Thursday, 15 August 2013

Maandalizi mbio za Uhuru yaanza




Maandalizi mbio za

 Uhuru yaanza









.
Wanariadha zaidi ya 300 kutoka nje ya nchi wametuma maombi ya kushiriki kwenye mbio za Uhuru Marathon zilizopangwa kufanyika Desemba 8, Dar es Salaam.
Jana Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fennela Mkangara ametaja wajumbe 11 aliowateua kwenye kamati ya maandalizi ya mbio hizo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals Communication LTD, Innocent Meleck alisema jana kuwa mbio hizo zitakuwa na vipengele vinne.
Kwa mujibu wa Meleck, kutakuwa na mbio ndefu za marathon (Km 42), nusu marathon (km 21), mbio za kujifurahisha (Fun run km 5) na mbio maalum za km 3 kwa ajili ya viongozi.
“Hivi sasa tuko kwenye mchakato wa kutafuta wadhamini, yule atakayejitokeza kudhamini mbio za marathon ndiye atabeba jina la mashindano hayo,” alisema Meleck.
Fenella amewataja Said Meck Sadiki, Sophia Mjema, Allan Kijazi, Julliana Yasoda, Zamaradi Kawawa, Hamad Ndee, Josiah Mfungo, George Kavishe, Gabriel Nderumaki, Habbi Gunze na Meleck kuunda kamati ya mashindano hayo.
“Mbio za Uhuru zina lengo la kuimarisha umoja, upendo, mshikamano na amani ya taifa letu hivyo mbali ya wageni walioomba kushiriki Watanzania wengi wamejiandikisha kushiriki,” alisema Waziri Fenella.
Mbio hizo zilizopangwa kufanyika kwenye viwanja vya Leaders Club zitafuatiwa na tamasha la Uhuru usiku wa siku hiyo kuamkia Desemba 9 ambapo Tanzania itakuwa ikiadhimisha miaka 52 ya Uhuru.
Wakati huohuo, Mashindano ya wazi ya taifa ya Kuogelea yamepangwa kufanyika Septemba 28 na 29 kwenye bwawa la kuogelea la shule ya Braeburn la jijini Arusha.
Katibu mkuu msaidizi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka aliliambia gazeti hili jana kuwa mashindano hayo yatashirikisha timu mbalimbali za mikoa, shule, waogeleaji kutoka sehemu mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Kwa mujibu wa Namkoveka, waogeleaji hao watachuana katika mtindo unaotambuliwa na (Fina).

No comments:

Post a Comment