Miaka 50 baada ya kufariki ;
Watafiti wagundua
kazi zaidi za Shaban Robert
Kipimo |
Komba |
Hakuna apingaye kuwa Shaban Robert alikuwa manju
wa fasihi ya Kiswahili, ambaye hata baada ya miaka 50 tangu kifo chake
mwaka 1962, hakuna aliyejitokeza kumpiku kwa kiwango alichofikia katika
fani ya fasihi.
Mpaka sasa kazi zake nyingi bado zinaishi, huku zikiwa zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali na kusambazwa kote duniani.
Bila shaka, mtu huyu anabaki kuwa miongoni mwa
watu muhimu waliowahi kutokea nchini. Lakini inashangaza kuwa familia
yake na hata historia yake vimetelekezwa!
Hata mahala lilipo kaburi lake katika kijiji cha
Machui, Kusini mwa Jiji la Tanga, pameshindwa kuendelezwa japo kwa kuwa
na makumbusho madogo ya mwanafasihi huyo aliyetamba ndani na nje ya
mipaka ya Tanzania.
Kimsingi, eneo hili mbali ya kuwa sehemu muhimu
katika historia ya nchi, pia lingeweza kutumika kama darasa la
kuwakusanya watu, hasa watafiti na wanahistoria kutoka pembe zote za
dunia. Ukitoa simulizi isiyovutia ya kusahauliwa kwa Shaban Robert,
baada ya utafiti wa miaka mingi kuna habari mpya za kugunduliwa kwa kazi
nyingine za gwiji huyo.
Kwa mujibu wa mwanafasihi bobezi nchini, Profesa
Mugyabuso Mulokozi, aliyeshiriki katika utafiti huo, kazi hizi
hazikuwahi kufahamika awali.
Anasema katika utafiti wao mpya wamegundua
mafungu ya barua ambayo Shaabani Robert aliyaweka katika makundi ya
nyaraka za kifamilia, kazi na ajira, pamoja na kiofisi.
‘’Baadhi ya barua zinahusu uhusiano kati ya mtu
na kaka yake. Shaaban Robert alijipa jukumu la kulea, anazungumzia
umuhimu wa mtu kutenda mema na umuhimu wa elimu katika dunia
hii’’anabainisha.
Pia anasema katika utafiti huo wamebaini makala
za mashairi alizopeleka kwenye mashindano, na kuwa mashairi hayo bado
ni muswada yakisubiri kuchapishwa.
Misukosuko ya kisiasa
Miongoni mwa mambo yanayoibua maswali kwa
wanafasihi wa sasa ni namna Shaaban Robert alivyoweza kuepuka misukosuko
ya kisiasa, hasa enzi za ukoloni kwani baadhi ya kazi zake zipo
zilizokuwa zikipinga unyanyasaji wa Waafrika.
Jambo hili pia limebainika katika utafiti huo mpya. Inadaiwa
kuwa katika vita Kuu ya Pili ya Dunia(1939-1945), aliandika utenzi wa
vita hiyo akiisifia Uingereza kuwa ilikuwa na haki dhidi ya dola ya
Wajerumani.
Utenzi huo haukuifurahisha Ujerumani na gwiji
huyo wa fasihi ya lugha ya Kiswahili aliwekwa katika orodha ya watu
watakaonyongwa endapo Wajerumani wangeshinda vita.
Aidha, kwa mujibu wa Profesa Mulokozi miongoni
mwa kazi zilizogunduliwa, ni sehemu ya utenzi alioandika akilalamikia
kuhamishwa vituo vya kazi mara kwa mara.
Sehemu ya utenzi huo inanukuliwa ikisema:
’Nimezaliwa Tanga 1909, tangu utoto sina kituo hasa, naona sina siasa ila kuandama njia’’
Mashairi mengine yanatajwa kuwa yanaelezea mila za watu wa Tanga.
