kutoka kwake.
Habari inapokuwa hadithi, hatuna budi kutafuta chanzo ili ibaki kuwa habari. Yasijekuwa yale ya mgonjwa wa mguu kupasuliwa kichwa na wa kichwa kukatwa mguu. Ndiyo, habari ilishakuwa hadithi na wapokeaji wa hadithi hiyo ama kwa uzembe, bahati mbaya au kutokuelewa wakafanya yaliyofanyika.
Uzembe unaweza kusababishwa na mazoea ya mgema kwenye kuti, bahati mbaya yaweza kuwa mpasuaji alitoka kupigwa talaka tatu na mwenzi wake na kutokuelewa huenda ikaletwa na huyo mtu kuajiriwa na ‘Mjomba’. Hakuwahi kuambiwa kuwa ‘Leg’ ina maana ya mguu.
Niliwahi kuona tu mfano wa chatu na mbwa kupitia kwa mzungu na Mwafrika. Siku moja niliingia Sheraton International Hotel pale kwenye viwanja vya Gymkhana. Nikashikwa fulana na mlinda usalama wa pale kwani “sikukidhi vigezo” vya kuingia mule. Nilivaa fulana, sarawili ya Jeans na viatu vya wazi.
Mzungu niliyekuwa naye (mdada) alisogea kujua tatizo. Yeye alivaa fulana, kaputura ya khaki na viatu vya wazi. Aliuliza kulikoni? Akajibiwa kwa swali “upo naye huyu?” Alipojibu “ndiyo” mimi nikaambiwa naweza kuingia. Nilitamani kubaki ili niulize tatizo lilikuwa nini ili siku nyingine nipite kwa amani.
Kwa vyovyote tatizo halikuwa rangi, kwani watu weusi waliingia na kutoka humo. Wala si viatu vya wazi kwani huyu mwenzangu angezuiwa kama mimi. Au ni suruali ya Jeans? Lakini ina tofauti gani na khaki aliyovaa mzungu? Tena basi yake ilikuwa ni kaputura, na alikuwa mtoto wa kike. Heshima gani ile?
Nikajua kuwa saa ya mkubwa daima ipo sawasawa. Nadhani ile dhana ya mbwa kuneng’eneka kwa chatu ndiyo asili yake. Ukweli hadi tulipoingia sikutaka kuligusia hilo, ingawaje huyu mdada alinichokonoa kutaka kujua. Maana ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza maishani kukikanyaga hiki ‘kisiwa cha amani’.
Nilikuja kuiona tena jirani sana na hapo. Ni pale mbele ya Ukumbi wa YMCA. Kulikuwa na vibanda vidogo vilivyouza urembo wa Kimagharibi na vingine vikiuza urembo asilia. Alikuja dada Mwafrika mrembo hasa. Mweusi kama mnubi, mwembamba na mrefu. Akasimama kibandani na kuchagua hereni na mikufu ya rangi ya dhahabu.
Hata hivyo, wakati analipa na kujiandaa kuondoka, aliingia dada mzungu na kuchagua bangili za vifuu na hereni za mbegu za matunda. Akalipa na kuondoka na mara nikamwona dada mrembo akibadilisha ile dhahabu kwa vifuu. Kwamba yeye hajui kizuri ila mzungu, ingawaje hadi leo nashangaa jinsi alivyomudu kuwa na rangi yake asilia hadi katika ujana wake.
Bado ninalo suala la mbwa na chatu. Historia ya maumbile inatukumbusha Nabii Nuhu. Alifanya kazi nzuri sana ya kuwaokoa wanadamu dhidi ya gharika kuu. Mungu wao aliwakasirikia kwa mabaya yao, akaamua kuwaangamiza. Siku moja baada ya kazi hiyo, akakamata kinywaji. Aliuchapa kikwelikweli hata akalala bila kujisetiri.
Wakati huo Nuhu alikuwa na watoto watatu; Ham, Sham na Japhet. Sasa Ham alipotaka kutoka, akamkuta mzee wake katika hali ile. Kitabu kinaandika kuwa akawafuata nduguze akicheka. Akawaambia twendeni mkaone. Nao wakashtuka (sijui kama waliona), wakachukua shuka na kurudi kinyumenyume hadi wakafikia kumfunika mzee.
Mzee alipokuwa sawa alitoa laana kubwa kwa Ham. “Daima utakuwa mtumwa wa nduguzo”! Sina uhakika kuwa mzee aliota au aliambiwa kilichofanywa na Ham. Masikini Ham ndiye baba wa watu weusi. Yeye na uzao wake wakawa wakibadilishiwa mabwana; leo mzungu, kesho Mwarabu na keshokutwa Mhindi. Mtu mweusi hajawahi kuitawala rangi nyingine, zaidi ya kuteka makabila madogo jirani kama ilivyokuwa kwa Mfalme Chaka.


Watu weupe wametuzidi akili katika jambo hili: Sisi ni watumwa wake. Kabla wao hawajapata demokrasia, sisi tulikuwa na mfumo wa kutekana na kujenga mataifa yenye nguvu. Rejea mfumo wa kabila la Nguni au Zulu. Ilisaidia kujilinda na adui asije ingia padhaifu na kutusumbua.
Leo hatutekani tena. Tunaweza kukaa na kukubaliana muungano wa uchumi. Ikumbukwe kuwa muungano wa nchi za Kirusi ulianzia wakati wa vita kuu ya Ulimwengu iliyoendeshwa na Ujerumani chini ya Hitler. Yeye pia aliziunganisha Ujerumani mbili kuwa moja yenye nguvu sana.
Bahati yao koo limenikauka. Lakini hili nitaliongea tena, no… nitalimalizia. Alamsiki kwa sasa, wacha niwahi hapo jirani.

Tembo wa Jioni

No comments:

Post a Comment