Sunday, 25 August 2013

WANANCHI WANASEMA NINI??



 
Tembo


WAZIRI WA MABO YA NDANI
ASKARI... POLICE
"Alhamisi wiki hii Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alinishangaza baada ya kuwaeleza Watanzania kuwa alichukua jukumu la kuwavua madaraka maofisa wanne wa polisi, kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo."

Majukumu waliyoshindwa kuyasimamia  maofisa hao yalisababisha askari  10 wa vyeo vya chini kushindwa kuwajibika ipasavyo na kufanya mambo kinyume na majukumu yao, hivyo kusababisha saba kati yao kufukuzwa kazi, mmoja kusimamishwa na wawili kupewa onyo kali.
Ilinishangaza kwa kuwa Dk Nchimbi alisahau kuwa mara kadhaa wananchi na wanaharakati wamekuwa wakiwataka baadhi ya mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete akiwamo Dk Nchimbi mwenyewe, wajiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao,  tena kwa uzembe au makosa ambayo hawajayafanya wao bali yamefanywa na watu walio chini yao.
Tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi  katikati ya mikono ya polisi pamoja na matukio ya wananchi kuuawa kwa kupigwa risasi  mkoani Morogoro, Arusha, Tabora nani alivuliwa madaraka, wakati maofisa wa jeshi hilo walikuwapo maeneo ya tukio na inawezekana walishuhudia kinachoendelea?
Wiki mbili zilizopita askari ‘feki’ wa usalama barabarani mwenye cheo cha sajini alikamatwa akiwa katika majukumu kama yanayofanywa na askari halisi wa kikosi hicho, lakini hadi sasa hatujasikia kuchukuliwa hatua za kinidhamu dhidi ya ofisa yeyote wa kikosi hicho.
Inawezekana kabisa wanaohusika katika matukio ya  uhalifu na utapeli yanayoidhalilisha  polisi na nchi kwa ujumla ni maofisa wa ngazi za juu ambao wanawatumia askari wa vyeo vya chini, hivyo nao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki, siyo kuvuliwa madaraka tu.
Huenda jeshi limepwaya kiutendaji, limeelemewa na matukio mabaya, baadhi ya askari wake wamechafuka, hivyo wanaleta picha mbaya kwa jeshi zima?
Baada ya kauli ile ya Dk Nchimbi, nilijiuliza maswali mengi kichwani, hivi polisi wakikosea wanachunguzwa na nani, au iundwe tume huru kuwachunguza maana inaonekana wazi kuwa sasa limeshindwa kujichunguza lenyewe  kama ambavyo imekuwa ikitokea hata kwa mambo ambayo wanatuhumiwa wao.
Nasema hivi baada ya kutafakari utitiri wa matukio ya uhalifu nchini ukiwamo ujambazi, utekaji, uteswaji na kushambuliwa kwa watu na hata mauaji.
Jeshi limeshindwa kukabiliana  na vitendo hivyo, ndiyo maana wananchi wamefikia hatua ya kulaumu na kulalamika kuwa kasi ya polisi imeshuka kiasi cha kushindwa kuwabaini wahalifu.
Hivi sasa matukio yanayovihusu vyama vya upinzani ndiyo yanayopewa kipaumbele, ikiwa ni pamoja na upelelezi kukamilika kwa wakati na watuhumiwa kukamatwa usiku wa manane, kusafirishwa kwa helikopta kupelekwa mahakamni tena kwa mbwembwe za hali ya juu.
Mpaka leo zimebaki stori tu kwa baadhi ya matukio likiwamo lile la Dk Stephen Ulimboka, polisi wanataka ushahidi gani kuthibitisha makosa yaliyofanywa na askari wake, matukio ambayo picha zake zipo tena hadharani tu katika vyombo vya habari.


Sitaki kuzungumzia kesi zilizopo mahakamni, lakini zipo ambazo ushahidi wake ulifanyika kwa siku chache tu, lakini yale matukio yaliyowasababishia watu ulemavu, mauti mpaka leo yamesokomezwa chini ya kapeti.
Wiki hii polisi saba ‘feki’  walikamatwa wakiwa na sare za jeshi hilo, tena wakiwa doria huku mmoja akiwa na cheo cha meja na walikuwa na redio ya mawasiliano pamoja na  bastola, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kuna kitu kinaendelea ndani ya jeshi hilo.
Huenda watu wa namna hii wakawa na mtandao wao ndani ya jeshi hilo, mtandao ambao unawalinda, unawapatia sare za polisi, bastola na hata kuweka vigingi ili wasikamatwe na polisi wanaofuata maadili ya kazi yao.
Ndiyo maana nikasema kuwa kuwafukuza kazi askari wa vyeo vya chini siyo suluhisho, aliyeshiriki wizi na ambaye ameshindwa kusimamia majukumu yake mpaka wizi ukatokea wote wanatakiwa kufukuzwa kazi ili iwe fundisho kwa wengine, nani anayejua pengine nao walihusika kwa namna moja au nyingine.
Kwa mtindo huu siyo ajabu tukasikia yule Msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo, Renatus Chalamila, ambaye alipewa likizo baada ya kutajwa mara nyingi kuhusika kuwatoza fedha vijana walioomba ajira za uaskari, akavuliwa madaraka yake kama ilivyotokewa kwa wale maofisa wanne.
Wapo waliochukuliwa hatua kwa  kufukuzwa kazi, lakini wapo wengi waliobaki, kwa mtindo huo wa kuwaacha vigogo wanaoendelea kuwa na mtandao wa askari wa vyeo vya chini sidhani kama haki ya raia itapatikana......

swara kitanzini

No comments:

Post a Comment