TASWIRA ya kimataifa ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye katika siku za hivi karibuni aliibua mzozo wa kidiplomasia na Rais Jakaya Kikwete, inaonekana kuchukua mwelekeo wa kuchuja badala ya kustawi kwa namna ilivyokuwa miaka michache tu iliyopita, MTANZANIA Jumapili limebaini.
Baada ya kuvuma kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Kagame, aliyekuwa akibeba taswira ya mtu shupavu na shujaa, amegeuka na kuanza kuonekana kiongozi mpenda vita, makuu na rais anayeweza kusababisha kuibuka na kukua kwa ufa mkubwa wa kimahusiano kati yake binafsi na viongozi wenzake wa ukanda huu wa Afrika.
Nje ya bara hili, kuzorota kwa taswira ya kiongozi huyo kunaonekana kuanza kugusa hisia za wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanadiplomasia wanaoheshimika na viongozi wakuu wa mataifa ya Ulaya, Marekani na ndani ya Umoja wa Mataifa.
Siku chache baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kukaririwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani akimtaka Rais Kagame kuacha kukisaidia kijeshi kikundi cha waasi wa M23, kidole hicho cha lawama kinaonekana kuungwa mkono kwa kasi na makundi mengine ya kimataifa.
Kagame, ambaye kwa miaka mingi amekuwa kiongozi kipenzi cha mataifa ya Ulaya na hasa Marekani tangu alipofanikiwa kumaliza mapigano yaliyosababisha mauaji ya halaiki nchini kwake mwaka 1994, katika siku za hivi karibuni taswira yake inaonekana kubadilika na kuchukua mwelekeo wa lawama zaidi kuliko sifa.
Matamko na maandishi yenye mwelekeo wa lawama ambayo yalitolewa dhidi yake katika siku za hivi karibuni yameanza kuchukua mwelekeo unaoonyesha kwamba Kagame wa sasa si yule tena aliyekuwa akitajwa kuwa mfano wa kuigwa wa viongozi wapenda maendeleo na wazalendo wa kweli katika Afrika.
Tukio la hivi karibuni kabisa, ni makala ya uchambuzi iliyochapishwa katika gazeti la Uingereza la The Telegraph, ambayo ilieleza namna majeshi ya Rwanda yalivyokuwa yakijipenyeza ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kutoa misaada ya silaha na vyakula kwa kundi la waasi wa M23, ambalo limekuwa likipigana Mashariki mwa nchi hiyo tangu mwaka 2010.
The Telegraph katika makala yake hiyo lilidurusu ripoti ya Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Right Watch, iliyotolewa mwezi mmoja uliopita, ambayo pamoja na mambo mengine, iliainisha ushahidi wa namna vikosi vya Jeshi la Rwanda vilivyokuwa vikishiriki katika vitendo vya kiharamia ndani ya DRC.
Katika uchambuzi wa ripoti hiyo, The Telegraph limeainisha kwamba ndani ya Rwanda, wanaume na vijana wadogo wenye umri wa miaka 15 wamekuwa wakilazimishwa kupewa mafunzo ya kupigana kijeshi kwa lengo la kulinda maeneo yenye utajiri wa madini katika mpaka wa nchi hizo mbili.
The Telegraph limeandika kuwa licha ya utetezi wa awali wa Uingereza juu ya misaada inayopelekwa Rwanda kuwa haimaanishi nchi hiyo inakwenda vitani Kongo, lakini sasa uhalisia wa tuhuma dhidi Rwanda umejiweka hadharani.
Andrew Mitchell, Katibu wa zamani wa Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa nchini Uingereza, alikuwa mstari wa mbele wa kumtetea Rais Kagame dhidi ya shutuma za kuchochea mapigano Kongo, pamoja na kupingwa vikali na mbunge wa nchi hiyo, lakini Julai mwaka jana alifanikiwa kuidhinisha msaada wa pauni milioni 16 kwa ajili ya serikali ya Rwanda.
Awali Mitchell alipata kumshawishi Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kwamba madai yaliyokuwa yakiihusisha serikali ya Kagame na tuhuma za kuwaunga mkono waasi wa M23 hayakuwa na ukweli.
Ushawishi huo ambao ulipingwa vikali na wabunge wa nchi hiyo katika mjadala wa bajeti ya misaada, hatimaye ilisababisha Mitchell alazimike kung’atuka katika nafasi hiyo ya uongozi kwa sababu za kisera.
Kitendo cha wabunge kupinga mtazamo huo wa Mitchell kutokana na kuwa na imani yao kwamba Rwanda imekuwa ikisaidia kundi la waasi wa M23, mrithi wa kiti chake, Justice Greening, alilazimika kufuta misaada ya kifedha kwa taifa hilo yenye thamani ya jumla ya pauni milioni 21 mwishoni mwa Novemba, mwaka jana.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kagame alipata kukaririwa akieleza namna alivyokuwa akikerwa na maamuzi ya Jumuiya ya Kimataifa kuikatia misaada Rwanda, hatua alizozielezea kwamba zitalifanya taifa hilo liendelee kustawi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ziliibuka tuhuma zilizoelekezwa kwa Kagame na Majeshi ya Rwanda kwa namna walivyokuwa wakishiriki katika mapigano ndani ya DRC.
Alikuwa ni Balozi wa Kudumu wa Ufaransa ndani ya baraza hilo, Alexis Lameck, ambaye alikariri taarifa za kutoka kwa Msemaji wa UN aliyeko Kinshasa nchini Kongo, Edmond Mulet, ambazo zilikuwa zikiinyooshea Rwanda kidole cha namna ilivyokuwa ikishirikiana na M23.
Shutuma mpya dhidi ya Kagame zinakuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja sasa, tangu gazeti hili la MTANZANIA Jumapili lilipoandika kwa mara ya kwanza namna taswira ya sasa ya kiongozi huyo inavyoweza kuwa mwanzo wa hatma mbaya kwake.
Katika gazeti hilo, ilielezwa namna Kagame anavyokabiliwa na hatari ya kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kama ilivyopata kuwa kwa aliyekuwa Rais wa Liberia, Charles Taylor.
Kama ilivyo kwa Kagame anavyohusishwa na vita ya Kongo, Taylor alituhumiwa kwa miaka mingi kama mbabe wa vita vya Sierra Leone, ambayo iligharimu maisha ya takribani zaidi ya watu 50,000.
Kwa sasa Taylor anatumikia kifungo cha miaka 50 jela, baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita nchini Sierra Leone.
Ngorongoro |
No comments:
Post a Comment