Monday, 16 September 2013

Magereza zinapofananishwa na jehanamu...nani wa kunyooshewa kidole!?????

Badala ya kuwa ni eneo la mafunzo bora, magereza nchini zinalaumiwa kuharibu zaidi wanaofungwa.Matokeo yake asilimia 25 ya wanaoachiwa au kumaliza kifungo hufanya makosa na kufungwa tena


Dar es Salaam. Jeshi la Magereza Tanzania lilianzishwa rasmi kama idara kamili ya Serikali Agosti 25,1931. Awali, shughuli za magereza zilikuwa sehemu ya jeshi la polisi.
Kimsingi sababu kubwa ya uwepo kwa jeshi hilo sio kutesa, bali kutumika kama mamlaka kamili ya kuwalinda kwa haki wote ambao wanapaswa kutumia jela yaani wafungwa. Azma ni kuwatengeneza ili wanaporudi uraiani wawe jamii bora.
Mtuhumiwa
alaumiwe nani
Kwa maelezo ya wengi wanaotoka kwenye magereza, ni kwamba magereza ni kama jehanamu yaani eneo ambalo maisha ni ya mateso badala ya kutumika kama eneo la mafunzo ili kuzalisha jamii bora zaidi. Baadhi ya wafungwa wanasema kila kitu katika magereza nchini ni kibaya kuanzia sehemu za kulala hadi chakula, huku ikionekana wazi hakuna jitihada za kuboresha hali hiyo.Mikakati mingi ya kuboresha mazingira ya magereza ni kama imekuwa porojo zisizo na utekelezaji.
Hali mbaya ya magereza
Licha ya kauli za waliowahi kufungwa kuelezwa namna hali ya magereza ilivyo mbovu, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama hivi karibuni ilionekana kushtushwa na hali ya maisha ya watu walioko jela nchini. Kwa mfano kamati ilisema kuna msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu.
Kamati hiyo ilisema ilitembelea Gereza la Segerea na kushuhudia hali mbaya ya gereza hilo ambapo msongamano wa wafungwa na mahabusu ulikuwa mbaya.
“Si gereza hili tu magereza yote nchini hali yake ni mbaya wafungwa ni wengi kwa zaidi ya asilimia 23, hii ni hatari sana na inaharibu hata sifa ya nchi yetu,” anasema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa.
Aidha hadi sasa utekelezaji wa adhabu mbadala haufanyiki licha ya Rais Jakaya Kikwete kutoa maagizo ya aina hiyo. Asilimia 90 ya wafungwa na mahabusu waliopo magerezani ni vijana, hivyo kupunguza nguvu kazi ya taifa.
Mbunge wa Namtumbo Vita Kawawa, ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo,anasema hali za magereza ni mbaya kwa kuwa takwimu zinaonesha idadi ya wafungwa nchini ni 36,552 wakati uwezo wa magereza hayo ni wafungwa 29,400.
Mbunge wa viti maalum, Magdalena Sekaya anasema amewahi kushuhudia ukatili wanaofanyiwa wafungwa kwenye gereza la Kilimo, wilayani Urambo, mkoani Tabora.
Anasema ndani ya gereza hilo la wanawake tu, ni jambo la kawaida wafungwa na mahabusu kuvuliwa nguo na kupekuliwa sehemu mbalimbali za maungo yao ya mwili, ikielezwa kuwa ni upekuzi wa kawaida wenye lengo la kuimarisha usalama; anataja wahusika wa unyanyasaji huo kuwa ni askari magereza wanawake.Hata hivyo magereza iliyanusha madai hayo ikisema si ya kweli.

Maisha ya wafungwa
Baadhi ya wananchi akiwemo Suleiman Mhawi, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam anasema “Jeshi la Magereza limekuwa likilalamikiwa mno kuhusu kero mbalimbali, zikiwemo huduma mbovu kwa wafungwa na msongamano mkubwa wa mahabusu. Jamii ya Tanzania inataka kuona viongozi wa magereza wanasimamia kidete kuhakikisha wafungwa kama walivyo watu wengine, wanapata huduma zote zinazohitajika kila siku. Hali kadhalika litakuwa ni jambo la busara kuona msongamano mkubwa ambao umekuwa kero kila mwaka unapunguzwa haraka. Makazi duni ya askari yanapaswa kuboreshwa”.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja, hata hivyo katika hotuba yake baada ya kuapishwa, aliahidi kufanya mengi kwa lengo la kuboresha hali ya magereza na mazingira ya utendaji.
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi ambaye hivi karibuni alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya kufunga mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu, kwenye Chuo cha Maafisa magereza Ukonga, Dar es Salaam anawataka askari magereza nchini kutumia taaluma yao katika kurekebisha tabia za wafungwa siyo kuwatendea ukatili.
Anasema Serikali imeweka adhabu ya kifungo gerezani kwa lengo la kurekebisha tabia ili anapomaliza kifungo awe na tabia nzuri. Waziri anaeleza kutoridhishwa na taarifa zinazoeleza kuwa asilimia 25 ya wanaotoka gerezani hufanya makosa tena na kujikuta wakifungwa tena.
“Mkitumia utaalamu wenu magerezani hakutafananishwa na jehanamu, bali kila atakayeonekana kutenda mabaya katika jamii, ndugu, jamaa na rafiki wa mtu huyo wataona umuhimu wa kumleta gerezani ili abadilishwe tabia,”anaeleza waziri Nchimbi.
Mkuu wa Chuo hicho, Mubarak Simwanza anasema asilimia 25 ya wafungwa wanaoachiwa kwa msamaha wa Rais au wanaomaliza kutumikia adhabu ya kifungo, hurudishwa tena gerezani kwa makosa mbalimbali.
Hata hivyo Simwanza anaeleza kuwa pamoja na mambo mengine, hali hiyo inachangiwa na jamii kutokuwa tayari kuwapokea na kuwakubali watu wanaomaliza kutumikia adhabu ya kifungo.
“Ukiweka kando athari nilizotaja awali, hata jitihada za Serikali kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, zinakwamishwa,” anasema Simwanza.

No comments:

Post a Comment