Ibrahim
Kamwe, mdau wa ngumi na promota wa mchezo wa masumbwi Tanzania, ambaye
pia ndio muandishi wa uchambuzi huu kama sehemu ya kuonyesha picha
kamili ya sekta ya ngumi.
Baadhi yetu tukiwa na umri
wa kuanzia miaka sita nyumbani huwa tunaanza kupewa uzowefu wa kuuza visheti, maandazi,
vitumbua, karanga nk na vikibaki nyumbani hauli chakula mpaka viishe.
Bondia Thomas Mashali, akionyesha mkanda wake.Picha hii haihusiani na kilichoandikwa humu, ila imetumika kwasababu imeelezea sekta ya masumbwi.Nikiwa na maana mabondia wengi wanatoka uswahilini ni watu wa hali duni wengi wetu hatujakalia madawati ya shule wengine tuliojitahidi tumefika darasa la tano au sita kama wazazi walikomaa ndio tunamaliza la saba.
Bondia
Mbwana Matumla, akiwa kwenye matukio yake ya ngumi ulingoni katika
mapambano ya masumbwi. Picha hii haihusiani na kilichoandikwa humu, ila
imetumika kwasababu imeelezea sekta ya masumbwi.
Shuleni
mwalimu mkali, darasani afundishi mpaka usome tuisheni ndio unapata kufundishwa
kidogo na ukishindwa maswali yake viboko vya ghazabu, hapo ndipo tunapoamua
kuachana na shule na kutinga mitaani.
Michezo yetu ni katika
madampo na vichochoroni na tukifikia umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea
tunajua jinsi ya kutafuta pesa kwa kuuza njiwa,kucheza kamari, malani, kuiba
kuku na bata.
Na kwa wale walio watukutu
zaidi kuuza na kuvuta bangi ni sehemu ya maisha ya kawaida tu huku mitaani
kwetu.
Mara nyingi mlo kwetu ni
mmoja tu kiubishoo au kuwa wageni ndio tunakula milo miwili. Katika maisha yetu
muda mwingi tupo huru na michezo kuliko kusoma hasa kolokolo, ngoma, mpira na
ngumi, mpira tunacheza mabarabarani, vichochoroni na madampo wakati ngumi
tunajifundisha katika makamali vichochoroni au uwani kwa kina master begi.
Au tairi limefungwa juu
ya mti tizi linaendelea bila vifanyio vya mazoezi vilivyo rasmi mwendo
mdundo tunasonga na tunashinda au kufanya vizuri katika mashindano yetu
tunayoshiriki na hali yetu duni hihi hii ya kimaisha.
Majina yetu kutangazwa sana
katika vyombo vya habari na kupata umaarufu mkubwa nchini, nchi jirani na
hata nchi za Ulaya, lakini ukibahatika kututembelea na kuangalia tunapoishi na
familia zetu na umaarufu tulionao maisha yetu mabovu yanasikitisha.
Tanzania hakuna sehemu
rasmi za kufanyia mazoezi ya ndani zilizotengwa na serikali kwa ajili ya
raia wake wapenda michezo na kama zipo ni chache katika makambi ya jeshi kwa
masharti magumu kwa raia wa kwawaida.
Siku za nyuma wakazi wa
mjini kama vile kisutu,gerezani na kariakoo walikuwa wanafanya mazoezi pale
anatoglu, siku hizi huwezi kusikia kuna mwanamichezo katokea gerezani au
kariakoo, iliyobaki kwao ni kuuza na kutumia madawa ya kulevya na kukimbizana
na wafanyabiashara wa maeneo hayo, naweza ilaumu serikali kwa kutoendeleza
michezo bali ilishiriki kuuwa kabisa michezo maeneo hayo na mengineyo zaidi.
Kwa sisi tulionza kukuwa
kimchezo Pambano la ngumi likiandaliwa huwa tunalipwa kuanzia shilingi alfu 5
mpaka 20 kwa mapambano haya madogomadogo na iwapo kutakuwa na pambano kubwa na
kupata bahati ya kucheza unaweza lipwa shilingi alfu 40 mpaka laki moja.
Mapambano makubwa yanaweza
kuwa moja,mawili au matatu kwa mwaka hayazidi hapo, haya mapambano madogo
tunaweza pata mawili mpaka sita kwa mwaka.
Msiwaone mabondia wakicheza
mkadhani wana kipato kikubwa la hasha, ni wale tu wachache waliobahatika kupata
wadhamini au waratibu wenye uwezo wa kipesa ndio kidogo hutoka.
