Waislamu wasali chini ya
ulinzi mkali wa polisi
 Ulinzi mkali jana uliimarishwa jijini Dar es 
Salaam baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba waumini wa Kiislamu 
wataandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu 
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa 
Ponda.
 Ulinzi mkali jana uliimarishwa jijini Dar es 
Salaam baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba waumini wa Kiislamu 
wataandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu 
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa 
Ponda.
Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha 
kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda Hospitali ya 
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kumuweka Gereza la Segerea.
Kiongozi huyo alikuwa amelezwa MOI kwa madai ya kupigwa risasi begani akiwa mjini Morogoro.
Hata hivyo, akiwa bado anatibiwa MOI, Jumatano 
alisomewa shtaka la uchochezi akiwa kitandani na Mwendesha Mashtaka wa 
Serikali, Tumaini Kweka akidaiwa kutenda kosa hilo katika maneo 
mbalimbali ya nchi kati ya Juni 2 hadi Agosti 11, mwaka huu.
Kutokana na fununu za baadhi ya waumini kupanga 
kufanya maandamano, ulinzi uliimarisha maeneo mbalimbali ya jiji hususan
 misikiti ambayo inadaiwa wanasali wafuasi wake.
Msikiti wa Mtambani
Waumini katika Msikiti wa Mtambani jana waliswali 
swala ya Ijumaa katika usimamizi mkali wa magari matano ya askari wa 
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Hata hivyo, hali katika mazingira ya msikiti huo 
ilikuwa ni tulivu huku waumini wakisikiliza kwa makini kila kinachosemwa
 na viongozi wao, huku taratibu za ibada zikiendelea kama kawaida licha 
ya kuwepo kwa ulinzi mkali.
Mapema kabla ya kuswali swala ya Ijumaa ambayo 
iliswaliwa saa saba za mchana, gari tano za kikosi cha kutuliza ghasia 
zenye askari waliovalia kivita na zana za kazi ikiwemo bunduki, yalikuwa
 yameegeshwa mbele ya lango kuu la msikiti huo, kitu kilichofanya 
litolewe tangazo msikitini hapo la kuwataka Waislamu kuja kuswali bila 
kuogopa vitisho vya magari hayo.
Saa 5:18, lilisikika tangazo kutoka msikitini hapo
 ambalo lilisema, “Njooni msikitini msiogope vitisho vyao, hatutafanya 
vurugu lakini kama wanataka kupambana na sisi waje na tutapambana nao,” 
ilisikika sauti ya mtoa tangazo ndani ya kipaza sauti.
Baada ya swala magari ya askari yalipungua na 
kubaki magari matatu ambayo hadi saa 9:45, bado yalikuwa yameweka kambi 
upande wa pili wa barabara kwenye eneo ulipo msikiti huo.
Wakati wa ibada waumini hao walionyesha hisia zao 
baada ya kusomwa dua ya zaidi ya saa moja na nusu kama ambavyo hufanya 
kwenye swala ya alfajiri, na kilio kikatanda msikiti mzima yaani kwa 
upande wanawake na wanaume.
Baada ya ibada alisimama kaka mkubwa wa Sheikh Ponda, Maabadi 
Issa Ponda na kusema kuwa wao kama familia wapo pamoja na waumini wa 
taasisi hiyo na hawajahuzunishwa hata kidogo na kilichomtokea ndugu yao 
kwa kuwa anafanya kazi ya Mungu, huku akisisitiza akaze uzi afanye zaidi
 ya alichokifanya malipo yake atayakuta mbele ya haki.
Mwisho wa ibada hiyo waumini waliamrishwa na 
viongozi wao kuondoka eneo hilo kwa kukwepa kuonekana wanafanya fujo na 
kuwapa nafasi wanaotaka kuwakamata baadhi ya masheikh kupata nafasi 
hiyo.
Kitu kilichokuwa sio cha kawaida ni wanawake 
wawili waliodaiwa kuwa Usalama wa Taifa kukamatwa wakiwa wamejipenyeza 
msikitini humo, huku wakiwa na rangi za kucha kitu ambacho Waislamu 
hawafanyi na kuwa na nywele za bandia kitu ambacho pia kwa Muislamu 
ambaye anaswali hawezi kuingia nazo msikitini na kuzuiliwa kuendelea 
kuwepo eneo hilo.
Hapo awali Saa 4:00 asubuhi Msemaji wa Jumuiya 
hiyo, Rajabu Katimba alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti Sheikh Juma 
Saidi Ally, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa kitendo 
alichofanyiwa Ponda na kwa kupigwa risasi na kutolewa hospitali wakati 
akiwa anapatiwa matibabu na kinyume cha haki za binadamu, utawala bora 
na uhuru wa maisha ya mtu.
Alisema jumuiya hiyo inapinga kwa kauli moja tume 
iliyoundwa na polisi kuchunguza tukio hilo, na hawatatoa ushirikiano wa 
aina yoyote katika tume hiyo.
