Wakuu wa majeshi wazua utata;
washauri rais asiwateue
Mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, kuhusu Rais kuwateua Wakuu wa Majeshi Nchini, yamezua mvutano kwa Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Liwale, Mkoani humo, wakipinga mapendekezo hayo na wengine wakiyaridhia.
Hayo yalijitokeza juzi wakati wa mkutano wa
kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na wajumbe hao kueleza
kuwa Rais kuwateua wakuu wa majeshi hawatatenda haki dhidi yake.
Baadhi walieleza Rais ni Mkuu wa Nchi hivyo jukumu
hilo kutokufanywa na yeye ni kuhatarisha usalama wa taifa na wakati
wowote nchi inaweza kupinduliwa. Akiwasilisha maoni ya kundi la tatu,
Juma Mangora alisema Mkuu wa Majeshi asiteuliwe na Rais, bali jukumu
hilo lifanywe na Baraza la Taifa la Ulinzi.
“Kama Mkuu wa Majeshi atateuliwa na Rais kutakuwa
na kila hila ya kulipa fadhila na inakuwa vigumu kumchukulia hatua kali
pindi atakapokiuka taratibu kutokana na kujuana zaidi,” alisema Mangora
na kuongeza: “Ili kuleta uwajibikaji wa Jeshi hilo, Baraza la Taifa la
Ulinzi likichukua jukumu hilo litamfanya hata Mkuu huyo wa jeshi
kutokumwogopa Rais na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.”
Naye Mohamed Dondwa alisema Mkuu wa Jeshi la
Polisi anatakiwa kupatikana kupitia Baraza la Wakuu wa Polisi kutokana
na wao kumjua yupi anayestahili. Alisema kumpata Mkuu wa Polisi kupitia
kuteuliwa na Rais hakutakuwa na utendaji uliotukuka miongozi mwa jeshi
hilo na wananchi kuendelea kulilalamikia kutokana na kutokutenda haki
kila kukicha.
Kwa upande wake, Hashim Majanjagara alisema
kuwapata wakuu wa majeshi pasipo Rais kuhusika kuwateuwa nchi inaweza
kupindiliwa pasipo kujua. “Rais ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama hivyo yeye ndiye anatakiwa kuwateuwa bila kufanya
hivyo na kutumia njia nyingine wanaweza kumsaliti kwa kushawishiwa na
baadhi ya watu nan chi kuingia katika hatari na vita,” alisema
Majanjagara.
Wavutana zaidi
Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Liwale,
mkoani Lindi, wamevutana kuhusu uwepo wa nafasi ya mgombea huru katika
Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, wakieleza kuongeza wigo wa
kukithiri vitendo vya rushwa. Mjumbe wa Baraza hilo, Anord Ligai
akiwasilisha maoni ya kundi la kwanza alisema, kuwapo kwa mgombea
binafsi kutasababisha kupata kiongozi asiyekuwa na uadilifu kutokana na
kutokupitia michakato ya kumpata. Abasi Matulilo alisema, katika mambo
saba ya Muungano moja wapo ni vyama vya siasa hivyo kuwapo kwa mgombea
huru kutaligawa taifa.
No comments:
Post a Comment