|  | 
| SIMBA | 
|  | 
| Zigua Simo na Njero | 
Dar/Mikoani. Kukithiri kwa rushwa miongoni mwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi nchini, kumesababisha silaha ndogondogo hususan bastola kumilikiwa na watu wasio na sifa nchini.
|  | 
| Bastora | 
|  | 
| Fedha...Biashara | 
Hivi sasa hata vibaka ambao awali walikuwa 
wakitumia visu na mbao za misumari kupora mali za watu, sasa wanafanya 
uhalifu huo kwa kutumia bastola.
Mbali ya vibaka kumiliki bastola, wahamiaji haramu
 walioko ndani ya mipaka ya Tanzania inayopakana na Rwanda, Burundi na 
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanadaiwa kuingiza silaha nzito, 
ambazo zinatumika kwa ajili ya matukio ya kihalifu.
Jinsi silaha zinavyopatikana
Uchunguzi unaonyesha moja ya njia ambayo imekuwa 
ikitumika watu wasiokuwa na sifa kupata bastola au bunduki ni kutumia 
mawakala au baadhi ya maofisa polisi, waliopo katika mikoa mbalimbali 
ambao huwatafutia vibali vya kumiliki.
Utaratibu wa kawaida ni kwamba waombaji wanaotaka 
kumiliki silaha ni lazima wajadiliwe katika kamati za ulinzi na usalama 
za mtaa au kijiji, wilaya na mkoa na kuhojiwa ili kujiridhisha kama 
mwombaji ana sifa.
Mkoa wa Kilimanjaro
|  | 
| Silaha za rashasha | 
“Unataka kibali cha kumiliki bastola? Una milioni 
moja na nusu nikuunganishe na jamaa Dar anakufanyia process (mchakato) 
zote anakuletea kitabu,”alisema kijana mmoja jina tunalihifadhi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, baadhi ya 
maofisa wa Jeshi la Polisi makao makuu na wale waliopo mikoani, 
wamegeuza suala la kumilikisha watu silaha kama mradi wa kujitajirisha.
“Tatizo la nchi hii ni corruption (rushwa) kwa 
sababu unajiuliza hivi hawa vijana wadogo kabisa wanamiliki bastola na 
hawakujadiliwa kwenye kikao chochote,”alidokeza mfanyabiashara mmoja.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wapo wanaojiita wafanyabiashara, 
lakini ni matapeli wa kimataifa nao wamepewa vibali vya kumiliki bastola
 na wakati mwingine huzionyesha waziwazi wakiwa baa.
“Ufyatuaji wa risasi siku hizi umekuwa 
holela…ninavyofahamu ukifyatua hata risasi moja, lazima uandikishe 
maelezo polisi ulifyatua kwa sababu zipi siku hizi lakini hilo 
halifanyiki,” ilidokezwa.
Inadaiwa kuwa kutokana na kuwapo kwa ulegevu wa 
vyombo vya dola hususan Polisi, baadhi ya wamiliki wa bastola hizo 
wamekuwa wakizikodisha kwa majambazi ambao huzitumia katika uporaji.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ulegevu huo katika 
kudhibiti matumizi ya silaha, kumetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki 
kukodisha bastola zao na kurudishiwa baada ya matukio pasipo 
kugunduliwa.
Dar es Salaam
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa 
kuongezeka kwa idadi ya watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria 
jijini Dar es Salaam, kumeongeza matukio ya uhalifu.
Baadhi ya watu ambao wapo karibu na maofisa wa 
polisi makao makuu wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwatafutia watu 
vibali vya kumiliki silaha.
Watu hao wamekuwa wakijipatia Sh600,000 hadi Sh900,000 kwa kibali kimoja cha kumiliki silaha.
Hali hiyo imesababisha wahalifu wengi wakiwamo vibaka mitaani kumiliki silaha ambazo wanazitumia kupora watu mitaani.
Mussa Radhamn Mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam
 anasema hali ni mbaya, hivi sasa hata vijana wasiokuwa na kazi 
wanamiliki silaha.
Alisema hivi sasa huwezi kupita uchochoroni kuanzia saa 4:00 usiku, lazima utakutana na vibaka wakiwa na bastola.
Wahamiaji haramu
Mkoa wa Kagera
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, 
mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Ngara alisema kuwa silaha nyingi hasa 
bunduki za rashasha (sub machine gun) zinanunuliwa nchini Burundi.
“Wakati kambi za wakimbizi za Lukole zikifanya 
kazi, silaha zilikuwa zikipatikana kwa wingi, lakini kwa sasa kwa kuwa 
wakimbizi hao wameondoka, silaha zinafuatwa hukohuko,” alisema na 
kuongeza:
“Kuna watu wana uhusiano na wenyeji wa Burundi, 
basi wanaziagiza tu… bunduki moja ya SMG ni kama Sh200,000 wanakuletea. 
Unajua kule kwa sasa kuna njaa kali kwa hiyo yale makundi ya waasi 
yalikuwa na silaha nyingi hayana jinsi ila kuziuza ili kujikimu 
kimaisha.”
