Zigua simo na njero |
bodaboda |
Miongoni mwa watu waliojikuta katika hali hiyo ni Sadi Mussa, kijana anayejihusisha na shughuli ya biashara ya usafiri wa pikipiki, maarufu bodaboda, katikati ya jiji la Mbeya licha ya kuwa chombo hicho kilimsababishia kuishi miezi mitano bila kuweka chakula cha aina yoyote katika tumbo lake.
Kijana huyu ndiyo anakuwa mtu wa kwanza kumuona mara nilipowasili katika stendi ya Mwanjelwa jijini Mbeya akiwa katika shughuli zake za kutafuta abiria,kovu dogo alilokuwa nalo jichoni ndilo lilikuwa chanzo cha kusimulia mkasa alikutana nao mwishoni mwa mwaka jana.
Mussa (31) anasimulia kuwa licha ya kuendesha pikipiki kwa muda wa miaka tisa, hatosahau namna ambavyo chombo hicho kilivyotaka kukatisha uhai wake na kumrudisha nyuma kimaendeleo.
“Nakumbuka ilikuwa mwezi wa kumi mwaka jana, baada ya jioni ya tarehe 27 nilienda kuangalia chakula mahali ambapo siku zote huwa naenda kula, lakini sikupata nikalazimika kurudi nyumbani nikachukue pikipiki ili niende kutafuta sehemu nyingine ndipo nilipokutana na ajali hiyo ambayo sikuwahi kuifikiria maishani,”anasema Mussa ambaye asili yake ni mwenyeji wa Mtwara.
Anakiri wazi kuwa mwendo wa kasi aliokuwa nao ulimsababisha kushindwa kulikwepa gari dogo lililokuwa linakatiza njia panda, hivyo akajikuta ameliingia na kupoteza fahamu.
“Yani kilikuwa kitendo cha haraka mnno nikashindwa kufanya lolote nikajikuta nipo chini kwa bahati nzuri nilikuwa nafahamika, watu wakajaa eneo la tukio lakini haikunichukua muda nikapoteza fahamu na kuzinduka siku mbili baadaye ambapo nilijikuta nikiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya,”anasimulia Mussa.
Kama ilivyo kwa binadamu wengine Mussa alikumbwa na mshangao wa hali ya juu alipozinduka na kujikuta na uvimbe mkubwa katika kichwa chake,hapo ndipo alipoangusha kilio na kujua kuwa huo ndiyo mwisho wa maisha yake.
Anaeleza kuwa siku ya tatu akafanyiwa upasuaji ambao ulichukua zaidi ya saa tisa, lakini kichwani mwake akiwaza namna ambavyo angeweza kumudu gharama za matibabu akiwa katika hali hiyo ya ugonjwa, ukizingatia kuwa hakuwa na ndugu yeyote jijini Mbeya.
Hofu ya gharama kubwa za matibabu ilimsababisha Mussa kuomba kutoka hospitali ili akaendelee na matibabu nyumbani kitu ambacho kilipingwa na daktari aliyemfanyia upasuaji kwa kuwa hali yake ilihitaji uangalizi mkubwa kwa kipindi cha mwezi mmoja.
“Baadaye nilijulishwa kuwa taya lilivunjika fuvu langu la kichwa lilipata ufa, muda wote wa upasuaji nilishuhudia vyuma vikiingizwa kichwani lakini akili yangu ilikuwa inawaza gharama ningewezaje kuzimudu wakati nikiwa kitandani na kukaa kwa mwezi zaidi hali ingezidi kuwa mbaya sikuwa na mtu yeyote wa kumtegemea,”alisema.
Anasema ilimbidi kumuelezea hali halisi daktari wake ambaye aliguswa
na maisha yake hivyo akamruhusu kurudi nyumbani na kumuahidi kwenda
kumuangalia maendeleo yake kila siku kitu ambacho
kilifanyika,aliruhusiwa na kupewa dawa ambazo zingeendelea kumsaidia.
