Tembo |
Ni saa nne asubuhi, asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji cha Chikunja, wilayani
Masasi, wameshawasili kwa Binti Palanga, wakinywa pombe aina ya gongo. Wengine wameketi chini ya mkorosho wakinywa chibuku, na baadhi wapo katika kikundi wakishirikiana kopo lililojaa pombe maarufu ya wanzuki.
Si kijiji cha Chikunja pekee, haya ndiyo maisha ya
wakazi wa maeneo mengi nchini Tanzania ambao takwimu zinaonyesha
wanakunywa zaidi pombe za kienyeji kuliko wale wanywaji wa pombe
nyingine zinazotengenezwa viwandani.
Pia, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO)
zinaonyesha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye wanywaji
wengi zaidi wa pombe ukilinganisha na nchi nyingine.
Miongoni mwa nchi 55 za Afrika zilizo chini ya
uangalizi wa WHO, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanywaji
wengi zaidi wa pombe baada ya Nigeria na Uganda. Nchi nyingine zenye
kiwango kikubwa cha wanywaji ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
Kenya, Angola na Afrika Kusini.
Hata hivyo takwimu hizo za WHO, licha ya kuonyesha
kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye wanywaji wengi wa pombe,
takwimu hizo ziliweka wazi kuwa, asilimia kubwa ya Watanzania hao,
wanakunywa pombe za kienyeji au kwa jina jingine ‘mataputapu’.
Kwa mfano, katika wanywaji hao, asilimia 86
wanakunywa pombe za kienyeji kama wanzuki, chibuku, rubisi, mbege,
dadii, choya, moonshine, banana na gongo wakati ni asilimia 10 tu
wanaokunywa bia na asilimia moja wanakunywa mvinyo wa viwandani, huku
asilimia tatu wakinywa pombe nyingine kali zilizotengenezwa viwandani.
Kwa mchanganuo huo, wanaokunywa pombe za viwandani ni asilimia 14 tu ya wanywaji wote.
Dk Andrew Kitua wa Hospitali ya Hubert Kairuki
anasema baadhi ya pombe huchanganywa na vilevi vyenye hatari kiafya kwa
mfano anasema, methanol, ethanol au furfural inapozidi husababisha upofu
na haitakiwi kunywewa na binadamu.
Anasema, kwa kawaida pombe za kienyeji
hutengenezwa kwa kusindika nafaka, na nafaka hizo zinapochachushwa
hutengeneza vilevi(alcohol).
Anasema hata hivyo kiwango cha ‘alcohol’ hicho
kimetofautiana kulingana na aina ya nafaka iliyotumika, kiwango cha joto
kilichotumika kusindika na muda uliotumika kuchachusha pombe hiyo.
Pamoja na madhara ya vilevi, Mfamasia katika
Hospitali ya Amana, Charles Lymo anasema, tatizo lingine linalosababisha
madhara kwa wanywaji wa pombe za kienyeji ni aina ya unywaji na namna
ya upikaji.
“Kuna pombe zinachanganywa na hamira, hamira
zenyewe hazina kipimo, huwezi kujua hamira hiyo inaweza kuleta madhara
makubwa kwenye mwili wa binadamu,” anasema.
Anaongeza na kusema kuwa aina ya unywaji wa pombe za kienyeji
husababisha magonjwa ya kuambukiza, kwa mfano, kopo moja la mbege huweza
kutumiwa na watu zaidi ya kumi au mrija mmoja waweza kutumika na watu
wengi jambo ambalo linaweza kusababisha maambukizi ya kifua kikuu.
“Lakini pia, maji yanayotumika kutengeneza wakati
mwingine yana vijidudu vya amoeba au minyoo, wanywaji wengi hupata
maradhi haya na kuharisha” anasema Mfamasia Lymo.
Pia, ripoti hiyo imeonyesha kuwa, bara la Afrika
linaongoza kwa kuwa na wanywaji sugu wa pombe duniani ambapo asilimia 25
kati yao ni wale wanaokunywa kupita kiasi.
Utafiti uliofanywa na Dk Joseph Saria na wenzake
kuhusu kiwango cha pombe za kienyeji na madhara yake kiafya nchini
Tanzania, umeonyesha kuwa, pombe nyingi za kienyeji zinachanganywa na
kemikali ambazo zina madhara ya kiafya kwa wanywaji.
Kwa mfano pombe kama choya, dadii, mnanasi, mbege,
moonshine na gongo mchanganyo wake huzalisha sumu kama Methanol,
Butanol, Acetaldehyde na Furfural.
Katika utafiti huo uliochapishwa Julai mwaka jana
katika Jarida la Sayansi(TAJNAS) imeelezwa kuwa unywaji wa pombe hizi za
kienyeji unasababisha maradhi ya saratani hasa ya koo na mdomo , ini,
wakati pombe zenye kiwango kikubwa cha furfural zinatajwa kuwa na sumu
inayosababisha uvimbe katika ubongo, maradhi ya ini na figo.
“Pombe nyingi za kienyeji huchanganywa majumbani
na pasipo kupimwa hivyo uwezekano wa kuwa na sumu kali zenye madhara ni
mkubwa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa Watanzania wengi
hukimbilia pombe za kienyeji kwa sababu ya unafuu wake wa bei,
ukilinganisha na pombe zinazotengenezwa viwandani ambazo ni ghali.
Lakini pia, utafiti huo ulionyesha kuwa pombe za
kienyeji hazitengenezwi vijijini pekee, bali hutengenezwa kwa wingi
katika vitongoji vya miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na
Mwanza.
Ingawa Tanzania kuna sheria ya ununuzi wa pombe
ambapo pombe inaruhusiwa kuuzwa kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 na
kuendelea, hata hivyo sheria hii haihusiki au haitekelezwi huko vijijini
ambako kuna wanywaji wengi zaidi na inasemekana kuwa watoto wa miaka 10
ambao tayari wengi wao ni walevi wa pombe hizo za kienyeji.
Pia, unywaji huo unashamiri zaidi vijijini kwa
sababu sheria nyingi zinatekelezwa mjini kwa mfano sheria ya kiwango cha
pombe kwenye damu pindi mtu anapoendesha gari ni asilimia 0.8 au umri
wa wauzaji wa pombe katika vilabu. Lakini kwa vijijini sheria hizo
hazifuatiliwi.
Chui |
Twiga |
WHO inaeleza kuwa madhara ya pombe kiafya
husababisha vifo vya watu milioni 2.5 kila mwaka, ambapo kati yao,
vijana 320,000 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 29 hupoteza maisha kwa
magonjwa yanayosababishwa na unywaji wa pombe.
Pombe inaelezwa kuwa ni sababu kuu ya tatu duniani kwa kusababisha maradhi na pia ni chanzo cha matatizo mengi ya kijamii kama uvivu, mashambulizi, kutelekeza familia na husababisha watu kufanya ngono zisizo salama.
Pombe inaelezwa kuwa ni sababu kuu ya tatu duniani kwa kusababisha maradhi na pia ni chanzo cha matatizo mengi ya kijamii kama uvivu, mashambulizi, kutelekeza familia na husababisha watu kufanya ngono zisizo salama.
No comments:
Post a Comment