WAZEE wetu walikuwa na sababu
Eiyer, WAZEE wetu walikuwa na sababu ya kuzuia wachumba kukutana kimwili kabla ya ndoa…!
 |
mahusiani |


Nimesoma mada ya rafiki yangu Eiyer
kuhusiana na suala la wanandoa kukutana kimwili kabla ya kufunga ndoa
ili kufahamiana zaidi. Lengo kama alivyoeleza rafiki yangu huyu ni
kuepuka mitafaruku inayoweza kutokea baada ya kuingia katika ndoa na
kukutana na hali ambayo haikutarajiwa. Ukitaka kujikumbusha kuhusu mada
hiyo bofya hapa:
Yes,i'm goin to marry you,but before that i just wanna make sure of something...
Eiyer
ametoa mifano kadhaa ambayo siwezi kuipinga, lakini lengo langu hapa ni
kuweka angalizo kuhusiana na suala zima la kukutana kimwili kwa wapenzi
kabla ya ndoa ili wanaofanya hivyo waweze kujua athari za kufanya jambo
hilo ni zipi?
Ni kweli kwamba, siku hizi vijana wengi huamini kuwa, baada ya kukutana
kimwili, ndipo wanapoweza kudai kwamba, wamewafahamu wapenzi wao vizuri
na kwamba kukutana kimwili ndiyo mapenzi au kupendana kwenyewe.
Wanapokutana kimwili na kuvutiwa na tendo la kujamiiana, huamini kabisa
kwamba, uhusiano nao utakuwa mzuri. Kwao, tendo la kujamiiana ndiyo
kipimo cha uimara wa uhusiano wao.
Baada ya kufanya mapenzi, wapenzi huamini kwamba, sasa wanaweza
kujitolea kwenye uhusiano huo na kwamba, wanaweza kuwa na nguvu nao.
Suala hili, wataalamu huliita mtego wa kimapenzi. Huitwa hivyo kwa
sbabu huwafanya wapenzi kutoangalia sifa nyingine na badala yake
kuweka nguvu kwenye mwili, yaani tendo la kujamiiana.
Upofu hutokea kutokana na kuzalishwa kwa kemikali nyingi mwilini, zenye
kumfanya mtu asiweze kujiuliza kuhusu maeneo mengine ya kimaisha ya
binadamu, zaidi ya mwili. Kinachotokea ni miili kuvutwa na wale tunaodai
tunawapenda kwa kuzalisha homoni inayofahamika kama phenylethylamine au PEA kwa kifupi.
Kemikali au homoni hii pamoja na nyingine kama vile dopamine na norepinephrine (ambazo huchochea hali ya kimwili) na testosterone
(ambayo huongeza hamu ya kujamiiana), huzalishwa baada tu ya kukutana
kimwili. Baada ya kuzalishwa kwa homoni hizi, akili ya mtu huona mwili
tu, yaani mapenzi na siyo sifa nyingine.
Hapa ndipo ambapo, mtu anajikuta hawezi kujizuia kukutana tena kimwili
na mpenzi wake, mara baada ya kukutana naye mara moja. Baada ya kufanya
mapenzi na kufika kileleni, huzalishwa homoni iitwayo oxytocin
(ambayo huhusika na mihemko), homoni hii humfanya mtu kujikuta anapenda
kuwa karibu na kujifunganisha na mtu aliyefanya naye mapenzi. Naweza
kusema ukaribu kwa wapenzi wawili huongezeka na unakuwa ni ukaribu wa
mwili zaidi.
Kuzalishwa kwa homoni hizi, ni jambo ambalo mtu hawezi kulizuia na huwa
linakuja kwa nguvu sana, kiasi kwamba, mtu huwa kama amepoteza ufahamu
wa maeneo mengine ya kimaisha isipokuwa mapenzi tu. Wale waliowahi
kuwa na uhusiano wa kimapenzi kabla ya ndoa au wale wanaotoka nje ya
ndoa zao kwa kuvutwa kimwili na wapenzi wengine wanajua inavyokuwa.
Lakini homoni hizi, hatimaye huanza kupungua na mtu huanza kuhisi
kwamba, alikosea. Haoni tena au kuhisi kama ilivyokuwa awali. Sasa haoni
kuwa mpenzi wake ni mzuri au anayefaa kama alivyokuwa anaona awali.
Kwa sababu, homoni zile zimeshuka sana, mwili unakuwa hauna maana tena.
Kwa bahati mbaya kile kilichokuwa kinaitwa upendo kilikuwa kimefungiwa
kwenye mwili na homoni hizo ambazo sasa hazipo. Hivyo, wapenzi hawana
tena cha kushika ambacho, wataweza kukiita mapenzi.
Naamini sasa unajua ni kwa nini tangu kale kabisa suala la wachumba
kukutana kimwili kabla ya ndoa lilikuwa linapingwa sana na wazee wetu.
Ni kwamba, watu wanapokutana kimwili , uwezo wa kukaguana tabia unakuwa
umefungwa kutokana na kufumuka kwa homini hizi ambazo, hubadili hali ya
mtu na hisia zake kwa ujumla.
Hebu jiulize, ni kwa nini mapenzi yanayoanza kwa moto sana,huzimika
haraka au kwa kishindo sana? Ni kwa sababu yamejengwa juu ya msingi
usioaminika, yaani kutokana na mihemko ya kimapenzi! Penzi linalokuwa
polepole na lisilotanguliza kukutana kimwili ndilo lenye kushika, kwani
halina msingi wa mwili…..
No comments:
Post a Comment