Nanenane ni ya wakulima,
siyo Serikali
![]() |
chui wa Tanzania |
![]() |
Tembo wa Tanzania |
Waasisi wa programu ya kuifanya siku hiyo iwe
rasmi kwa wakulima walitaka wakulima watumie siku hiyo kama fursa ya
kuonyesha mazao yao, kubadilishana mawazo miongoni mwao kuhusu kilimo na
kutafuta namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwa lengo la
kuongeza tija na uzalishaji.
Pia maadhimisho hayo yalilenga kuwasaidia wakulima
kufanya mashauriano kuhusu namna ya kupata masoko ya kuwapatia bei
nzuri kwa mazao yao.
Masuala ya pembejeo za kilimo na mbinu za
kufanikisha kilimo cha kisasa yalipewa kipaumbele siku hiyo, kwani
wakati huo wataalamu wa kilimo na ‘mabwanashamba’ walikuwa sambamba na
wakulima na viongozi wa vyama vya ushirika ili kuwapa ushauri katika
maeneo husika.
Wakati huo wakulima walikuwa wakijiona kama wadau
muhimu katika sekta ya kilimo na vyama vya ushirika vilikuwa
vikiwajibika kwao kikamilifu, tofauti kabisa na hali ilivyo hivi sasa.
Inasikitisha kuona kwamba hivi sasa sio tu
maadhimisho hayo hayawahusishi tena wakulima katika kiwango tulichokijua
wakati ule, bali pia yametekwa na taasisi za Serikali, wanasiasa na
wakala wa maendeleo wasiohusika na kilimo hata kidogo.
Kila wizara, mashirika ya umma na idara za
Serikali zimejenga mabanda ya maonyesho kwa gharama kubwa ili kutumia
siku hiyo kutangaza bidhaa na shughuli zake, nyingi zikiwa hazina
uhusiano wowote na masuala ya kilimo, hivyo kuifanya Siku ya Wakulima
kupoteza maana ya kuanzishwa kwake.
Shamrashamra za wakulima tulizokuwa tukizishuhudia
siku hiyo zimepotea kutokana na viongozi wa Serikali na wanasiasa
kuteka siku hiyo kwa sababu za kimasilahi.
Mkanganyiko kuhusu siku ya kilele cha maonyesho ya
Siku ya Wakulima umetokana na kuwapo mkono wa Serikali katika maonyesho
hayo ya wakulima.
Badala ya kukiachia Chama cha Wakulima Tanzania
(Taso), kitekeleze jukumu lake la kuratibu maonyesho hayo, ikiwa ni
pamoja na kuamua siku ya kilele cha maonyesho hayo kutokana na uwezekano
wa kuingiliana na Sikukuu ya Iddi el Fitri, Serikali imepenyeza mkono
wake na kuamua kwamba jana ndio iwe siku ya kilele cha maonyesho hayo.
Matokeo yake ni mkanganyiko, kwani kanda nyingine, ikiwamo Mbeya
zimeamua kilele hicho kiwe leo.
Katika siku za hivi karibuni zimejitokeza sauti
kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini zikitaka ifanyike tathmini juu ya
ubora wa maonyesho hayo katika miaka 10 iliyopita ili kuona kama
yamekuwa yakifanyika kulingana na malengo ya kuanzishwa kwake.
Moja ya sauti hizo ni ile ya Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Erasto Mbwilo ambaye wakati akifungua maonyesho hayo Kanda ya
Arusha, alisema tathmini hiyo itaonyesha kama yana faida au hasara na
kuongeza kwamba huenda yakatumia gharama kubwa pasipo kuwasaidia
wananchi.
Tunaungana na mkuu huyo wa Mkoa na wengine wengi ambao wameuliza
maswali kuhusu ubora na umuhimu wa maonyesho hayo katika muktadha wa
gharama kubwa zinazotumika kuyaendesha.
Kama tulivyosema hapo juu, kimsingi wakulima ndio
walikuwa walengwa wakubwa wa maonyesho hayo, lakini sote tumeshuhudia
Serikali na wanasiasa wakiyapa sura ya kibiashara, huku wakulima
wakipigwa changa la macho.
No comments:
Post a Comment