SEHEMU YA PILI:
Matukio ya Kisiasa
Mji wa Bor, Sudan Kusini wadhibitiwa
na wanajeshi waasi
Jeshi la Sudan Kusini limesema
haliudhibiti tena mji muhimu wa Bor, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa jeshi
hilo kukiri kushindwa katika mapigano yanayoendelea kwa siku ya nne sasa kati
ya makundi pinzani ya wanajeshi.
Mapigano hayo makali yanatishia
kuitumbukiza nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Msemaji wa Jeshi la
Sudan Kusini, Kanali Philip Aguer, amesema leo (19.12.2013) kuwa wanajeshi
waasi wanaomtii aliyekuwa makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar wameutwaa mji
wa Bor.
Amesema viongozi katika mji huo
ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei, hawapokei simu zao, hatua inayoifanya
serikali kuu kuamini kwamba wamejiunga na waasi.
Kanali Aguer amesema wamepoteza
udhibiti wa mji wa Bor na kwamba milio ya risasi imesikika usiku kucha ingawa
bado hawana taarifa kuhusu waathirika au watu walioyakimbia makaazi yao kwa
sababu operesheni za kijeshi bado zinaendelea.
Watu 19 wauawa Bor
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Martin Nesirky amesema raia 19 wameuawa katika mji wa Bor, akifafanua
kuwa taarifa hizo zimetolewa na shirika la Msalaba Mwekundu nchini Sudan
Kusini.
Amesema wasiwasi pia umeongezeka
katika majimbo ya Unity na Upper Nile na mji wa Torit na mapigano yamesambaa
katika miji mingine ya taifa hilo tajiri kwa mafuta.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini,
Michael Makuei Lueth, amesema kiasi watu 500, wengi wao wakiwa wanajeshi,
wameuawa na wengine 700 wamejeruhiwa katika mapigano hayo yaliyoanza wakati wa
jaribio la mapinduzi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Rais Salva Kiir amesema yuko tayari
kuanza mazungumzo na makamu wake aliyemfukuza kazi mwezi Julai, Riek Machar.
Kiir anamlaumu Machar kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa na kwa
kuanzisha mapigano. Hata hivyo, Machar amekanusha madai hayo.
IGAD na juhudi za kumaliza mapigano
Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya
nje kutoka mataifa manne ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Mashariki na Pembe
ya Afrika-IGAD, wameelekea Sudan Kusini kuanza juhudi za kumaliza mapigano hayo
yanayozusha hofu ya kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mawaziri hao
wanatokea Kenya, Djibouti, Ethiopia na Uganda.
Kwa upande wake Marekani imeelezea
wasiwasi wake mkubwa kuhusu mapigano ya Sudan Kusini, huku Waziri wake wa mambo
ya nje, John Kerry akitoa wito wa kuwepo utulivu. Marekani na Uingereza
zimeanza kuwaondoa wafanyakazi wake kutoka Juba.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki-Moon alisema jana Jumatano (18.12.2013) kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na
mzozo wa kisiasa ambao unaweza ukasambaa zaidi na unatishia kuitumbukiza nchi
hiyo kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Maelfu ya raia wa Sudan Kusini
wameyakimbia makaazi yao na kwenda kutafuta hifadhi kwenye ofisi za Umoja wa
Mataifa tangu yalipozuka mapigano siku ya Jumapili.
No comments:
Post a Comment