Saturday, 17 August 2013

Haba na haba Bado si haba

Wanaotaka penzi la siri 

wengi ni matapeli



NI wazi wajinga duniani hawawezi kwisha, ndio maana kwenye jamii utashangaa kuona baadhi yao wanafanya mambo yanayoshangaza umati.
Pamoja na kushangaza huko, lakini watu hao hawawezi kugundua kuwa wanachofanya au kufanyiwa kinaibua maswali kwa wengine.
 
 
Wawili wapendanao pichani.
Nasema haya, huku nikiamini kuwa mambo hayo yapo na yataendelea kuwapo katika jamii. Ndugu msomaji wangu, kwenye jamii yetu, wapo watu waliokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na wapenzi wao, tena wakiambiana kuwa wanapendana kwa dhati.
Lakini sio kweli. Ni uongo tu. Kwanini nasema hivyo? Siku zote wawili hawa wanaoambiana wanapendana kwa dhati, baadhi yao hupenda sana mapenzi ya siri.

Hawapendi hata wengine wajuwe kwa sababu wanazojua wenyewe. Najua ndio kuna utamu wake  mapenzi ya siri, ila kwa undani zaidi inaonyesha watu wanaoamua kufanya penzi hilo la siri hawapo huru.
Kujificha huko ni ishara kuwa huwenda wanadanganya. Huwenda mmoja wapo yupo kwenye uhusiano kwa zaidi ya mmoja.
Kama sio mwanaume basi atakuwa mwanamke. Kuna uzuri wake wapenzi kuishi kwa kujiachia. Hii hutokea kama watu hao wamejiweka wazi.
Kama wazazi wanajua uhusiano wao kwa wale wasiokuwa watoto chini ya miaka 18, kwanini muendelee kufanya siri?
Nani mwingine anaogopewa? Kuna hatari kuwa ndugu yangu unaiba penzi la watu. Inapoonekana kuwa wewe ndio mwizi utasemaje?
Hii ni kwasababu tangu mwanzo hujakuwa mkali na kupinga hilo penzi la siri. Wakati mwingine mtu anaulizwa juu ya ukaribu wake na mtu Fulani.
Lakini majibu yake hushangaza wengi. Anajibu ni rafiki yake. Majibu haya hutolewa bila kuangalia kama anayezungumza naye ni ndugu au rafiki tu.
Huu ni uwendawazimu wa aina yake. Kuna kila sababu ya kuangalia nyendo zako msomaji wangu. Sikatai wawili wanaweza kujificha kwa faida wanazojua wenyewe, ila wakati mwingine wapenzi wetu hutumia nafasi hiyo kutusaliti na kutoka na wengine.
Lazima uwaze kwanini mtu wako anahitaji usiri zaidi katika penzi lenu? Je, hakuna njia ya mkato anayopita mtu wako? Je, hakupotezei muda?
Unaweza kukaa na mtu na kuendelea na penzi lenu la siri, ila baadaye unagundua kuwa yupo kwenye uhusiano na mtu mwingine na wapo kwenye mpango wa kufunga ndoa.
Sauala hilo litakusumbua kichwa. Lakini haya yote utakuwa umepoteza mwenyewe muda. Mara nyingi anayefanya siri katika uhusiano wako, basi ana uwezo wa kutoka na mwingine bila hata kujuana.
Kila mtu anaambiwa ni rafiki. Kila mtu afiche siri. Kwanini? Wewe ni mwanafunzi? Bado ni mdogo kiasi cha kuogopa kuwa wazi katika mapenzi?
Kama bado ni mdogo hupaswi kabisa kuwa kwenye uhusiano na kama ni mwafunzi endelea na shule. Acha kupoteza muda wa watu kwasababu ya uhuni wao.
Ndugu msomaji wangu, kama wewe ni mhusika katika hilo, hebu jaribu kumgomea mpenzi wako na umwambie muda wa kujificha umepitwa na wakati.
Mueleze ni wakati sasa wa kuwa huru. Hii ni kwa wale waliofikia umri wa kuwa na wapenzi au wachumba, maana ina uzuri wake.
Mwanamuziki Hussein Jumbe aliwahi kuimba wimbo wake uliojulikana kama ‘Mapenzi ya Siri’. Ni wazi mapenzi haya yanasumbua na hayana uhuru.
Hata kumshika mkono mpenzi wako itakuwa ngumu kwasababu mnafanya siri. Pamoja na yote hayo, mwisho wa siku unaweza kufa kwa presha utakapogundua kuwa mtu wako yupo kwenye uhusiano na mtu mwingine.
Sikatai usiri huo kama ni maridhiano ya wote wawili, lakini pia ni wakati wa kupeana ukweli wa jambo hilo, hasa kama hakuna kizuizi cha wawili hao kuwa kwenye uhusiano.
Napinga usiri wa wapenzi ambao hutumia fursa hiyo na kuendelea na uhuni kwa kutoka kimapenzi licha ya kuwa kwenye uhusiano na mtu wake.
Tukutane wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment