TAHADHARI: FEDHA NI HATARI KWA AFYA YAKO


Fedha ni hatari kwa afya ya binadamu kwani huweza kusababisha madhara makubwa.
Katika uchunguzi, ilibainika kuwa fedha za noti na zile za sarafu
huweza kukusanya na kusambaza vimelea vya magonjwa hatari kutoka kwa mtu
mmoja kwenda kwa mwingine.
Mtaalam wa magonjwa mbalimbali, Dk. Richard Marise, ametanabahisha
kwamba tafiti mbalimbali duniani zimeripoti kuhusu vimelea vinavyoweza
kusafirishwa kupitia fedha ambavyo ni Staphylococcus Aureus,
Escherichiacoli,Fecal Bacteria na sumu nyingine.
“Tafiti nyingi
zilizofanywa katika nchi zilizoendelea, zimegundua kuwa vimelea
hatarishi kwenye fedha hasa za noti ambapo vingi hutokana na uchafu
utokao kwa mwanadamu mwenyewe kwa mfano; kinyesi, mkojo na jasho.
“Vimelea hivyo kwa pamoja husababisha magonjwa kama boils (magonjwa ya
ngozi) pneumonia, toxic shock syndrome (homa za sumu mwilini), diarrhea
(kuharisha), gum diseases (magonjwa ya fizi), homa za vipindi na
meningitis (uvumbi wa bongo) ambao kama hakuna matibabu huweza
kusababisha kifo,”
alisema Dk. Richard.
Akifafanua jinsi fedha
zinavyoweza kusafirisha magonjwa, daktari huyo alisema fedha huweza
kushikwa na mtu asiyeosha mikono yake kwa maji safi na sabuni baada ya
kutoka kujisaidia, kisha hela hiyo huweza kutua mikononi mwa mtu
mwingine ambaye huacha jasho lake na kuongeza vimelea vya magonjwa
mengine juu yake.
Mzunguko huo unaweza ukawa mkubwa kufikia hatua ya
vimelea kusambaa kwa mamilioni ya watu hivyo kuifanya jamii kuwa katika
hatari zaidi ya maambukizi ya ugonjwa husika.
Dk. Richard
alikazia kuwa
“maambukizi hutokea kama mtu aliyeshika hela hizo atagusa
sehemu zenye unyevunyevu kwenye mwili wake kwa mfano jicho, mdomo na pua
ambapo vimelea hivyo vitapata nafasi ya kuingia ndani ya mwili.”
Katika mazingira ya kawaida, fedha zenyewe huhifadhiwa katika mazingira
hatarishi ambapo kuna mifano ya watu kuhifadhi fedha ndani ya nguo za
ndani au kwenye matiti (akina mama zaidi). Fedha pia huweza kudondoka
kwenye uchafu wa aina mbalimbali na kuokotwa kisha ikatumika tena.
Ukiachilia mbali kubeba vimelea vya magonjwa, fedha zinaweza kubeba sumu
na madawa ya kulevya juu yake ikiwa itapitia kwenye mikono ya mtu
aliyeshika vitu hivyo.
“Ni vyema ukatumia fedha kwa uangalifu,
usiweke hela mdomoni na ukumbuke kuosha mikono yako kila mara kwa maji
na sabuni ili kujikinga na maambukizi,”
alitahadharisha Dk. Richard.
No comments:
Post a Comment