Kwa sisi wengine ukiangalia
elimu ya kusoma hatuna kazi hakuna na mchezo wa ngumi tunaupenda na pengine
tuna vipaji na kwa kufanya vizuri katika mapambano yetu, hivyo mchezo ndio huwa
kama ajira zetu kwa sababu tunapata chochote kidogo kupitia mchezo huo kuliko
kuiba au kukimbizana na mapolisi katika kamari na kuishia jela.
Kwetu sisi mabondia huona
ni jambo la kifahari na hufurahi mno pale tu tunapopata pambano la nje ya nchi
na hufurahia kupanda ndege na vile vimisosimisosi tunavyopata tukiwa mahotelini
ugenini, tukihadisiana mambo ya safari uswahilini kwetu tunahisi tunakosa mambo
mengi ya raha.
Hapo ndipo mawakala wa ngumi
hutupata na mabondia huwa wanadiriki kukubali kwenda kucheza popote tukijua
tutapanda ndege tunakula raha bila kujali na wala kuhoji tuendako
tutalipwa kiasi gani cha pambano nitakalocheza wala kujua usalama wangu.
Ukiangalia umbumbumbu na
maskini tulionao mabondia,hapo wajanja wenye pesa zao, wafanyabiashara na
baadhi ya viongozi wanatumia udhaifu tulionao mabondia kutuhadaa kwa kutupatia
safari za nje za kimichezo au matembezi ya kwenda kufanya mazoezi ughaibuni na
hatimae kutubebesha mihadarati(madawa ya kulevya) bila kujua kwa
kutuwekea katika mizigo tunayosafiri nayo.
Pindi kuna baadhi ya
wafanya biashara hao wenye pesa zao hutuweka wazi wakati unaenda pigana umbebee
mzigo wake na atakulipa pesa nyingi ,hapo ndipo tunapobanwa ukiangalia nyumbani
tunalalia telemka tukaze tunashindia tembele mlo mmoja msosi wa kengele
tena kwa masimango, mfukoni sina kitu na wala sina kazi itakayonipatia pesa ya
kula kwa sasa (hapo sijaingiza mambo ya kodi) demu wangu namlinda vipi.
Hii njaa na umaskini tulio
nao mabondia,hapo ndio vigogo wanapoamua kututumia kwa kutubebesha madawa
ya kulevya kusafirisha nje wakijua wazi hatuwezi kataa kutokana na dhiki tuliyo
nayo, tutakubali tu kwani hakuna apendae kulala njaa , kulala pachafu au
kuvaa midabwada.
’siwezi acha dili la pesa
kama hili wakati jina langu kubwa kila kona linatajwa mitaani na vyombo vya
habari lakini mimi binafsi nauli ya daladala sina,siku ya tatu leo nakula mlo
mmoja kwa siku, watoto hawapo katika hali nzuri, mazoezi yenyewe sifanyi kwa
raha nafikiria nitapata wapi mshiko, leo unaniletea ishu ya pesa niikatae si
nitakuwa kichaa’wadau wenzangu wa ngumi ,wapambe wao.
Na walio karibu na sisi
mabondia wana nguo za bei kubwa wanapendeza , wana magari, ukiangalia mimi
bondia ndie mtendaji wao mkuu nipo ovyo sina kitu mfukoni wala tumboni madeni
kibao yaani majanga matupu.
Ushauri wangu kwa serikali
au taasisi zinazohusika na wanaolichukia jambo hili kiukweli maana wengine
hujifanya kulichukia mdomoni pembeni ndio watendaji wakuu wa kuwatumia
wanamichezo au wasanii kwa faida zao.
Mabondia au wanamichezo tuboreshewe
maeneo yetu ya michezo ikiwemo katika vilabu vyetu na maeneo ya mazoezi, vifaa
viongezwe ikiwezekana kodi ya vifaa vya michezo ipunguzwe ili viwe vingi nchini
mabondia wasibabaike na vya kuazima au kuangalia katika tv vifaa nya wenzetu.
Serikali iwajali mabondia, isaidie kudhamini semina za walimu wa ngumi ili
wawaongoze vema vijana wao.
Magym ya makusudi yajengwe
na maeneo ya wazi wasigawane wenye pesa na viongozi kwa faida zao wajenge
sehemu za michezo ya ndani(indoor), na kama pia itatumika njia ya kutoa
madarasa matupu katika mashule yetu kwa ajili ya kutuachia sehemu ya mazoezi ya
jioni itasaidia sana kukuza mchezo na walimu wenye taaluma kufundisha vizuri
kuliko mabondia kufundishana vichochoroni na kutokuwa na nidhamu ya mchezo wala
maisha.
No comments:
Post a Comment