JESHI LA POLISI LAKUMBWA NA MITIHANI....
|
Kilimanjaro |
|
Kamanda wa Police Tz |
SIKU
chache baada ya kukamatwa kwa
askari feki wa usalama barabarani, Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata watuhumiwa saba wa
ujambazi, wakiwa na sare za Polisi, huku mwingine akijifanya ofisa
Usalama wa Taifa.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaa, Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao
walikamatwa wakiwa na sare za Polisi jozi mbili.
Watuhumiwa
hao ni Khamis Mkalikwa (40), Magila Werema (31), Nurdin Bakari (46),
Materu Marko (32), Louis Magoda (34), Amos Enock (23) na Amiri Mohammed
(45), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Sare
hizo, kwa mujibu wa Kamanda Kova, ni zenye cheo cha Sajenti wa Kituo,
huku jozi moja ikiwa na jina linalosomeka SSGT A.M Mduvike.
Watuhumiwa hao walikamatwa jana katika eneo la Kiluvya, baada ya askari kuweka mtego, ambao ulifanikiwa kuwanasa.
Alisema
watu hao walikuwa wakitumia silaha, sare za jeshi la Polisi na redio ya
mawasiliano katika uhalifu wao na hivyo kuwafanya baadhi ya watu
kutupia lawama Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na uhalifu.
Alisema
watuhumiwa hao, wanahusishwa na uhalifu katika maeneo ya Boko, Tegeta,
Mbweni, Bahari Beach, na maeneo mengine ya jiji. Alisema watu hao ni
hatari zaidi.
Watuhumiwa
hao walikuwa wakitumia gari aina ya Cresta GX, 100 yenye namba T 546
BWR na baada ya kuona wamezingirwa na askari maeneo hayo, walifyatua
risasi moja hewani, lakini askari walipambana nao na kufanikiwa
kuwakamata.
“Mbali
na vitu hivyo pia wamekamatwa na bastola moja aina ya Brown yenye namba
B.3901, ambayo ilikuwa na risasi nne na ganda moja, tunawashikilia kwa
upelelezi na baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Kova.
Katika
hatua nyingine, Kamanda Kova alisema wanamshikilia mtuhumiwa Alquine
Masubo (42) maarufu kama Claud, kwa kosa la kujifanya ofisa wa Usalama
wa Taifa.
Claud
ambaye ni mkazi wa Yombo Buza, alikamatwa akiwa na vielelezo mbalimbali
pamoja na nyaraka za idara hiyo, ambapo baada ya kuhojiwa alikiri kuwa
yeye si mfanyakazi wa idara hiyo.
Kova
alisema mtuhumiwa huyo alipopekuliwa zaidi, alikutwa na bastola aina ya
Browing yenye namba A. 956188-CZ83 ikiwa na risasi 12 ndani ya kasha
lake.
“Alipopekuliwa
nyumbani kwake alikutwa na bastola nyingine aina ya Maknov yenye namba
BA4799 ikiwa na risasi 19 na kitabu cha mmiliki chenye namba CAR
00071678, ikiwa na jina la P.1827 LT COL Mohammed Ambari, jambo ambalo
haliwezekani kwa mtu mmoja kumiliki silaha mbili,” alisema Kova.
Mtuhumiwa
huyo pia alikutwa na kitambulisho cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
chenye namba 7001- E. 1075 na kompyuta mpakato aina ya Toshiba.
“Huyu
ni tapeli wa siku nyingi na taarifa zake tulikuwa nazo, anatumia kivuli
cha idara ya usalama wa taifa kufanya utapeli, lakini sasa ndiyo mwisho
wake na wananchi wamjue” alisema.
No comments:
Post a Comment