Anaeleza kuwa alikumbana na ugumu wa hali ya juu aliporudi nyumbani
kwani mdomo wake ulikuwa umefungwa na nyaya zilizomzuia kufuungua hata
kuweza kula na kumeza dawa.“Nilijikuta nikibubujikwa na machozi, kwani wakati huo wazo langu lilikuwa kupona tu na ningewezaje kupona wakati dawa hazipiti mdomoni kwa kuwa nimebanwa,”anaeleza na kuongeza:
“Siku ya kwanza ikapita lakini kesho yake nikajipa moyo nikajaribu kunywa maji nashukuru Mungu yalipita kwenye mwanya uliopo mdomoni kwangu, hakuna hata siku moja niliyofikiria kuwa mwanya unaweza kuwa msaada.”
Baada ya kuona maji yanapita kwenye mwanya Mussa akapata akili ya kuyeyusha dawa alizopewa na kuzinywa kwa mtindo huo,tatizo la njaa likaanza kumnyemelea akaanza kujaribu juisi ambayo nayo ilipita bila wasiwasi kwenye mwanya na hatimaye kufika tumboni.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya Mussa kwa kipindi cha miezi mitano, kuishi kwa kutegemea juisi ambayo alikuwa akinywa maboksi manne yenye ujazo wa lita moja ambazo huuzwa kuanzia Sh2,500 mpaka Sh 2,700 kila boksi.
Haikuwa rahisi kwa Mussa kuweza kumudu pesa yote hiyo katika kipindi chote cha miezi mitano, ilhali hakuwa na kazi yoyote ya kumuingizia kipato zaidi ya kutegemea akiba kidogo ambayo nayo ilianza kuisha kutokana na kutumia zaidi ya Sh 10,000 kwa siku kwa ajili ya kununua juisi.
Anasema hali iliendelea kuwa hivyo mpaka alipotolewa vyuma vilivyoshikizwa kwenye taya na fuvu lake, ndipo alipoanza kujifunza upya kula na kuongea kuwa ilimuwia vigumu kunyanyua mdomo kama ilivyokuwa awali kabla ya ajali.
Baada ya miezi mitano kukatika akalazimika kuingia mitaani kutafuta ridhiki licha ya kuwa hakuwa amepona vizuri, lakini ukata wa maisha ulimsukuma kuchakarika ili aweze kupata pesa ya kulipia kodi na matumizi yake madogomadogo.
Kwa bahati mbaya kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi kabla ya ajali ilifilisika, hivyo akalazimika kutafuta shughuli nyingine na kimbilio la pekee lilikuwa kuendesha bodaboda kazi ambayo anaifanya mpaka sasa.
Maisha mapya ya udereva wa bodaboda
Pamoja na kukutana na ajali hiyo kubwa Mussa amejikuta akijiingiza katika uendeshaji wa bodaboda, ili aweze kumudu kupata kipato kitakachomuwezesha kumudu maisha yake.
“Ukweli ni kwamba sipendi kabisa hata kusikia kuhusu pikipiki, lakini
nitafanyaje na mimi nahitaji pesa nalazimika kufanya kazi hii ili
nijipatie kipato, lakini umakini wangu umeongezeka maradufu kwa kuwa
najua hatari ya chombo hiki ambacho vijana wengi wamekuwa wakikichezea
na kudhani kuwa wamekizoea kupita kiasi bila kujua wanahatarisha
maisha,”anasema na kuongeza
“Hapa nilipo hata nikisikia pikipiki inapita kwa mwendo kasi mwili
wote unanisisimka nakumbuka maumivu niliyopitia, mpaka sasa siamini kama
nipo hai na ninaendesha tena chombo hiki hatari mnno kwa
binadamu,”alisema.Anamaliza kwa kutoa wito kwa Serikali na wanajamii kwa ujumla kuwapa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa bodadoda, kinyume na hapo taifa litaendela kuwapoteza vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.
No comments:
Post a Comment