Taka mwili zinavyogeuzwa
na kuwa malighafi
Uchafu wa hali ya juu…usiofaa kwa kutazama, wala kuutumia kufanya kazi fulani, umegundulika kuwa na manufaa lukuki kwa matumizi ya binadamu. Uchafu huo si mwingine bali ni kinyesi cha binadamu pamoja na mkojo.
Mfumo wa usafi wa mazingira ya kiikolojia
hautiliwi maanani hapa nchini, pamoja na kufafanuliwa kwa kina na
wataalamu mbalimbali, lakini bado imekuwa ni vigumu kwa Watanzania
kuitilia maanani na kuitumia kwa tija.
Barani Asia, taka mwili zimekuwa zikihifadhiwa na
kufanyiwa utafiti kwa miaka zaidi ya 1,000, huku mfumo huo ukilindwa
katika vifungu vya sheria ya kutunza taka ya mwaka 1988, Korea ya
Kusini.
Kitaalamu mfumo huo unajulikana kama Ecological
Sanitation System, ambao unatumia taka mwili za binadamu na kuzirejesha
katika matumizi yenye thamani huku ukitunza mazingira.
‘Taka mwili’ zinafaa kwa nishati
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Fredrick Mwanuzi anasema kama usimamizi wa mazingira
utazingatiwa basi ipo haja ya kufanyia utafiti taka mwili kwa ajili ya
matumizi mbalimbali kwa sababu zina manufaa makubwa katika nyanja
mbalimbali.
Mwanuzi anasema wakati umefika sasa kinyesi cha
binadamu kichukuliwe kama malighafi badala ya uchafu na kutumia mbolea
hiyo kwa ajili virutubisho vya kilimo, nishati, pamoja na dawa za
binadamu.
“Kilo 25 hadi 50 za kinyesi huzalishwa na mtu
mmoja kwa mwaka, hii ni sawa na kilo 0.55 nitrogen, 0.18 phosphorus na
0.37 potassium, vilevile binadamu huzalisha kiasi cha lita 400 za mkojo
kwa mwaka ambazo huwa na kg 4.0 nitrogen, 0.4 phosphorus na 0.9 za
potassium,” anasema.
Wataalamu wa mazingira nchini Tanzania walijaribu
‘taka mwili’ kuzifantia mchakato wa kitaalamu ili kuwa malighafi,
walichagua eneo la Majumba Sita jijini Dar es Salaam lengo kubwa likiwa
ni kuzuia kinyesi kinachotoka chooni kuchafua maji ambayo yapo ardhini.
Mtaalamu wa mazingira Esnati Chaggu alifanya
utafiti na kugundua kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Jiji la Dar
es Salaam wanatumia vyoo vya shimo ambavyo vinachafua maji yaliyomo
ardhini huku watu wengi wanategemea maji ya visima vyenye urefu zaidi ya
meta 6.75 pamoja na mabomba ambayo huathiriwa na kinyesi kinachofukiwa
ardhini. “Maji yaliyoko ardhini yanaathiriwa na aina ya vyoo ambavyo
Watanzania wanavitumia, asilimia 90 hutumia vyoo vya shimo.
“Tulichagua eneo la Majumba Sita ambalo lina
asilimia kubwa ya visima vyenye kina kifupi na wakazi wengi wanatumia
vyoo vya shimo na wengine hawana kabisa na wanajisaidia vichakani,”
anasema.
Kutokana na mazingira hayo walibuni namna ya
kuhifadhi kinyesi cha binadamu kwa manufaa na pia kutunza mazingira hasa
maji ambayo yalisababisha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kama
kipindupindu na kuharisha.
“Tulibuni teknolojia ya Ecosan, (usafi wa mazingira) ambayo vyoo
vilitumika katika kudhibiti taka mwili, vyoo vya aina mbili
viligunduliwa cha kwanza ni kile cha kuchuchumaa na kukaa ambavyo
viliwekewa sehemu ya kutenganisha mkojo,” anasema Chaggu.
Anafafanua kwamba mkojo ulielekezwa kupita katika
bomba kuelekea katika chombo cha plastiki chenye ujazo wa lita sita
ambacho huwekwa nje ya choo na kuchimbiwa ardhini, taka hizo huhamishwa
baada ya siku 13 baada ya chombo kujaa wakati huo kinyesi hukusanywa
sehemu nyingine moja kwa moja kutoka katika choo cha kuchuchumaa.
“Lakini ili yabaki maji machache katika kinyesi
majivu humwagiwa katika shimo la choo kila baada ya kujisaidia, njia hii
ni bora katika kupunguza harufu na maambukizi ya magonjwa,” anasema.
Aina ya pili ni choo cha kukaa cha 96 Ecosan au
‘Ecological Sanitation’ . Dk Mwanuzi anaeleza kwamba taka mwili, kinyesi
kigumu hutenganishwa na mkojo.
“Hii ina usalama zaidi kwa matumizi bila wadudu
wabaya. Ukitenga mkojo una bei nzuri sokoni kwa kuwa unauza kama mbolea
ya UREA,” anasema
Kilimo Kwanza
Professa Mwanuzi anasisitiza matumizi ya kinyesi
cha binadamu kwa wakulima hasa katika mkakati wa Kilimo Kwanza na
nishati kwa wakazi wa vijijini.
Anasema kinyesi cha binadamu pia kinatumika
kutengeneza nishati ya gesi ambayo kitaalamu huitwa ‘biogas’ ambayo
inafaa zaidi kuendeshea injini, umeme na kupikia.
“Gesi hii ina manufaa kwa familia zilizoko vijijini kwa ajili ya kuzalisha umeme,” anasema.
No comments:
Post a Comment