Katimba alisema kuwa kutokana na tukio hilo, 
jumuiya hiyo imeitisha mkutano wa dharura utakaofanyika Viwanja vya 
Nurul- Yakin siku ya Jumapili saa 9:00 alasiri, kutafakari kwa pamoja na
 hatimaye kuchukua hatua za msingi zitakazoleta tija ya kweli ili 
viongozi wa Kiislamu wasiendelee kudhalilishwa.
“Hatupingi kukamatwa, wala kusomewa shitaka kwa 
kuwa ndiyo sheria, tunachopinga ni jinsi alivyokamatwa na kunyang’anywa 
haki yake ya kutibiwa,” alisema Katimba.
Mitaa ya Kariakoo
Misikiti mbalimbali ya Kariakoo kama Idrissa na 
Mtoro hapakuwa na maandamano wala fujo zozote zile na waumini 
walionekana kuhudhuria wengi kwenye ibada.
Katika misikiti hiyo askari polisi walionekana 
wakiwa wamesimama na silaha zao tayari kwa kupambana na fujo zozote 
ambazo zingeweza kutokea endapo maandamano yangefanywa kama ilivyo kuwa 
imepangwa, lakini hali ilionekana kuwa tulivu baada ya maandamano hayo 
kuahirishwa.
Baada ya ibada waumini hao walionekana 
wakisambaratika kwenda maeneo yao ya kazi huku askari nao wakiendelea na
 ulinzi ili kuahakikisha utulivu na amani.
Kwa ujumla eneo la Kariakoo lilikuwa tulivu huku 
watu wakiendelea na kazi zao kama kawaida licha ya kwamba wengi 
walihofia pengine kungekuwa na fujo endapo maandamano yangefanywa na 
waumini hao wa kiislamu.
Msikiti wa Idrissa
Msikiti wa Mchangani
Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu 
nchini, Musa Kundecha amesema vyombo vya usalama na Watanzania kwa 
ujumla wamepotoshwa na taarifa kuwa waislamu walipanga kuandamana baada 
ya sala ya Ijumaa kupinga kupelekwa gerezani Katibu wa Taasisi za 
Kiislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kundecha aliyasema hayo mara baada ya sala ya 
Ijumaa katika msikiti wa Mchangani na kuongeza kuwa wamepanga kufanya 
mkutano na waislamu wote utakaofanyika viwanja vya Mwembe yanga siku ya 
jumapili saa9 jioni na sio maandamano kama ambavyo iliripotiwa na baadhi
 ya vyombo vya habari na vyombo vya usalama kuamini na kuanza kutoa 
vitisho.
Pia alisema serikali kupitia chama tawala 
haiongozi taifa katika dhana ya utawala bora, badala yake wanatumia 
mabavu kuwanyamazisha wananchi wanaojitambua na kudai haki zao suala 
ambalo kwa waislamu halikubaliki hata kidogo.
“Hakuna kiongozi aliyeitisha maandamano kwasababu 
tunatambua suala la katibu( shekh Ponda) ni la kisheria ila 
nimeshangazwa na kauli za vitisho toka kwa vyombo vya usalama.
Aliongeza kuwa, suala linalowaumiza Waislamu si 
kupelekwa gerezani kwa Shekh Ponda bali ni kitendo cha vyombo vya 
usalama kumpeleka gerezani ikiwa bado analalamikia maumivu makali ya 
bega pamoja na kutokubebwa kwa dawa alizoandikiwa na daktari.
Kundecha kwa kile alichokiita taarifa kwa waislamu
 alisema ni lazima wakutane siku ya Jumapili, na kusema kuwa vyombo vya 
usalama ni waalikwa namba moja katika mkutano huo ili waweze kujua 
ukweli wa mada watakazojadili waislamu ikiwemo suala la Shekh Ponda na 
sio kuchukua taarifa zisizo na uhakika na kuaza kutoa vitisho.
Msikiti wa Idrissa
Katika msikiti wa Idrissa uliopo Kariakoo wilayani
 Ilala, baada ya ibada ya saa 7 mchana kuisha baadhi ya waumini 
walionekana wakiwapa wenzao waraka unaohusu tukio la Sheikh Ponda Issa 
Ponda.
Waraka huo ulionekana ukigombaniwa waumini wa 
msikiti huo huku ukiwa na ujumbe wa kulaani kitendo cha Sheikh Ponda 
kupigwa risasi..
Wakati huohuo, polisi waliendelea kuimarisha ulinzi katika mitaa mbalimbali ukiwamo wa Msimbazi ambao upo karibu na msikiti huo.
Polisi hao waliokuwa na mbwa huku wengine 
wakitumia pikipiki kufanya doria kwa kile walichodai kuwa Waislamu 
wamepanga kufanya maandamano licha ya kupigwa marufuku jana.
Katika msikiti wa Mtambani wilayani Kinondoni, baada ya ibada 
kuisha baadhi ya makundi ya waumini yalionekana yakijigawa kuingia 
mitaani huku wengi wakihamisishana kuandamana lakini hawakufanya hivyo.

No comments:
Post a Comment