Katika kazi mpya zilizogunduliwa pia anazungumzia
jinsi watu walivyoweza kupata tiba. Kwa mfano, anasema mtu alipougua
alikwenda kwenye tambiko, msikitini kuombewa au hospitali.
Akimzungumzia Shaaban Robert, mwanafunzi wa
Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Felix Sosoo
anasema kuwa alikuwa ni mtunzi aliyeheshimika na ametoa mchango mkubwa
kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Mwanafunzi huyo kutoka Ghana anasema amefika
nchini kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili na baada ya masomo atarudi
Chuo Kikuu cha Ghana kama mtaalamu wa lugha hiyo.
Anasema anajivunia kusomea katika nchi anayosema
ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili na kuwa lugha hiyo ni utambulisho
wa utamaduni wa Afrika. Matarajio yake ni kubobea na kuwa mtalaamu zaidi
wa lugha hiyo.
‘’Nimetoka Ghana kujifunza Kiswahili ambayo ni
kama lugha ya Afrika, hapa najifunza Kiswahili fasaha. Lugha hii
itanirahisishia kujifunza lugha nyingine pia’’ anasema Sosoo
Akitoa maoni yake kuhusu umahiri wa Shaaban
Robert, msanii wa Kimataifa John Mugango, anasema mtunzi huyo ameacha
somo kwa Taifa kuendeleza watu wake kulingana na vipaji
walivyonavyo.
Anasema vipaji vingi vinapotea kwa kutoendelezwa na kuwa badala
yake wanapatikana wataalamu wanaofanya kazi kwa shinikizo la kukosa
ajira na siyo kwa sababu ya kupenda kazi husika.
‘’Tusomee vipaji vyetu, ukiona daktari
anakukaripia baada ya kumfikisha mgonjwa hospitali, ujue huyo ana damu
ya ajira katika kazi yake na siyo udaktari wa kujitambua’’anabainisha
Mugango
Naye Mwalimu Domician Domonick kutoka Shule ya
Sekondari Bukoba, anashangaa gwiji huyo kutopewa shahada ya heshima na
taifa, kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kukuza lugha ya
Kiswahili.
Anasema Shaabani Robert ana mchango mkubwa katika
kuifanya lugha hiyo iheshimike duniani. Analalamika kuwa hivi sasa
Serikali inapitisha vitabu vya kufundishia lugha hiyo ambavyo maudhui
yake ni dhaifu.
Anasema vitabu vinavyotumika hivi sasa vingi
havina mantiki ya fasihi na kwa vyovyote haviwezi kulinganishwa na vile
vilivyotungwa na Shaaban Robert. Anarejea baadhi ya vitabu vyake kama
vile Mapenzi Bora kinachoonyesha umuhimu wa elimu.
Kauli ya mtoto wa Shaban Robert
Ikbal Shaaban ambaye ni mtoto wa Shaaban Robert anasema kazi za baba yake hazijasaidia kuboresha maisha ya familia aliyoiacha.
Anaeleza kuwa wapo wajanja wanaofaidika na jasho
la baba yao na kuwa hakuna pato linaloingia katika familia yao kutokana
na mauzo ya kazi hizo.
‘’Bado hatujaona faida ya kazi zake zaidi ya
kuitwa kwenye semina, kuna wajanja wanaonufaika na jasho lake,tuko
mbioni kuanzisha vita mpya dhidi ya kazi za marehemu’’ analalamika.
Ikbal anadai kuwa gwiji huyo wa lugha ya
Kiswahili hajapewa heshima ya kutosha na Taifa, licha ya kuwa kazi zake
zinaendelea kutumika kuendeleza na kuitangaza lugha hiyo.
Kwa hali yoyote ile, huu ni wakati wa kumuenzi
Shaaban Robert kwa kutambua mchango wake kwa taifa, huku tukiendelea
kuwaandaa wanafasihi wengine wa baadaye.
Home |
No comments:
Post a Comment