Friday, 16 August 2013

Pombe si chai,




Pombe si chai, waliwahi kusema Waswahili 
wakiwa na maana



 kubwa, ina madhara kwa watumiaji wake. 





Wengi wetu katika jamii hutumia kilevi au pombe za aina mbalimbali na mara nyingi baada ya hapo huhisi uchovu mwingi, adha lukuki ambazo wakati mwingine huambatana na kiu na kukosa hamu ya kula.
POMBE SI CHAI
Hali hiyo huwatokea wengi hasa kesho yake au wakati mwingine muda mfupi baada ya kurudi nyumbani na baadhi yao
wamekuwa wakiita hali hiyo, ‘mning’inio.
Kwa ufupi, hiyo ni hali yenye madhara kimwili kutokana na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Tatizo hili huathiri wanywaji wengi huku baadhi yao wakipata kero kubwa siku inayofuata, wengine wakitamani kutokugusa tena kinywaji, ingawa baada ya hali hiyo kuisha hujikuta wakirudia kunywa na kusahau madhara yaliyowapata.
Kwa Kiingereza, hali au tatizo hili huitwa ‘hangover’, ambapo unaelezwa kuwa  kati ya asilimia 25-30 ya wanywaji wote, miili yao inao ukinzani na tatizo hili, hivyo huwa hawalipati.
Bara la Ulaya, ndilo linatajwa kuongoza kwa unywaji mwingi wa pombe ambako inakadiriwa kuwa mtu mzima hunywa wastani wa lita 12.5 kwa mwaka, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takwimu za 2012.
Nchini Tanzania, taarifa au takwimu za mauzo na matumizi ya pombe, zinataja Kilimanjaro, Arusha na Dar es salaam kuwa maeneo vinara wa unywaji wa pombe.  Kote duniani, vifo vya watu milioni 2.5 vinakadiriwa kutokea kila mwaka kutokana na unywaji wa pombe.
Magonjwa kadhaa yanayoonekana kusababishwa na unywaji pombe ni pamoja na  moyo, mishipa ya moyo, kisukari, ugonjwa wa ini, kuharibika kwa kongosho, ukosefu wa vitamini mwilini, magonjwa ya akili, kushindwa kuwa na kumbukumbu.
Tatizo hili limekuwa na mambo mengi ambayo ni potofu katika jamii, wengine wakishauriana wanapokuwa na tatizo hili  wanywe pombe kesho yake ili kuweza kutatua tatizo la mning’inio.
Wanywaji wazoefu huita hali hiyo, ‘kuzimua’, wengine hushauriana kula mlo mwingi kabla ya kulala, kula vyakula vyenye uchachu kama vile, ndimu au limao au kunywa na kujimwagia maji mengi mwilini.
Dalili za mning’inio

Kwa ‘wapiga maji” wazoefu, dalili hizi wanazifahamu vizuri pengine wasihitaji hata kusoma hapa, ila hawafahamu kwa nini zinatokea.
Kwa jumla, mning’inio hutofautiana kati ya pombe na pombe na mtu na mwingine. Pia, dalili huchukua saa kadhaa baada ya kunywa na huweza kuwepo kwa siku moja au zaidi.
Pombe za ina zote husababisha mning’nio, mfano wa aina za pombe ni bia, pombe kali kama spirits, whisky na mvinyo, ambazo zote huleta madhara ingawa pombe kali huwa na madhara zaidi.
Sababu kubwa ni kuwa pombe kali zina kiwango kikubwa cha kilevi kuliko pombe zingine, pia zile pombe zenye rangi kama vile brandy, whisky na mvinyo husababisha mning’inio zaidi kuliko zisizo na rangi.
Pombe hizo zina kirutubisho  cha congeners ambalo ni zao litokanalo na pombe kuvundikwa kwa muda mrefu na kuchacha pia kemikali zinazotumika kihifadhia pombe zisiharibike pia uwepo wa virutubisho kama zinki na vitu vingine kwa ajili ya kuipa ladha pombe navyo huchangia mning’inio.
Dalili za mnining’inio
Ni upungufu wa maji mwilini, kutokuwa na nguvu, kichwa kuuma, mwili kuwa mchovu, kichefuchefu, kutapika, kuharisha, joto la mwili kupanda, kukosa hamu ya kula, kutokuwa mtulivu, kutokupatana na mwanga na sauti, kutokuwa na usingizi mzuri, uwezo wa kufikiri au kiuamuzi hupungua, pia kuaw na shida ya harufu, kuonja ladha au mawazo ya pombe.
Umeng’enyaji pombe mwilini
Pombe kufika katika tumbo la chakula  ambako ndani ya dakika chache huwa imeishanyonywa kwa asilimia 20 na kuingia moja kwa moja katika mzunguko wa damu na kufika katika ubongo hapo ndipo hali ya kujihisi kulewa huanza.
Hakuna chakula chochote chenye tabia hii zaidi ya pombe na sehemu iliyobakia huendelea kwenda katika utumbo mdogo na hunyonywa pamoja na vyakula vingine huku kiasi kingine hutolewa kwa njia ya jasho, mate, mkojo na hewa unayopumua.
Tofauti na vyakula kama mafuta, wanga na protini ambavyo humeng’enywa na kisha nishati/sukari huweza kuhifadhiwa, kwa pombe ni tofauti kwani huwa na nishati tupu (empty energy) isiyoweza kuhifadhiwa ni hii ndiyo sababu mwili huacha kumeng’enya vyakula vingine na kuanza kumeng’enya pombe.
Kwa kuwa nishati ipatikanayo haina pa kuhifadhiwa mwilini, hivyo  pombe huingia haraka katika damu na kufika katika ubongo na hali ya kulewa huanza kutokea.

