Ukimpa shoga upenyo
Mwanamke, Ukimpa shoga upenyo kwa
mwenzi wako, itakula kwako...!
Unapokuta mwanamke au mwanaume anamlaumu mume au mke wake kwa kitendo
chake cha kukaa na kuzungumza na mtu wa jinsia nyingine mara kwa mara
utasemaje, je utasema ni wivu uliopitiliza?
Inawezekana ikawa ni wivu, lakini kwa upande wa pili, huenda haitokani
na wivu, bali ukweli kwamba, watu wawili wa jinsia mbili wanapozoeana
katika kuzungumza, hatimaye uwezekano wa kukutana kimwili hujitokeza.
Kwa kupitiwa au kujisahau, wanawake wengi huwa wanawapa nafasi marafiki
au shoga zao kuwa karibu na waume zao kwa kuzungumza, wakiamini kwamba,
kuzungumza tu, hakuwezi kuwa na madhara. Huku ni kujidanganya kwa
kiasi kikubwa.
Kwa kadiri watu wa jinsia mbili wanavyozoeana katika kuzungumza na
hasa wanapoanza kuzungumzia mambo yao ya ndani, ndivyo ambavyo mipaka
huvukwa na kujikuta wakihusiana kimwili.
Pale mpenzi kuwa karibu mara nyingi na mtu mwingine wa jinsia tofauti
kwa maelezo kwamba, ‘ni rafiki tu,’ ujue tatizo liko karibu kuanza kama
halijaanza. Kuwa karibu sana kwa mazungumzo mara kwa mara na mtu wa
jinsia nyingine, ni aina ya uzinzi pia, kutegemea tu aina ya mazungumzo.
Labda nijaribu tu kuwasaidia wale ambao wako kwenye uhusiano tayari.
Wanapohisi dalili fulani, kuhusiana na rafiki zao wa jinsia tofauti,
wanapaswa kujua kwamba, hivi karibuni, urafiki huo utaisha na watakuwa
wapenzi. Kama hawataki kuharibu uhusiano waliomo, wanapohisi dalili
hizi wanapaswa kujitoa.
Kama mtu ana rafiki wa jinsia tofauti, ambaye siku zote amekuwa
akijiambia ni marafiki tu, anapojikuta ameanza kumwotea ndoto za mchana
kama za Alinacha, ni hatari. Kumwotea ndoto za mchana rafiki wa jinsia
tofauti si dalili nzuri hata kidogo na haiashirii jambo jema huko
mbeleni.
Kama mwanaume ana rafiki wa jinsia tofauti na anapokuwa na jambo au
mambo ya kutaka mtu mwingine ayasikie ili ahisi nafuu, anayaweka kwa
ajili ya rafiki huyo, badala ya kumwambia mkewe, urafiki huo utageuka
balaa sasa hivi.
Kuna wanaume ambao hata kama ametaka kugongwa na gari, hatazungumza
jambo hilo na mkewe, bali atangoja akikutana na huyo rafiki yake wa
jinsia tofauti ndiyo amweleze. Hata kama mwanaume huyu hajashiriki tendo
la kujamiiana na rafiki huyo, uwezekano ni kwamba, bado kitambo kidogo
watashiriki.
Mwanaume anapoona na kuamini kwamba, rafiki yake wa jinsia nyingine
anamwelewa vizuri zaidi kuliko mkewe, ni wazi kabisa kwamba, hiyo ni
hatari, kwani ni safari ya moja kwa moja kuelekea kushirikiana kimwili.
Kama imefikia mahali ambapo mume anashiriki kujadili siri za mke wake na
rafiki wa jinsia nyingine ni dalili mbaya kwamba, watu hao kama
hawajaanza kushirikiana kimwili, wataanza muda mfupi ujao.
Mwanaume kuanza kumnunulia rafiki wa jinsia nyingine nguo za ndani,
pafyumu, mapambo na vitu vya aina hiyo. Jambo hilo ni ishara kwamba,
ile, ‘ni rafiki yangu tu,’ itafutika sasa hivi na watu hao watakuwa
wapenzi.
Mwanaume........Kama uko kwenye urafiki ambao una dalili hizo, ni vema
kuanza kukagua mwenendo wako na huyo rafiki yako. Kama hutaki kutoka
nje ya ndoa yako, inabidi au ujitoe kwenye urafiki huo, au uache
kufanya hayo mambo niliyoyaeleza.
Namalizia kwa kuwaambia wanawake kwamba, huna haja ya kumwacha huru
shoga yako na mumeo kwa kudhani ni vigumu kwa watu hao kukusaliti.
Wakianza kushiriki mazungumzo ya kihisia haraka sana wataingia mahali
ambapo watataka kushirikiana kimwili.
Hata wao katika hatua za awali watakuwa hawana lengo la kushiriki tendo
la kujamiiana, lakini mazungumzo yao, hatimaye yatawafanya waungane
kihisia na kitakachofuata kitakuwa ni maumivu kwako.
Weka mipaka ya makusudi, onesha kutoridhishwa na mume au mpenzi wako ama
shoga yako unapoona mmoja au wote wanajisahau na kuanza kuwa karibu
sana kimazungumzo.
Suala la ‘shogako leo alipita ofisini kwangu,’ kutoka kwa mume au mpenzi
wako, usilikubali kirahisi. Suala la ‘nasikia shemeji anasafiri,
naomba anipe lifti, na mie naenda Morogoro,’ usikubali kirahisi. Bora
uambiwe una wivu kuliko kuja kupoteza……
No comments:
Post a Comment