WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WATUHUMIWA KWA UFISADI
WAKURUGENZI WA HALMASHAURI
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini mtandao wa
ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri mbalimbali hapa
nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha,
Mwanza, Mbeya na Ilala. Aidha Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed
Mbarouk alisema keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili
wananchi waweze kuwafahamu.
Mbarouk
alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi
ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya
wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na
kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali, lakini bado
wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana
na hali hiyo, kamati hiyo imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala
hilo.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na
wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa
ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri
zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson
Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua
na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye alisimamishwa
kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea kupata
mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
No comments:
Post a Comment