Pombe huugharimu mwili kwani umeng’enyaji wake hutumia maelfu ya nishati/sukari mwilini na maji mengi, pia maji hupotea mwilini kwani pombe huchochea figo kuruhusu maji mengi kutoka kwa njia ya mkojo hivyo mtu hupoteza maji kwa kukojoa sana.
Athari za kupungua maji mwilini  ni maji kupungua katika mzunguko wa damu, mishipa ya damu kusinyaa, kichwa kuuma, midomo kuwa mikavu na uchovu mkali, kupungua kwa sukari husababisha ubongo kukosa sukari ya kutosha, hivyo kichwa kuuma na mwili kuwa mchovu. Uwepo wa pombe tumboni huathiri kuta tumbo, hivyo kuta hizo hupata uchokozi na kusababisha kichefuchefu, kutapika na kuharisha.
Ini kuwa na kazi ya ziada kuondoa sumu zilizopo katika pombe ambayo tayari ipo katika mzunguko wa damu kwa mtindo uitwao oxidation, hii  husaidia pombe kutokudhuru seli za mwili, ini huweza kuathirika na tishu za ini kuweza kuharibika. Kwa jumla, pombe ni moja ya visababishi vikuu vya ugonjwa wa ini (liver cirrhosis), hapa ndipo pombe husagwa na kuvunjwa vunjwa,  kisha zao liitwalo acetalydehde hupatikana.
Zao hili ni sumu kwa mwili kwani inavuruga majimaji ya vinasaba (mutagen) na ni kisababishi hatari cha saratani (carcinogen). Madhara yake ni makubwa kuliko hata pombe yenyewe na mwili huchukua muda mwingi zaidi kukivunja kwenda katika zao lingine lisilo na madhara.
Namana ya kuepukana mningi’inio
Njia kuu ya kuepukana tatizo hili na madhara mengine ya pombe ni kuacha kunywa pombe, kwa wale watakaoshindwa basi ni vyema wakanywa kwa kiasi, unywaji wa maji mengi na vyakula vyenye majimaji mengi husaidia kupunguza makali na dalili za mning’inio.
Tiba ya vyakula asili
Kula vyakula vyepesi- mayai yana kirutubisho cysteine, kinachokata makali ya mning’inio, maziwa ni chakula zaidi kuliko maji na husaidia kukuongezea maji huku yakikupa madini ya kalsiamu ambayo itarahisisha kuondokana na kuchoka.
Kunywa maji- Utaendelea kutokuwa mtulivu mpaka pale tu mwili utakaporudisha kiwango cha maji mwilini, maji ni nyenzo kuu ya kuondoa tatizo hili, ukiweza kunywa juisi kama za machungwa, juisi ni nzuri zaidi na kama tu tumbo lako litastahimili.
Magadi- Weka kijiko kimoja cha chai cha magadi (baking soda) katika kikombe au glasi moja ya maji, halafu kunywa hii pia husaidia kukata makali ya mning’inio.
Mazoezi mepesi- Hii inasaidia kunyanyua kazi za kimwili zilizoathirika, hivyo husaidia kuondoka kwa mabaki ya sumu iliyotakana na umeng’enyaji wa pombe. Mazaoezi ya tasaidia pia upelekaji wa oksjeni katika sehemu mbalimbali za mwili, hivyo seli kuendelea kuondoa makali ya sumu mwilini.

Oksijeni- Kama utapatiwa oksijeni katika huduma za afya ni moja ya njia ya kuondoa mning’inio na kuharakisha kukoma kwa dalili na kuondoa sumu kwa haraka.
Vitamini B (thiamine)-Hii husaidia kurudisha kirutubisho kiitwacho glutarate katika ubongo ambacho nacho kinachangia kichwa kuumwa, vitamini  hii hupungua baada ya kunywa pombe, kwa kunywa kirutubisho cha vitamini B huwa na faida kubwa kwa afya.

No comments:

Post a Comment