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Idara ya 
Uhamiaji katika mpaka wa Rwanda na Tanzania (Rusumo), Mahirande Samuel 
alisema ni vigumu kudhibiti wahamiaji haramu hasa katika mpaka wa 
Burundi kwani ni mkubwa na uwezo ni mdogo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, 
Philip Kalangi alisema wahamiaji hao wamekuwa wakishiriki katika matukio
 ya uhalifu wakishirikiana na wenyeji.
“Wahamiaji haramu wamechangia sana katika matukio 
ya uhalifu. Wanaharibu mazingira kwa kuchoma misitu, kuchoma mkaa, 
kupasua mbao na ujangili. Tunafaya juhudi kutekeleza agizo la Rais la 
kuwaondoa nchini na kazi inaendelea vizuri,” alisema na kuongeza:
“Hadi sasa tumeshakamata silaha aina ya bunduki za
 gobori 50 ambazo zimesalimishwa, ila wanaosalimisha hatuwajui maana 
huzitupia kwa viongozi wa vijiji na kukimbia. Silaha tulizokamata ni 
mbili ambazo ni SMG ikiwa na risasi 70 na gobori moja.
Akizungumzia tukio la Juni 15, mwaka huu, ambapo 
mabasi mawili yalitekwa na majambazi na kuwapora abiria katika pori la 
Kasindaga, Kamana Kalangi alisema bado uchunguzi unafanyika, lakini kuna
 kuhusika kwa wahamiaji haramu wakishirikiana na wenyeji.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Fabian Massawe 
alisema kuwa majeshi ya Tanzania kwa sasa yanajipanga kwa ajili ya 
operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu mkoani humo.
Kwa sasa majeshi yetu yanajipanga kwa ajili ya operesheni, alisema na kuongeza:
Kama Serikali itasaidia tunataka operesheni hii 
iwe endelevu, ila hatuwezi kuweka kambi za jeshi mipakani kwa sababu 
sheria za kimataifa haziruhusu. Operesheni hii ni kwa wahamiaji wa nchi 
zote zinazotuzunguka. Nashangaa Rwanda peke yao wanalalamika.
Alisema kuwa hivi sasa wahalifu wengi wanatumia bastola kupora watu mitaani tofauti na zamani walikuwa wakitumia mapanga.
Mkoa wa Mwanza
Uchunguzi unaonyesha kuwa watu wengi wamepata silaha kwa njia ya haramu.
Baadhi ya watu wamenunua kutoka kwa wakimbizi na 
wengine wakipata vibali vya kumiliki kupitia kwa mawakala au maofisa wa 
polisi wasiokuwa waaminifu.
Lugwecha Makune Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, alisema kuwa hali ya uhalifu mjini Mwanza hivi sasa inatisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu 
alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo alisema yupo nje ya ofisi atalitolea 
ufafanuzi baadaye.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la 
kuwarudisha makwao wahamiaji hao, huku idadi yao ikifikia zaidi ya 
10,000 waliorudi kati ya 50,000 wanaokadiriwa kuwepo nchini.
Wiki hii Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel 
Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema
 operesheni ya kuwandoa kwa nguvu wahamiaji waliobaki itakuwa ya 
kushtukiza.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema atafutwe baadaye.
Hata hivyo, alipopigiwa simu alisema afuatwe ofisini kwake kulizungumzia, lakini alipofuatwa alisema alikuwa na kazi nyingi.
Maoni ya watu mbalimbali
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
 (UDSM), Profesa Humprey Moshi alisema kuongezeka kwa matukio ya watu 
wanaotumia silaha, ni matokeo ya ukosefu wa amani katika nchi za jirani 
ambao umesababisha wahalifu kuingia nchini kwa njia za kificho wakiwa na
 silaha.
Moshi anasema ukiritimba katika upatikanaji silaha serikalini si
 sababu ya watu kununua silaha kwa njia za siri, bali ukosefu wa ajira 
kwa vijana na mmomonyoko wa maadili ndivyo vilivyoifikisha hali ya 
kutokuwa na usalama mahali ilipo leo.
“Taratibu za upatikanaji wa silaha serikalini siyo
 tatizo, migogoro katika nchi jirani ndiyo inayofanya silaha zipatikane 
kwenye mipaka yetu,” anasema.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), 
Profesa Tolly Mbwete alisema suala la upatikanaji silaha haramu si la 
Tanzania peke yake, nchi inapaswa kushirikiana na nchi zote na kushauri 
serikali za mitaa kushirikiana na vyama vya siasa kudhibiti tatizo hilo.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 
Profesa Gaudence Mpangala alisema upatikanaji wa silaha kiholela 
unatokana na kubadilika kwa mfumo wa maisha na kwamba baadhi ya watu 
siku hizi wanamiliki silaha kama njia mojawapo ya kujipatia fedha kwa 
njia za uhalifu.


No comments:
Post a Comment